Wakati mashindano ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani yalianza jana hapa, wachezaji watatu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wanasakwa na klabu za Ulaya, imedokezwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini hapa juzi na jana, klabu 12 za Ulaya zimetuma mawakala wao kuwafuatilia wachezaji hao watatu wa Bongo, ambao taarifa zao zimeanza kuzagaa Ulaya.
Mmoja wa mawakala anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Said Chano, alisema kuwa wachezaji watatu wa Stars ndio wanafuatiliwa kwa karibu sana na klabu hizo 12 za Ulaya.
“Klabu 12 za Ulaya zinaifuatilia kwa karibu sana Stars, lakini wako wachezaji watatu, ambao ndio tunawaangalia sana ,“alisema wakala huyo.
Hata hivyo, pamoja na kutowataja majina wachezaji hao wa Stars wanaofuatiliwa lakini mmoja wapo ni Mrisho Ngassa wa klabu ya Yanga, ambaye hivi karibuni klabu yake ilimtilia ngumu kwenda kufanya majaribio na klabu moja ya Norway ili kucheza soka la kulipwa.
Wakala huyo wa FIFA kutoka Senegal alisema kuwa wachezaji hao wamezivutia sana klabu za Ulaya, na tayari taarifa zao ziko Ulaya na zimewavutia sana .
Taarifa zisizo rasmi zinadai kuwa mbali na Ngassa, wengine wanaotolewa macho na mawakala hao wa Ulaya ni Jerry Tegete na Kigi Makassi.
Pia, alisema kuwa mashindano hayo yatakuwa nafasi tosha kwa wachezaji wa Tanzania kutengeneza majina yao ili kupata soko nje ya nchi.
Aliwapongeza CAF, Shirikisho la Soka la Afrika, kwa kuandaa mashindano hayo kwani yatasaidia sana kuwatangaza wachezaji wenye vipaji, ambao hawana uwezo wa kuonekana kirahisi nje.
Alisema Stars ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, na hata Senegal, ambayo jana usiku ilitarajia kucheza na Stars, inaihofia Tanzania.
Alisema kuwa endapo wachezaji wa Stars watakuwa makini wanaweza kufika mbali katika mashindano hayo.
Stars iko katika Kundi A pamoja na Zambia , Senegal pamoja na wenyeji Ivory Coast.
- SOURCE: Nipashe
Comments
Loading…