Wanasoka saba wamekamatwa wakihusishwa na tuhuma za kupanga matokeo ya mechi.
Taasisi ya Kukabiliana na Uhalifu (NCA) imesema wanandinga hao wana umri wa miaka kati ya 18 na 30 na wanachezea klabu za soka zilizo kaskazini magharibi mwa England.
Wanaume wengine sita walikamatwa Desemba mwaka jana kwa tuhuma kama hizo, lakini baadaye wakaachiwa kwa dhamana na sasa wamekamatwa tena na kuwekwa ndani.
NCA imesema kwamba wote 13 wanahojiwa na polisi kuhusiana na madai ya kwamba ya rushwa na kutakatisha fedha. Njia mbalimbali zinazotumiwa kupanga matokeo ni pamoja na mchezaji kufanya kosa makusudi ili apate kadi ya njano au nyekundu.
Lakini pia, wachezaji husika huweza kulipwa kitita cha fedha ili timu yake ifungwe kwa kukubali kizembe kona, kusababisha penati au kumrudishia kipa mpira kwa namna ambayo ama atashindwa kudaka uzame wavuni au mpinzani anase mpira huo na kufunga kirahisi.
Wachezaji wanaojulikana kwamba walipata kukamatwa kwa tuhuma hizo ni pamoja na mshambuliaji wa Blackburn Rovers, DJ Campbell, winga wa zamani wa Oldham Athletic, Cristian Montano na wengine wanne baada ya tuhuma hizo kutajwa kwenye vyombo vya habari.
Mchezaji wa zamani wa Portsmouth, Sam Sodje alipata kudai kwamba alikuwa wakala wa kupanga matokeo, ambapo kwa kadi ya njano na nyekundu kitita kikubwa kilotolewa, lengo likiwa kuipunguzia timu husika kiwango mchezoni hatimaye ifungwe.
Msemaji wa Bodi ya Ligi ya Soka amesema kwamba wameshajulishwa na mamlaka husika juu ya kukamatwa kwa wachezaji hao na kwamba watatoa ushirikiano wa kutosha kwao ili haki itendeke kwa mujibu wa sheria na soka ibaki kuwa safi.
Comments
Loading…