in , ,

Wasifu wa timu zinazoshiriki AFCON 2013

*Zipo zilizowaliza vigogo wa soka Afrika

*Zatamba kwa majina ya wanyama, ndege

 

Macho na masikio yanaanza kuelekezwa taratibu Afrika Kusini, ambako vikosi vya timu zinazoshiriki Michuano ya 29 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) vimeanza kuwasili.

Fainali hizi zinafanyika Afrika Kusini baada ya kuhamishwa kutoka kwa mwenyeji wa awali, Libya, kutokana na ukosefu wa usalama, kwani palifanyika mapinduzi yaliyomng’oa kiongozi wao, Kanali Muammar Gaddafi na bado hakujatulia.

Afrika Kusini walipewa nafasi ya kuandaa fainali hizi badala ya Libya, wakibadilishana, ambapo sasa Libya wataandaa fainali za mwaka 2017 ambazo ilikuwa Afrika Kusini wawe wenyeji. Morocco wataandaa zile za mwaka 2015.

Michuano hiyo inayoanza Januari 19 inashirikisha timu za taifa nchi 16, zilizopigana kiume na kujichuja kutoka kundi la timu 47.

Hata hivyo, Afrika Kusini hawakulazimika kutafuta kufuzu, kwa uenyeji wao ilikuwa lazima waingie kwenye fainali, kama ilivyo kwenye kombe la dunia.

Timu 46 zilizobaki ziliingia kwenye raundi tatu za kutoana jasho kupigania kufuzu, zikicheza nyumbani na ugenini katika makundi. Tuangalie wasifu wa timu zinazoshiriki:

Afrika Kusini – Bafana Bafana – Wavulana

Tukianza na wenyeji Afrika Kusini, timu yao huitwa Bafana Bafana na sifa kubwa zaidi katika katika medani ya soka ni kutwaa kombe hili mwaka 1996 walipoliandaa kwa mara ya kwanza.

Afrika Kusini iliandaa pia Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2010, lakini Bafana Bafana haikuvuka raundi ya kwanza.

ZambiaChipolopolo – Risasi za Shaba

Zambia wanaingia kwa Mzee Madiba kutetea kombe walilotwaa mwaka jana, hali ni tete, hata kocha Mfaransa Hervé Renard anakiri.

Zambia, kwa jina maarufu, Chipolopolo, hawajafanya vyema kwenye mechi za majaribio.

Baada ya uhuru timu yao iliitwa ‘KK 11’, kwa heshima ya jina la Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.

Mwaka 1991 walipoanza siasa za vyama vingi, timu ilibadilishwa jina na kuitwa Chipolopolo, yaani risasi za shaba, kwani Zambia ni wazalishaji wakubwa wa madini hayo.

Ni risasi hizo zilizowamaliza Ivory Coast kwenye fainali ya mwaka jana. Zambia wana kumbukumbu ya kuwafunga Italia mabao 4-0 kwenye michuano ya Olimpiki mwaka 1988, ambapo Kalusha Bwalya alifunga mabao matatu.

Ghana – Nyota Nyeusi

gyan

Black Stars wa Ghana wanaingia kwenye mtanange wa Afrika Kusini wakiwa na rekodi kubwa kwenye soka. Wamefuzu mara tano mfululizo michezo ya Olimpiki ya wakubwa.

Wameshinda mara nne kombe hili la AFCON na kuwa washindi wa pili mara nne pia. Walipata tuzo ya timu iliyoboreshwa zaidi ya Fifa mwaka 2005 na 2006 walifika raundi ya pili ya Kombe la Dunia chini ya kocha Ratomir Dujković.

Katika fainali za mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini, Black Stars walikuwa timu ya tatu ya Afrika kutinga robo fainali za Kombe la Dunia.

Nigeria – Tai wa Kijani

Nigeria wanaingia wakijua ndio waliowahi kufika nafasi ya juu zaidi Afrika katika ngazi za ubora wa soka kwa Fifa, kwani Aprili 1994 walikuwa wa tano.

Green Eagles (Tai wa Kijani) hao wameshinda kombe la AFCON mara mbili na pia kufika raundi ya 16 bora ya Kombe la Dunia mara mbili.

Mali -Tai

Mali wanaojulikana kama Les Aigles (Tai), walikaribia kutwaa kombe la AFCON mwaka 1972, lakini wakafungwa na Kongo mabao 3-2 kwenye mechi ya fainali.

