*Sturridge Liverpool, Cole na Chamackh West Ham
*Modric anarudi EPL, Arsenal wajikusanya kwa Villa
Pilika za usajili wa dirisha dogo zinaendelea kwa kasi, vigogo wakipigana vikumbo kupata wachezaji bora kuziba viraka.
Pamoja na klabu kubwa za Manchester United, Manchester City na Chelsea kuzoea kutamba, Tottenham Hotspur inaonesha haikuwa nguvu ya soda msimu wa kiangazi.
Spurs walinasa nyota kwa msimu huu, na wanaendelea na jitihada za kuimarisha kikosi chao kinachotambia katika tatu bora kwenye msimamo wa ligi.
Baada ya kuchelewa msimu uliopita hadi kukosa washambuliaji wa kutosha, Liverpool imemsainisha Daniel Sturridge kutoka Chelsea kuichezea kwa ‘muda mrefu’ na inamtaraji Tom Ince wa Blackpool.
Joe Cole aliyekuwa yupo yupo Liverpool amejunga na timu aliyoanzia akiwa kinda ya West Ham United, ambayo pia imemchukua Marouane Chamakh wa Arsenal kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.
Luka Modric aliyelazimisha kuondoka Spurs hadi akalimwa faini, sasa ana kiu ya kurudi Ligi Kuu ya England (EPL), baada ya kura kuonesha ndiye asiyevutia kuliko wachezaji wote wapya wa Real Madrid.
Hivi sasa vigogo wa Manchester United na City pamoja na Chelsea wanasemwa kupigana vikumbo kuwania mchezaji huyo mwenye thamani ya pauni milioni 33.
Usajili wa dirisha dogo lililo wazi hadi mwisho wa mwezi huu unaweza kumaanisha mengi kwa timu zinazowania ubingwa na zile zinazojinasua kushuka daraja.
Kimsingi huwa si kipindi cha usajili wa wachezaji wengi, kwani inakadiriwa kiasi cha pauni milioni 925 zitatumika ikilinganishwa na pauni bilioni 3.685 zilizotumika kati ya Julai na Agosti katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Hata hivyo, klabu zinaweza kujitutumua zaidi kusaini wachezaji Januari hii, maana zinajua kuna kitita cha pauni bilioni tatu zinakuja Julai kwa ajili ya haki za TV, hivyo kipato chao kitaongezeka.
Arsenal imeanza kampeni ya ‘kushusha mizigo’ yake, ambapo Johan Djpurou amekopeshwa klabu ya Hannover 96 ya Ujerumani hadi mwisho wa msimu huu.
Arsene Wenger anadaiwa kuuza na kutoa wachezaji asiowahitaji ili kupata nafasi kifedha ya kumchukua David Villa wa Barcelona, asaidie katika ufungaji mabao. Hata hivyo, yapo madai ya kumsubirisha hadi mwisho wa msimu.
Kinara wa upachikaji mabao wa Newcastle, Demba Ba ameshaanza shughuli Chelsea alikosajiliwa kwa pauni milioni 7.5.
Hakuwakawiza washabiki na mabosi wake wapya, kwani katika mechi ya kwanza ya kombe la FA dhidi ya Southampton amepachka mabao mawili.
Newcastle inayoanza kuchungulia eneo la timu tatu za kushuka daraja, imemsajili mlinzi mahiri wa Lille ya Ufaransa, Mathieu Debuchy kwa pauni milioni tano.
Spurs imemsajili kinda wa Standard Liege, Ezekiel Fryers na imeshafunga makubaliano na Schalke 04 ya Ujerumani kumchukua kiungo mshambuliaji Lewis Holtby Julai.
Spurs wanaofundishwa na Andre Villas-Boas imemtoa bure golikipa wake, Carlo Cudicini kwenda LA Galaxy.
Bado wamebakiwa na makipa mahiri wa kimataifa, Hugo Lloris wa Ufaransa na Mmarekani Brad Friedel.
Wigan iliyo kwenye nafasi tatu za chini ya msimamo imemchomoa mshambuliaji Angelo Henrique wa Manchester United kwa mkopo.
Comments
Loading…