*Arsenal, Chelsea, Spurs zawinda nafasi mbili
*Moyes: Everton tutawabana Chelsea vilivyo
Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza (EPL) inaingia mzunguko wa mwisho, timu tatu zikiwania nafasi mbili za kuiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arsenal, Chelsea na Tottenham Hotspurs wana kazi ngumu na muhimu kutafuta ushindi, huku kila moja akiomba wenzake wawili wapoteze mechi ili wawe salama zaidi.
Chelsea wanaocheza na Everton wangependa kushinda ili kujihakikishia nafasi ya tatu EPL na kufuzu moja kwa moja hatua ya makundi, badala ya kushika nafasi ya nne inayohitaji kuingia kwenye mtoano.
Kocha wa muda wa Chelsea, Rafa Benitez anayemaliza kibarua chake msimu huu, anakutana na David Moyes ambaye pia anakamilisha miaka 11 Everton na kujiandaa kwenda kuanza maisha mapya kama kocha wa Manchester United. Benitez bado haijulikani hasa ataenda wapi, lakini angependa kubaki katika moja ya klabu kubwa za EPL.
Arsenal wanaopepetana na Newcastle ugenini, wanahitaji kushinda kwa idadi yoyote ya mabao ili kujihakikishia nafasi, wakati Spurs wanaocheza na Sunderland wanatakiwa kushinda na kuomba Arsenal wafungwe au watoke sare, vinginevyo waombe Chelsea wafungwe halafu wenyewe Spurs wafunge mabao mengi.
Kwa hali ya kawaida, matarajio yao ni kushinda halafu waombe tu Arsenal wafungwe au watoke sare. Chelsea wana pointi 72, Arsenal 70 na Spurs wa Andre Villas-Boas wanazo 69.
Moyes amesema tayari kwamba angependa kumaliza muda wake Everton kwa staili, ikiwa ni kukusanya pointi tatu ili wafikishe 66 na kuweka rekodi. Moyes anamaliza mkataba wake mwisho wa msimu, na kabla hajaitwa United, alitaka mazungumzo ya kuhusu hatima yake klabuni yafanyike baada ya msimu kumalizika.
Villas-Boas bado ana mkataba Spurs, lakini atakumbuka kwamba aliyemtangulia, Harry Redknapp alifukuzwa kazi licha ya timu kushika nafasi ya nne msimu uliopita. Pengine kitu pekee anachomzidi nacho ni ujana, moja ya vigezo vya kocha mpya vilivyotolewa na Spurs wakati huo.
Sir Alex Ferguson anamaliza kazi ya ukocha United kwa kucheza na West Bromwich Albion ugenini wakati Manchester City waliomfukuza kocha Roberto Mancini nao watakuwa wenyeji wa Norwich City. Klabu mbili hizo za Manchester zimeshafuzu Ulaya, kwani United ni mabingwa na City wapo nafasi ya pili.
Mechii nyingine za kutafuta heshima ni kati ya Liverpool na QPR; Southampton na Stoke City; Swansea na Fulham; West Ham United na Reading na Wigan watakaokipiga na Aston Villa.
Nafasi za kucheza Ligi ya Europa zinakuwa finyu kwa wanaofuata nne bora, maana washindi wa Kombe la Ligi, Swansea na wale wa Kombe la FA, Wigan hawapo kati ya nne bora.
Hii ni mara ya kwanza washindi wa Kombe la FA wameshushwa daraja, ambapo Wigan wameungana na Reading na QPR kwenda ligi ya ngazi ya pili – Championship. Mechi zote za Jumapili hii zinaanza saa 10 jioni.
Comments
Loading…