*Al Ahly, Zamalek zatangazwa mabingwa kabla
Machafuko yanayoendelea nchini Misri yamesababisha kufutwa kwa mechi zote zilizosalia za Ligi Kuu ya Misri.
Baada ya Rais Mohamed Mursi kuondoshwa madarakani na Jeshi, na nafasi yake kukaimiwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba, Adly Mahmud Mansour, vurugu zimeendelea, hivyo mabosi wa Chama cha Soka Misri (EFA) kuamua kumaliza ngwe mapema.
Al Ahly na Zamalek zimetangazwa kuwa mabingwa, kwa vile zilikuwa katika nafasi za juu kwenye makundi mawili ya timu tisa tisa. Makundi hayo yaliyokubaliwa baada ya ligi hiyo kuanza tena Februari mwaka huu, baada ya kutofanyika kwa mwaka mzima, kutokana na maafa ya Uwanja wa Port Said yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 70.
Ilikuwa imepangwa kwamba, timu mbili za juu katika kila kundi, Ahly, Zamalek, Eppi na Ismaili – zingesonga mbele kwenye nusu fainali, ambapo washindi wangeingia fainali.
Hata hivyo, baada ya miezi mitano ya machafuko, baadhi yakiingiza kwenye soka pia na washabiki kupigwa marufuku kwenye mechi za kimataifa, mashindano hayo sasa yamefutwa kutokana na machafuko ya kisiasa, ambapo zaidi ya watu 50 wameuawa.
Bodi ya EFA ilikaa na kuamua kumalizwa ligi ili kuepuka athari zaidi, ambapo klabu 18 zilikubali uamuzi huo, lakini klabu mbili za Zamalek na Enppi walipingana na EFA.
Zamalek wanataka kuendelea kwa mechi zilizobaki na kuingia hatua mpya, na pia wanataka fidia iwapo hilo halitatokea.
Rais wa EFA, Gamal Allam anasema klabu inayokataa uamuzi huo haina haki ya kudai fidia, kwa sababu uamuzi huo ulichukuliwa kwa sababu za usalama.
Ilikuwa ligi hiyo imalizike Juni 29, lakini mechi zake zilisitishwa kutokana na maandamano na matukio ya vurugu yaliyoanza wiki kadhaa kabla.
EFA waliiuliza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iwapo mechi zilizobaki zingeweza kuchezwa, lakini maofisa usalama wakakataa, wakisema intelijensia ilionesha machafuko yalikuwa yakiendelea, na ndivyo imetokea, kwa Mursi kufukuzwa na sasa wafuasi wake wanaandamana kupinga.
Haijajulikana iwapo ushiriki wa Alhy na Zamalek kwenye mashindano yajayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika utaathiriwa au la.
Comments
Loading…