Wachezaji wa Afrika wanaonekana kuchanua katika soka ya Ubelgiji, moja ya mataifa ya hapa Ulaya yenye wachezaji wengi weusi na inaowaheshimu.
Muongo mmoja uliopita, katika mechi kulikuwapo Waafrika 10 na raia mmoja wa Latvia, Igor Stepanovs kwenye kikosi cha Beveren, ambapo watu walitania kwamba ilikuwa mechi baina ya Brugge na Ivory Coast, kwa sababu wengi wa wachezaji hao walitoka nchi hiyo.
Beveren ni klabu iliyokuwa na makazi yake nje ya viunga vya Jiji la Antwerp. Klabu hiyo kwa sasa imevunjwa. Ilikuwa na ushirika na akademia ya Jean Marc Guillou yenye makazi yake jijini Abidjan, Ivory Coast, hivyo wachezaji wengi waliletwa Ulaya kupita Ubelgiji.
Ni hao waliwaleta nyota wa soka kama akina Yaya na Kolo Toure, Emmanuel Eboue, Boubacar Barry, Arthur Boka na Gervinho. Ubelgiji imewavuta Waafrika wengi wanasoka, ilisita kidogo hapo kati lakini sasa yaelekea kasi inarudi.
Leo hii ukizungumzia klabu kama KV Oostende yenye makazi yake kwenye ufukwe wa West Flanders, utaona kwamba msimu huu wa ligi wameanza wakiwa na wanasoka tisa Waafrika, lakini si kutoka Ivory Coast, bali mataifa tisa tofauti.
Hawa wanaongozwa na nahodha ambaye ni raia wa Cameroon, Sebastien Siani, 28, akicheza nafasi ya kiungo mkabaji. Wengine ni Joseph Akpala, 28, mshambuliaji kutoka Nigeria, Elimane Coulibaly, 35, naye pia mshambuliaji na raia wa Senegal.
Wanaye mtu anayeitwa Cyriac Gohi Bi, au kwa jina jingine ‘Zoro’, kijana mwenye umri wa miaka 24, akiwa ni mshambuliaji wa Ivory Coast. Kuna kiungo wa Afrika Kusini, Andile Jali, 25, Yannick Loemba, 24, ambaye ni mshambuliaji wa pembeni kutoka Kongo.
Mdogo wake Romelu Lukaku wa Everton ya England, Jordan Lukaku, 21, naye anakipiga kwenye klabu hiyo. Huyu kama kakaye ni raia wa Ubelgiji, lakini asili yao ni Zaire, baba yao alikuwa mwanajeshi na aliikimbia nchi baada ya kuona matata ya Rais Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Za Banga.
KV Oostende pia wana mshambuliaji kutoka Zimbabwe, Knowledge Musona, 25 lakini pia kipa wa Timu ya Taifa ya Gabon, Didier Ovono, 32, anacheza soka huko.
“Sie ni familia kubwa, wote walio kwenye kikosi hiki wanaelewana vizuri na Waafrika ni sehemu muhimu sana ya timu.
Msimu uliopita tulianza vizuri kisha tukaanguka, lazima kuwa makini kuhakikisha tija na ufanisi vinaongezeka na tunakuwa na uendelevu katika kupambana na kushinda,” anasema Mkongomani Loemba anayefurahia matokeo ya timu, ambapo katika mechi tatu za awali, wameshinda mbili na kwenda sare moja katika Pro League – Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Mwafrika Kusini Jali ambaye ni injini ya Bafana Bafana, ni nyota klabuni hapo baada ya kujiunga na Oostende miezi 18 iliyopita akitoka Orlando Pirates. Musoma wa Zimbabwe aliwasili baada ya kushindwa kumudu mikiki ya Bundesliga nchini Ujerumani, lakini huko Ubelgiji ameanza kwa kufunga mabao.
Lukaku mdogo aliyezaliwa Antwerp akiamua anaweza kurudi kuchezea Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sababu bado hajaitwa kuchezea timu ya wakubwa ya Ubelgiji, tofauti na kaka yake. Amechezea timu ya vijana Ubelgiji lakini bado anakidhi matakwa ya Fifa kwa Kongo kwa kigezo cha wazazi wake kuzaliwa Afrika.
Alianzia soka yake kwenye akademia ya Anderlecht na sasa anajaribu kuanza soka ya kweli. Anasema anajihisi Mwafrika zaidi na kwamba iwapo angeitwa na Timu ya Taifa ya Kongo, kingekuwa kitu cha kuvutia.
Kipa Ovono wa Gabon anapendwa sana na washabiki na amekuwa akijitahidi sana kuzungumza kilugha – Flemishi. Baa ya mtaani kwao hivi karibuni iliandaa kinywaji maalumu kwa heshima yake, kikiandaliwa kwa mchanyato wa chokoleti, kilevi cha gin and rum, ndizi na sukari guru.