in , , ,

WACHEZAJI MZIGO YANGA

1: Nadir Haroub “Cannavaro”.

Hapana shaka Jangwa la kariakoo ni tofauti na ma Jangwa mengine. Ukame ndiyo sifa pekee ya Jangwa lolote, lakini hii imekuwa tofauti na jangwa la Kariakoo, jangwa ambalo lina vipindi vyote, vipindi vya masika na vipindi vya kiangazi.

Alikuja jangwani akiwa na umbo la shina la mchina. Watu walibeza sana, wakadharau, wakakebehi sana na mwisho wa siku wakatoa utabiri wao wa Nadir Haroub “Cannavaro” kutodumu katika klabu ya Yanga.

Ikawa tofauti na utabiri wa wengi, mbuyu ukamea na kukua jangwa la Kariakoo mpaka Samuel Etoo mchezaji mahiri kuwahi kutokea duniani akashuka chini na kumuomba jezi Nadir Haroub “Cannavaro” kama ishara ya yeye kukubali na kuheshimu kiwango chake.

Muda umekimbia sana, hakuna kitu kikubwa kilichofanyika nyuma kikaweza kufanyika sasa hivi kwenye miguu ya Nadir Haroub “Cannavaro”. Kwa sasa akili yake inahitajika zaidi kwenye benchi la ufundi kuliko miguu yake kuhitajika uwanjani. Miguu haina nguvu kubwa tena kama kipindi cha nyuma, heshima pekee ya kustaafu na kuanza kujifunza ukocha ndiyo anayostahili kwa sasa.

2: Geofrey Mwashiuya.

Hapana shaka unapakumbuka Mbozi, sehemu ambayo ilikuwa maarufu sana kipindi ambacho Geofrey Mwashiuya alipokuwa anasajiliwa.

Vita ilikuwa kubwa sana kwa mafahari wawili wa Kariakoo lakini mwisho wa siku yule mwenye rangi tatu akafanikiwa kuidaka nyota kutoka Mbozi.

Ilikuwa nyota ambayo ilitazamiwa kung’aa sana pale Jangwani. Usiku wenye giza kubwa ulikuja kuifunika hii nyota baada tu ya kukanyaga kariakoo, taa nyingi alizozikuta kariakoo aliziona zina mwanga mkubwa unaotosha kuweka nuru pale Kariakoo, hakuona tena umuhimu wa yeye kuifanya nyota yake ing’ae tena. Nyota ikaanza kufifia taratibu, akawa ameridhika kuwepo pale na hakuna jitihada ƴyoyote anayoifanya kuhakikisha anapigana na wingu zito lililofunika nyota yake.

Dalili kubwa zinaonesha huyu atarejea sehemu ambayo tutamsahau tena kwa kifupi hakuwa amejiandaa kuja kariakoo na kuishi maisha ya jangwani. Inahitaji moyo kumvumilia kukaa kwenye timu yenye presha ya mafanikio kama Yanga. Hofu yangu kubwa ni kuwa Yanga msimu huu wana dalili kubwa ya kupoteza ubingwa wao kitu ambacho kitaipa nafasi msimu kesho kusuka kikosi kipya, nahisi katika utaratibu wa kuondoa nywele zilizochakaa katika usukaji hii nywele ya Geofrey Mwashiuya itaangushwa chini.

3: Emmanuel Martin.

Mechi ya JKU dhidi ya Yanga ilifanya mboni ya jicho la George Lwandamina kupeleka taarifa kwenye ubongo wake kuwa kuna kitu kakiona kwa Emmanuel Martin.

Magoli mawili aliyoifunga Yanga yaliyosha kumpa pasi ya kusafiria mpaka Jangwani. Wengi walihoji sana, wakabaki kimya na kusubiri muda uzungumze.

Muda ushaanza kuonesha matokeo taratibu, Yanga imekuwa timu inayotegemea wachezaji wa pembeni wakati inashambulia.

Kwa kipindi kirefu wafungaji wake bora wamekuwa wachezaji wanaotokea pembeni. Tangu enzi za Edibily “Jonas” Lunyamila, Said Maulid “SMG”, Mrisho Khalfan Ngassa, kwa siku za karibuni ni Simon Msuva. Baada ya Simon Msuva kuondoka tulitegemea kina Emmanuel Martin waje kufanya kitu kulingana na utamaduni wa klabu husika.

Lakini imekuwa tofauti kabisa, Emmanuel Martin siyo mchezaji ambaye anaweza kuibeba Yanga kutokana na eneo alilopo kulingana na utamaduni wa Yanga.

4: Pato Ngonyani.

Kuna kuibeba timu na kuna timu kukubeba. Hapa kwa Pato Ngonyani tunapata tafasri moja tu kuwa Yanga inambeba.

Hana uwezo mkubwa wa kuibeba timu ya Yanga hata wa kuwa mmoja wa wachezaji wa Yanga. Ni moja ya wachezaji ambao hawana mabadiliko kila kukicha.

Aina ya uchezaji wake haiendani na mahitaji ya mpira kwa sasa. Ni kiungo wa kati lakini pasi zake nyingi ni square pasi, hapigi pasi za kuisukuma timu au kutengeneza nafasi nyingi za magoli.

5: Said Juma “Makapu”.

Hapana shaka msimu huu amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga. Kacheza nafasi mbili kwenye kikosi cha Yanga.

Nafasi ya kiungo wa kujizui na nafasi ya beki wa kati. Lakini ukweli unabaki pale pale huwezi kushindana na watu wakubwa kiushindani ukiwa na aina ya viungo kama Said Juma “Makapu”. Wachezaji ambao hawawezi kuisukuma timu kwenda mbele na kuiamrisha itembee. Matatizo aliyonayo Pato Ngonyani ndiyo anayo Said Juma “Makapu”.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Tunahubiri Weledi kwenye Koti la Yondani

Tanzania Sports

Kwa heri Arsene Wenger, tutakukumbuka