HATIMAYE michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya maarufu kama Euro imeaanza kutimua vumbi jana Juni 11 ambapo miamba ya soka barani humo Italia ilipepetana na Uturuki katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi. mchezo ambao ulimalizika kwa Italia kuwafunga Uturuki mabao 3-0.
Watoto wa Malkia Elizabeth yaani England wataanza mbio za kuwania ubingwa huo kwa kumenyana na Croatia jumapili Juni 13 mwaka huu kwenye dimba la Wembley.
Mashindano ya EURO 2020 yanafanyika mwezi Juni mwaka 2021 baada ya kuahirishwa mwaka jana kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona.
Kwa mujibu wa shirikisho la soka la Ulaya, limeagiza kila timu inaruhusiwa kuwa na wachezaji 26 katika vikosi vyao kutoka idadi ya kawaida ya 23. Idadi ya wachezaji itabidi kuwa 23 siku ya mchezo ambapo mwisho wa kuwasilisha majina ulikuwa tareje moja mwezi Juni mwaka huu.
Hata hivyo timu zinaruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wa vikosi vyao kabla ya kuanza mashindano hayo, endapo kutakuwa na wachezaji walioumia wakati wa maandalizi hivyio kuondolewa kikosini na kuitwa wengine.
Kabla ya michuano hiyo baadhi ya timu zimecheza michezo ya kirafiki, ambapo England wao walimenyana na Romania kujipima ubavu na kumpa nafasi kocha wao Gartehn Southgate kuimarisha timu hiyo kabla ya kuanza mashindano. Lililo mjadala kwa sasa ni namna kikosi hicho kilivyojaa damu change huku mchezaji mwenye umri mkubwa akiwa ni Kyle Walker akiwa na miaka 31.
TANZANIASPORTS katika tathmini yake inaonesha asilimia 99 ya kikosi cha England kina wachezaji chipukizi zaidi kuliko wakati wowote ambao timu imeshiriki mashindano iwe Fainali za Kombe la Dunia au Euro ya miaka ya nyuma. Southgate anaonekana kitengeneza kikosi cha chipukizi ambacho kimetokana na vijana wengi waliounda timu ya taifa ya vijana chininya miaka 20.
Kikosi cha England kinaundwa na; MAKIPA:Dean Handerson (Manchester United), Sam Johnstone (West Brom) na Jordan Pickford(Everton).
MABEKI; Ben White (Brighton), Ben Chilwell(Chelsea), Conor Coady(Wolves, Reece James (Chelsea),Harry Maguire(Manchester United), Tyrone Mings(Aston Villa), Luke Shaw(Manchester United)John Stone(Manchester City), Kieran Trippier (Atletico Madrid), Kyle Walker (Manchester United).
VIUNGO; Jude Bellingham (Borussia Dortmund),Jordan Henderson(Liverpool),Mason Mount(Chelsea),Kalvin Philips(Leeds United), Declan Rice(West Ham).
WASHAMBULIAJI; Dominic Calvert-Lewinbg (Everton), Phil Foden (Manchester City), Jack Grealish (Aston Villa), Harry Kane(Tottenham Hotspurs), Marcus Rashford(Manchester United), Bukayo Saka (Arsenal), Jadon Sancho (Borussia Dortmund) na Raheem Sterling(Manchester City).
England wametajwa kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi ya kunyakua ubingwa wa Euro 2020 ikiwa chini ya kocha ambaye aliinyima nafasi ya kusonga mbele katika fainali za mwaka 1996 alipokuwa mchezaji wa Three Lions, Gareth Southgate.
Katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ujerumani penalty iliyopigwa na kiungo wa England Gareth Southgate ilikwama mikononi mwa mlinda mlango mahiri Andre Kopke ambaye wakati huo umahiri wake ulifananishwa kama ana mikono 1000 ya kuokoa michomo. Machozi ya Waingereza yalikuwa makubwa wakati huo, ikizingatiwa fainali hizo ziliandaliwa katika ardhi yao. hivyo ndoto zao za kunyakua kombe hilo kwenye ardhi yao ziliyeyuka kama barafu kwenye kilele cha mlima Kilimanajri nchini Tanzania.
