Chama cha waamuzi wa soka hapa nchini Tanzania (FRAT) kwa kushirikiana na shirikisho la soka Tanzania TFF kinatarajia kuandaa kuendesha kozi kwa waamuzi wenye beji ya FIFA na waamuzi wa daraja la kwanza kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa michuano ya ligi kuu Tanzania bara.
Mwenyekiti wa chama cha waamuzi nchini Tanzania Omary Abdul Kadir amesema mafunzo hayo yamelenga katika kuwapiga msasa waamuzi hao ili kuwa na uwezo wa kutosha kuchezesha michuano hiyo.
Mwenyekiti huyo amesema waamuzi watakaofanya vibaya katika kozi hiyo watakosa nafasi ya kuchezesha michuano ya ligi kuu msimu ujao.
Katika kozi hiyo pia yatafanyika mafunzo ya COOPER TEST (mitihani ya majaribio kwa waamuzi hao) ambao kutafanyika mafunzo ya vitendo na nadharia na muamuzi atakaefanya vibaya basi hatochezesha michuano hiyo.
Mwenyekiti huyo wa FRAT hakutaja idadi ya waamuzi wanaowahitaji kuchezesha ligi kuu usimu ujao ila akasema watachagua muamuzi wa kuchezesha ligi hiyo kutokana na uwezo wake na yule mwenye uwezo mdogo haitajiki.
Kila msimu wa ligi kuu hapa Tanzania timu mbalimbali pamoja na washabiki wa soka wamekuwa wakiwalalamikia waamuzi wake wakisema wanauwezo mdogo huku wengine wakienda mbali kwa kusema eti ndio chanzo cha kushuka kwa soka la Tanzania na wengine wakisema wanapokea rushwa ila hadi leo hakuna alisibitisha kama kweli kuna rushwa katika hilo.
Ligi kuu Tanzania bara msimu ujao inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi ujao wa August tarehe 23/ 2009 na timu 12 zinashiriki ligi hiyo huku ikiwa na timu tatu zilizopanda daraja msimu uliopita.
Timu zilizopanda daraja ni Maji maji ( Wanalizombe) ya Songea mkoani Ruvuma, African Lyon (Wazee wa TMK) na Manyema Ranges (Mkuki wa Sumu) zote za Dar es salaam.
Comments
Loading…