WACHEZAJI wawili wa kimataifa wa Tanzania, Emanuel Gabriel na Nizar Khalfan wanatarajiwa kuondoka nchini kwenda barani Ulaya kusakata soka la kulipwa.
Katibu mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema Gabriel, ambaye anafunga ndoa Julai 14, ataondoka nchini Julai 19 kwenda Israel kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa, wakati Nizar anatakiwa Hungary.
”Kinachomchelewesha Gabriel ni harusi yake, anafunga ndoa mwezi huu tarehe 14. Isingekuwa harusi ungekuta ameshaondoka,” alisema Mwakalebela.
”Nizar pia yupo mbioni siku yoyote kuanzia sasa kwenda Hungary. Awali suala la viza ndilo lililomkwamisha, lakini kila kitu sasa hivi kinakwenda vizuri na ataondoka wakati wowote kuanzia sasa,” alisema.
Wachezaji wote wawili wana uzoefu wa kucheza nje ya nchi. Gabriel ameshakwenda Arabuni kucheza soka la kulipwa mara mbili na alirejea nchini mwishoni mwa msimu uliopita, wakati Nizar alikuwa nchini Kuwait kuchezea klabu ya Odlaham iliyomnasa wakati Stars ilipokwenda Uswisi kwa mazoezi.
Mwakaleleba pia alisema kuwa kiungo wa zamani wa Simba, Pius Kisambale na Erick Majaliwa wameondoka nchini juzi kwenda India na tayari wamesaini mkataba wa kuichezea klabu ya Dispot India ya nchini humo.
Alisema mbali na nyota hao pia beki wa Simba, Said Sued yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha safari yake ya kwenda barani Ulaya kusaka soka la kulipwa. Sued aligoma kusaini Simba msimu huu.
Mbali na wachezaji hao kutimkia nje, beki aliyeachwa na Yanga, Lulanga Mapunda na Uhuru Selemani, ambaye klabu yake ya Coastal Union imeshuka daraja, wamemwaga wino kuichezea Miembeni ya Zanzibar.
Mwakalebela alisema wachezaji hao wapo kwenye orodha ya kikosi cha Miembeni kitakachoshiriki Kombe la Kagame inayoanza kesho jijini Dar es salam na Morogoro.
Wakati huo huo Mwakalebela amesema Cheti cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) cha kipa mpya Mserbia wa Yanga, Obren Curkovic kimewasili.
Soka la tanzania litakua tu endapo vijana wa umri 17 wa timu ya taifa watendelezwa na sio wakubwa ambao tunawalazimisha tu wacheze soka la kiwango cha juu,kitu ambacho ni kigumu ingawaje kocha wa timu ya taifa katuweka sehemu nzuri kwa sasa.Naomba vijana waendelezwe tu tutafikambali.