Na sasa Gareth Southgate ndiyo kocha mkuu wa England. Anawaongoza Waingereza kwenye mbio za kunyakua taji hilo, na bila shaka amepania kufuta machozi ya washabiki na wananchi wan chi hiyo ambao wanakumbuka tukio la kufeli jaribio la kuitwaa taji hilo mwaka 1996.
Southgate ametaja kikosi ambacho kimesifiwa kujali damu change zenye uchu pamoja na kuwekeza kwa kikosi cha muda mrefu kwa nchi hiyo. Uteuzi wake umekuwa tofauti na makocha wengi wa England ambao hukumbwa na shinikizo la kuwachagua wachezaji nyota au wenye umri mkubwa kulingana na uzoefu wao.
Sasa Southgate amekuwa tofauti na hilo ndilo linaleta mjadala ikiwa watoto wa Malkia watamudu kutwaa kobe hilo wakiwa na kikosi kichanga?
England wamepangwa kundi D pamoja na Croatia, jamhuri ya Czech na Sctoland. Hilo ni kundi la majirani wawili England na Scotland ambazo zinaunda muungano wa falme za Uingereza.
Makundi mengine ni; Kundi A: Italia, Uswisi, Uturuki na Wales. Kundi B; Ubelgiji,Urusi,Denmark na Finland, Kundi C: Ukraine,Uholanzi,Austria na Macedonia kaskazini. Kundi D: England, Croatia, Czech Republic, Scotland,
Kundi E: Hispani , Poland, Sweden na Slovakia. Kundi F: Ujerumani, Ufaransa, Ureno na Hungary. Kundi F ndilo linatajwa kuwa la kifo ambako vigogo pekee watachuana kufuzu kwa hatua ya 16, ambapo linajumuisha bingwa mtetezi Ureno.
Kabla ya kuanza mashindano hayo England imecheza mechi za kirafiki dhidi Poland mwishoni mwa mwezi Machi walipibuka na ushindi 2-1 na Romania mwanzoni mwa mwezi huu.
Southgate alishakaa wiki mbili za kukaa na kikosi chake kuelekea mashindano hayo yanayofanyika katika majiji 11 tofauti ikiwa ni kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
England hawatakuwa na nafasi ya kusafiri kwani mchezo wao wa kwanza watacheza kwenye uwanja wa Wembley dhidi ya Croatia. Mchezo huo ni kama wa kisasi kwa England ambao walitolewa katika hatua ya nusu fainali na Croatia miaka mitatu iliyopita kutokana na bao la dakika za nyongeza la Mario Mandzukic.
Juni 18 England watakuwa na kibarua kingine cha kupepetana na wapinzani wao wa jadi Scotland kwenye dimba la Wembley. Mchezo huo ni kama unavyozikutanisha Zanzibar na Tanzania Bara kwenye mashindano yua Chalenji. Mwaka 1872 walicheza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ambao ulimalizika kwa suluhu. Timu hizo zilikutana tena mwaka 2017 ambapo Harry Kane aliiffungia bao la ushindi nchi yake katika muda wa ziada.
Mchezo wao wa tatu utakuwa Juni 22 ambapo watachuana na Jamhuri ya Czech ambao utachezwa kwenye dimba la Wembley. England ina njia tatu za kufuzu hatua ya pili, kumaliza kinara wa kundi, kushika nafasi ya pili katika kundi lao, na kuwa mshindi wa tatu mwenye matokeo mazuri (best third place teams).
Njia ya kwanza inaonekana kuwa muhimu na yenye uhakika zaidi. kama watashinda uongozi wa kundi D watachuana na mshindi wa pili wa kundi F linalojumuisha Ufaransa,Ujerumani,Ureno na Hungary. Ikiwa watashika nafasi ya tatu ya matokeo mazuri watapangwa kucheza na mshindi wa pili wa kundi E.