Hawakufuzu tena kwa mashindano hayo hadi 1994 walipofika nusu fainali, ambacho ni kilele cha mafanikio walichokifikia mara tatu tangu hapo, yaani 2002, 2004 na mwaka jana.

Mali ina rekodi kubwa ya kukomboa mabao ya karibuni zaidi, ambapo mwaka 2010 walitoka nyuma wakiwa wamefunga mabao 4-0 na Angola hadi kumaliza mechi kwa sare ya 4-4.

Tunisia – Tai wa Carthage

Afrika Kusini kuna tai wengine, nao ni Tunisia – Les Aigles de Carthage, yaani Tai wa Carthage. Hawa wamefuzu mara nne katika Kombe la Dunia, mara ya kwanza ikiwa mwaka 1978 nchini Argentina.

Tunisia ndiyo timu ya kwanza ya Afrika kushinda mechi kwenye kombe hilo, kwani waliwakung’uta Mexico mabao 3-1.

Waliwatoa jasho mabingwa watetezi enzi hizo, Ujerumani Magharibi na kwenda nao suluhu. Walifuzu mara tatu mfululizo kwa mashindano hayo – 1998, 2002 na 2006. Ndiyo timu pekee ya Afrika kushiriki fainali zote mbili za mwaka 2002 na 2006.

Kwa upande wa AFCON, walifanikiwa kutwaa kombe mwaka 2004 walipoandaa mashindano haya.

Ivory Coast – Tembo

Ivory Coast au Tembo ni timu nyingine yenye jina kubwa, na hadi mwaka 2005 mafanikio yao makubwa yalikuwa kutwaa kombe la AFCON dhidi ya Ghana kwa mikwaju ya penati nchini Senegal.

Tembo hawa wamefuzu mara mbili Kombe la Dunia mwaka 2006 na 2010, lakini hawakuingia hatua za makundi.

FIFA inaiweka Ivory Coast katika nafasi ya kwanza kati ya timu za Afrika, licha ya kwamba Ghana wamefanya vyema zaidi yao kwenye mashindano tofauti katika miaka mitano iliyopita.

Morocco – Simba wa Atlas

Simba wa Atlas ni timu ya taifa ya Morocco, walio chini ya kocha Rachid Taoussi.

Hawa ni washindi wa AFCON mwaka 1976 na ndio timu ya kwanza ya Kiafrika na Kiarabu kuongoza kwenye kundi lao katika Kombe la Dunia.

Heshima hiyo ilikuja mwaka 1986, walipomaliza mbele ya Uingereza, Ureno na Poland, timu ya kwanza ya Afrika kuingia raundi ya pili, wakaja kupigwa na Ujerumani bao 1-0, na Ujerumani ndio walikuja kuwa washindi wa pili.

Mwaka jana walitwaa ubingwa wa Kombe la Nchi za Kiarabu kwa kuwafunga Libya kwenye fainali.

Ethiopia – Swala wa Walya

Safari hii Ethiopia, au Walya Antelopes (Swala wa Walya) wamefuzu, baada ya kushindwa kwenye mchujo kwa miaka 31.

Katika ngazi ya FIFA wanashika nafasi ya 102, kwa CAF ni wa 28. Ethiopia, Misri na Sudan ndizo nchi washiriki wa mashindano ya kwanza mwaka 1957.

Walitwaa kombe mwaka 1962 walipoandaa.

Cape Verde – Papa wa Bluu

Simulizi za mende kuangusha kabati zilianzia kwa vijana wa Cape Verde, na pengine sasa ni sawa kujigamba kwa kujiita jina la Blue Shark (Papa wa Bluu).

Oktoba 14, 2012 ni siku ya kihistoria, maana Cape Verde walifuzu kwa michuano hii baada ya kuwafungisha virago Simba Wasiofugika wa Cameroon.

Papa hawa waliwatoa Cameroon kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya marudiano Stade Ahmadou Ahidjo jijini Yaoundé, Cameroon.

Awali, katika mechi ya nyumbani kwao, Cape Verde waliwapa Simba hao kichapo cha mabao 2-0.

Kwa mara ya kwanza katika historia yao, Cape Verde walicheza mechi na timu ya nje ya Afrika kwa kukipiga na Luxembourg na kutoka suluhu katika mechi ya kirafiki.

