Yohana Nkomola, ni moja ya jina ambalo lilikuwa linatajwa sana wakati tunaelekea Gabon kushiriki fainali za Afcon ya vijana ya umri wa miaka 17.
Lilikuwa linatajwa sana siyo kwa sababu tu alikuwa mchezaji wa mchezaji maarufu wa zamani, au alikuwa mtoto wa mwanasiasa maarufu hapa Tanzania.
La Hasha! Kitu pekee ambacho kilikuwa kinamfanya Yohana Nkomola kutajwa sana ni uwezo wake mkubwa aliokuwa nao.
Huyu ndiye ambaye aliibeba Serengeti Boys kwenda Gabon kwa mara ya kwanza katika historia ya mpira wa vijana.
Huyu ndiye aliyekuwa mshambuliaji tegemezi sana kwa wakati huo. Kwa kifupi alikuwa amebeba matumaini yetu kwa wakati huo.
Pamoja na kwamba timu hii iliundwa sana kitimu tofauti na timu hii ya mwaka huu lakini ilikuwa aibu sana kuukata mchango wa Yohana Nkomola.
Yohana huyu ambaye alitufanya tupate hofu kubwa sana pale tulipogundua ni majeruhi na siku za mashindano zilikuwa zimewadia.
Hofu ilikuwa kubwa sana ndani yetu kwa sababu taifa lilijua linaenda kupoteza mtu muhimu ndani ya kikosi cha Serengeti Boys.
Yohana huyu ambaye alitakiwa na vilabu vingi sana kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye timu za vijana za vilabu husika.
Ndiyo Yohana huyu huyu ambaye alikanyaga ardhi ya Misri kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Al Ahly ya Misri.
Klabu kubwa sana duniani, mabingwa wa kihistoria wa ligi ya mabingwa barani Afrika,.lakini Yohana Nkomola mguu wake ulikanyaga hapa.
Tena ulikanyaga kwa ajili ya kufanya kitu kikubwa sana, kufanya majaribio katika timu ya vijana ya klabu hii kongwe na kubwa duniani.
Usiniulize matokeo ya majaribio yalikuwaje. Swali gumu kwangu na siyo busara kutazama hiki katika mlengo ambao ni hasi.
Tulitazame hili katika mlengo chanya. Yohana Nkomola alifanikiwa kufanya majaribio kwenye klabu kubwa kama hii. Klabu ambayo wachezaji wengi wa Afrika wanatamani sana kuichezea.
Hiki ni kitu kikubwa sana na kitu hiki kinaonesha kitu kimoja. Yohana Nkomola alikuwa na kitu kwenye miguu yake.
Alikuwa na kitu ambacho kingekuwa na msaada mkubwa sana kupitia miguu yake ambayo leo hii hatujui wapi ilipo.
Kwa umri wake mdogo alifanikiwa sana kupata nafasi ya kufanya majaribio, kitu ambacho ni kikubwa sana na ni kitu ambacho wachezaji wengi hawajakifanya.
Kuna ubishi kusema kuwa huyu mtoto ni faida kwa miaka ijayo? Hapana shaka hakuna ubishi kabisa kwenye hili.
Na mara nyingi tumekuwa na utamaduni wa kupiga teke kila sahani ya mafanikio inayobahatika kuja mbele yetu.
Muda ukipita ndipo hapo tunapokuja kulikumbuka sahani hilo ambalo kwa muda huo linakuwa halina.kitu chochote kabisa.
Leo hii tunamsifia sana Kelvin John. Tunamuona kama mchezaji tegemeo katika miaka ijayo kwenye taifa letu.
Kitu ambacho ni kizuri sana lakini tunakosea sana kusahau baadhi ya vipaji ambavyo tushawahi kuwa navyo na kuviterekeza bila kujua wapi vilielekea.
Vipaji ambavyo vingekuwa msada mkubwa sana kwa miaka ijayo kwenye timu yetu ya taifa. Tujivunieni sana Kelvin John lakini tumtafuteni Nkomola aje akae na Kelvin kwa ajili ya stars ijayo.