Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesema suala la kuwepo kwa kipengele cha Upekee “EXCLUSIVITY” katika mkataba wa udhamini wa ligi kuu soka Tanzania bara kati ya kampuni hiyo na shirikisho la soka nchini – TFF ni la muhimu katika kuepuka migongano ya kimasilahi ya kibiashara miongoni mwa wadhamini.
Mkuu wa Udhamini na Mawasiliano wa kampuni ya Vodacom Tanzania Bw Kelvin Twissa amesema kampuni ya Vodacom inajali na kuthamini maendeleo ya vilabu nchini na kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa kutoa fursa zaidi zinazolenga kukuza kiwango cha uwekezaji katika soka kwa masilahi ya vilabu na taifa kwa ujumla.
Twissa amesema katika kutambua umuhimu wa kupanua wigo wa uwekezazi katika ligi kuu ya Vodacom na maendeleo ya vilabu kwa ujumla, kampuni ya Vodacom Tanzania ilikubali kwa moyo mkunjufu kuruhusu vilabu kutafuta wadhamini wengine ambao siyo makampuni yanayofanya baishara sawa na Vodacom.
Twissa alikuwa akizungumza katika kikao cha pamoja kilichowakutanisha Shirikisho la Soka Tanzania – TFF, Kamati ya Ligi Kuu na Mdhamini Mkuu kampuni ya Vodacom Tanzania kilichoketi jana jijini Dar es salaam.
“Tunatambua na kuheshimu utayari wa makampuni mengine ambayo yapo tayari kushirikiana na sisi katika kudhamini Ligi kuu ya Vodacom nasi tupo tayari kushirikiana nao na hivyo kuleta maendeleo ya mpira wa miguu nchini”Alisema Twissa
“Vodacom Tanzania inajivunia kuwa wadhamini wakuu wa ligi hii,tumeamua kuboresha udhamini wetu kwa sababu tunatambua umuhimu wa michezo kwa Taifa letu, sasa michezo si kwa ajili ya burudani tu bali imekuwa chanzo cha ajira na kuboresha maisha ya wanaojihusisha nayo,” Aliongeza Twissa.
“Tunaviomba vilabu vinavyoshiriki ligi kuu, vyombo vya habari na umma kwa ujumla kutambua kuwa azma ya Vodacom ni kuona mpira wa miguu unasonga mbele zaidi na ndio maana tumekuwa katika udhamni huu kwa zaidi ya miaka saba tukipitia vipindi tofauti lakini hatukuwahi kukata tamaa. Hivyo si vyema wakati huu soka yetu inapokua tukaruhusu hali inayoweza kusababisha changamoto katika uwekezaji wa soka.” Aliongeza Twisa
Twissa amesema kampuni ya Vodacom itaendelea kushirikiana na TFF, Kamati ya Ligi na wadau wengine wote wa mpira wa miguu nchini katika kukuza uwekezaji kwa kusaidia vilabu kupata wadhamini watakaosaidia maendeleo ya vilabu hivyo.
Comments
Loading…