KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo Jumatano imetangaza rasmi kumrejesha mgombea wa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Simba, Michael Wambura, kwa kupiga kura baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutofikia kauli muafaka juu ya maamuzi yao imeelezwa.
Hata hivyo Wambura anatarajiwa kujadiliwa tena kesho Ijumaa katika Kamati ya Maadili kutokana na mwanachama wa Simba, Jackson Sagonge ‘Chacha’ kuwasilisha malalamiko yake katika kamati hiyo tangu wiki iliyopita.
Akitangaza maamuzi ya rufaa hiyo iliyojadiliwa kwa muda wa siku mbili Wakili, Julius Lugaziya, alisema kuwa baada ya kupitia hoja 14 na mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na mrufani (Wambura) na maelezo kutoka kwa wanachama watano waliomuwekea pingamizi wakiongozwa na Said Rubeya, waliamua kupiga kura.
“Uamuzi wa Kamati ya Rufaa ulizingatia wingi wa kura, kwa sababu wajumbe hawakukubaliana kwa kauli moja kupata muafaka wa rufaa hii,” alisema Lugaziya kabla ya kueleza hoja ambazo kamati yake ilizijadili na kuamua kumrejesha Wambura kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa klabu hiyo.
Lugaziya alisema kuwa kamati yake imeamua kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa sababu kuu nne ikiwano Wambura kuendelea kushiriki kulipa ada ya uanachama na mchango wa mawazo isipokuwa uchaguzi uliopita.
Alisema pia mrufani huyo alikuwa akishiriki mikutano mikuu ya klabu na ya dharura iliyoitishwa huku kikatiba mwanachama anayeruhusiwa kushiriki ni hai.
Aliongeza kwamba Wambura amerejeshwa kutokana na kuteuliwa kwenye Kamati ya kuandaa Mpango Mkakati wa wa klabu hiyo na mapema mwaka huu aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji inayomaliza muda wake.
“Kimatendo hakuna mahali panapoonyesha Wambura alisimamishwa, na kama yeye alikuwa si mwanachama halali basi vikao vyote alivyoshiriki ikiwamo cha marekebisho ya katiba na kuteua Kamati ya Uchaguzi navyo ni batili,” Lugaziya aliongeza.
Alieleza pia suala na kusimamishwa uanachama halikuwahi kuhojiwa na mgombea huyo au mwanachama mwingine katika mkutano mkuu uliofuata na tangu alipoandikiwa barua ya kusimamishwa Mei 5 mwaka 2010 wakati tayari imefanyika mikutano minne na vikao vya kamati ya utendaji vilivyoanishwa katiba katiba 20.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kwamba uamuzi wa kamati yake hauwafungulii wadau kwenda mahakamani kudai haki ila unaelenga kukumbusha klabu na wanachama wengine wa TFF kuzingatia taratibu walizojiwekea kwa weledi badala ya kutumia taratibu hizo kwa manufaa hasi katika mchezo wa soka hapa nchini.
Katibu huyo wa zamani wa Chama cha Soka Nchini (FAT sasa TFF) amesema kwamba amepata taarifa hizo za kurejeshwa kwenye mchakato wa uchaguzi baada ya kushinda rufaa yake.
Hata hivyo Wambura alieleza kwamba atatoa mawazo yake juu ya maaamuzi ya kamati hiyo leo saa sita mchana atakapozungumza na vyombo vya habari.
“Sijapata rasmi ila nimezisikia taarifa hizo, nitazungumza kesho (Alhamisi) na waandishi wote jinsi nilivyoyapokea maamuzi hayo,” alisema kwa kifupi Wambura.
Klabu ya Simba inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Juni 29 mwaka huu na viongozi watakaochaguliwa watakaa madarakani kwa muda wa miaka minne.
Comments
Loading…