Tulikaa miaka 39 bila kushiriki michuano ya Afcon. Mioyo yetu ilikuwa inatamani sana siku moja sisi kwenda Afcon. Ilikuwa safari ndefu sana, safari ambayo ilichukua miaka 39.
Mwaka 2019 tulifanikiwa kufuzu michuano ya Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39. Kitu ambacho tulikuwa tunakisubiri kwa hamu sana na tulifanikiwa kukipata.
Haikuwa bahati kwetu sisi kupata nafasi hiyo adhimu ambayo ilituwezesha kwenda Afcon. Pamoja na kwamba kulikuwa na ushindani kwenye kundi letu Ila tulifanya mahesabu mazuri yenye nidhamu.
Nidhamu ndiyo iliyotubeba kwa wakati huo, nidhamu ya kuhakikisha tunashinda angalau mechi za nyumbani. Kwenye mechi tatu za nyumbani tulifanikiwa kushinda mechi mbili.
Cape Verde ambao walikuwa wapinzani wetu wa karibu kwenye kundi tulifanikiwa kuwafunga magoli 2-0, Uganda ambao walikuwa vinara wa kundi tuliwafunga nyumbani 3-0, mechi ambayo ilikuwa ya mwisho na ndiyo iliamua sisi kwenda Afcon.
Pamoja na kwamba tulitoka sare nyumbani dhidi ya Lesotho, lakini pia tulifanikiwa kutoka sare ya muhimu sana dhidi ya Uganda kwenye uwanja wao wa nyumbani. Sare ambazo zilituwezesha tupate alama mbili muhimu kimahesabu.
Nidhamu ya mahesabu ilitusaidia kwa kiasi kikubwa kwetu sisi kufuzu michuano hii ambayo tulikuwa tunaitamani kwa muda mrefu kwenye maisha yetu baada ya miaka 39.
Nidhamu hii ya kimahesabu ilisindikizwa kwa kiasi kikubwa na nidhamu ya kuwafanya wachezaji wetu kuwa na mechi nyingi za kimataifa, mechi ambazo ziliwawezesha wao kutojiona wageni kwenye mechi kubwa.
Mechi hizi za kimataifa zilipatikana kwa njia mbili, njia ya kwanza ni risk tulifanikiwa kupeleka baadhi ya wachezaji wetu muhimu kwenye ligi ambazo zina ushindani mkubwa kuzidi ligi yetu ya nyumbani.
Ligi ambazo ziliwapa wachezaji wetu mechi nyingi za kiushindani wa kimataifa . Wachezaji muhimu kama Mbwana Ally Samatta na Simon Msuva walikuwa na mechi nyingi za kimataifa na zenye ushindani kwa sababu ya kucheza ligi za kimataifa na zenye ushindani.
Pia vilabu vyetu hapa nyumbani vilikuwa vinafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, wachezaji wengi walipata mechi za kiwango cha ushindani kupitia michuano ya ligi ya mabingwa barani Africa na kombe la shirikisho.
Tukawa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wamecheza mechi nyingi sana za kimataifa kama kina Aishi Manula, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, John Bocco na wengine wengi.
Huu ndiyo ukawa mwanzo wa sisi kufikia matamanio yetu ya kwenda Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39. Kiu yetu ikawa imekatika.
Kuna kitu kimoja ambacho tumebakiza, ni sisi kuwaona waamuzi wetu wakichezesha michuano ya Afcon. Lakini pamoja na sisi kutamani wao wanaonekana hawatamani kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya aina ya maamuzi ambayo wanayatoa kwenye ligi yetu.
Maamuzi ambayo hayatoi matumaini kama watakuja kuchezesha michuano ya Afcon. Waamuzi wetu wanatakiwa kuwa na tamaa mioyoni mwao kwanza.
Watamani kuchezesha michuano mikubwa, wakianzia hapa naamini itakuwa rahisi kwao wao kufikia lengo la kuchezesha michuano mikubwa kama Afcon .
Itakuwa mwanzo kwao wao kuchezesha vizuri kwenye ligi yetu huku wakiwa na imani kuwa kuchezesha vizuri kwenye ligi yetu kutawapa nafasi kubwa ya kuchezesha michuano mikubwa.