Angola – Swala Weusi

Majina ya wanyama yanapendwa katika timu, japo wengi hawafanyi vizuri. Ndivyo ilivyo kwa Angola – Swala Weusi.

Angola walijipambanua kwa kushika nafasi ya 45 kwa umaarufu wa soka chini ya FIFA mwaka 2002. Kilele cha mafanikio yao ni kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006. Huko walitolewa hatua ya mwanzo kwa kufungwa mechi moja na kutoa sare mbili.

Wana rekodi ya kuwafunga Cuba bao 1-0 mwaka 1977 na walifuzu kwa AFCON mara ya kwaza mwaka 1996. Wameshinda Kombe la COSAFA mwaka 1999, 2001 na 2004.

Niger – Swala

Swala wengine kwenye mashindano haya wanatoka Niger, nao wanaitwa ‘Menas’ au ‘Dama Gazelle’. Japokuwa ni timu dhaifu katika eneo lenye timu kali la Afrika Magharibi, Niger imewahi kupata matokeo ya kushitua katika nyakati za kufuzu.

Walionesha ufanisi wakati wa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 1982 kwa kuwafungisha virago Somalia na Togo kwa mabao ya ugenini, lakini wakatolewa na Algeria katika raundi ya tatu, zikabaki timu nane tu.

Mwaka 1990 waliweka rekodi kwa kuwararua Mauritania mabao 7-1, ushindi wao mkubwa zaidi hadi sasa.

Niger walishinda mechi zao zote za nyumbani kuwania kufuzu AFCON mwaka 2004, lakini zikakasoro pointi tatu kuwavusha. Ni timu inayosumbuliwa na matatizo ya fedha.

Togo – Chiriku

Ukiachana na wanyama, Afrika Kusini kuna ndege pia, na hapa tunazungumzia Chiriku wa Togo waliofanikiwa hata kucheza Kombe la Dunia mwaka 2006.

Kumbukumbu iliyo mbichi bado ni kushambuliwa kwa basi la timu hiyo katika mpaka wa Angola na Kongo, wakiwa safarini kwenda Michuano ya AFCON 2010 nchini Angola.

Watu watatu waliuawa kwenye mashambulizi hayo yanayodaiwa kufanywa na waasi wa kisiasa, na Togo wakajitoa mashindanoni kutokana na kiwewe na mshituko wa mashambulizi na msiba huo.

Kwa hiyo wanaingia kwenye mashindano ya mwaka huu wakiwa na kumbukumbu hiyo chungu, na pengine itakuwa kichocheo cha kufanya vizuri.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo – Chui

Chui wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wenye historia ya wachezaji wanaosakata soka safi, wamefuzu kwa mashindano haya.

Chui hawa wanashikilia nafasi ya 51 kwenye ubora wa viwango wa FIFA na walikuwa timu ya kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kufuzu kwa Kombe la Dunia. Wametwaa kombe la AFCON mara mbili.

Burkina Faso – Farasi Wasiohasiwa

Soka ni pamoja na utani, kucheka na hapa timu ya Burkina Faso inatoa nafasi hiyo, kwani inaitwa ‘Les Etalons’, yaani Farasi Wasiohasiwa. Walijulikana kama Upper Volta zamani kabla ya jina la nchi halijabadilishwa mwaka 1984.

Huwa wanaanza michuano mingi vyema, lakini huishia njiani, na walifanya vizuri zaidi kwenye soka mwaka 1998, walipomalizia nafasi ya nne walipoandaa mashindano haya.

Algeria – Mbweha wa Jangwani

Mbweha wa Jangwani ndiyo timu ya taifa ya Algeria, iliyofika mbali kisoka kwa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mara tatu – mwaka 1982, 1986 na 2010. Mwaka 1982 waliwafunga waliokuwa mabingwa wa Ulaya, Ujerumani Magharibi mabao 2-1 na kushitua ulimwengu.

Mbweha wa Jangwani hawa wametwaa mara moja tu kombe la AFCON, nayo ilikuwa mwaka 1990 walipoandaa michuano hii.

Mahasimu wa kisoka wa Algeria huwa ni Morocco, Tunisia na Misri, lakini Mafarao wa Misri wamekuwa zaidi miaka ya karibuni, hadi kuhusisha matukio ya fujo.

[email protected]

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ronaldo hat-trick fires Real into Copa quarters

Stoke mbendembende kwa Chelsea