*Tunaposikia klabu za England ni nzuri tusisahau kuwa zamani wachezaji walikuwa wenyeji. Leo asilimia kubwa ya wachezaji si wananchi. Hivyo kocha wa taifa anapoingia huwa na majukumu ya kujenga kitu isiyokuwa na uwezo mzuri
Juzi Alhamisi FA ya England ilimchagua Gareth Southgate, Meneja mpya wa England kocha wake rasmi wa taifa. Uchaguzi wa Southgate umetokea baada ya kutimuliwa Sam Allardyce mwezi Septemba. “Big Sam” alikabidhiwa wadhifa uliokuwa na mkataba wa miaka miwili lakini akanyang’anywa baada ya siku 67 na mechi moja tu. Ilidaidiwa alipenda rushwa na kukiuka maadili ya uongozi kwa kufichua siri za wachezaji kwa mwanahabari bandia aliyemdaka akisema sema ovyo.
Gareth Southgate aliyekuwa kocha wa timu ya vijana wa chini ya miaka 21 ya England aliteuliwa kocha wa muda (caretaker) baada ya miezi miwili na mechi nne alizoshinda zote.
Kazi ya umeneja wa timu ya England hulinganishwa na Waziri Mkuu kwa ugumu. Vyombo vya habari hudadavua kila mwenendo wa kocha na kuangalia kila mechi na kutoa maoni. Si kazi rahisi na toka England ianze kucheza mechi za kitaifa baada ya vita vikuu vya pili imeajiri makocha 18. Meneja pekee aliyeambulia kombe la kimataifa ni Sir Alf Ramsey aliyeiongoza England kuchukua Kombe la Dunia la 1966 uwanja wa Wembley, London. Wengine wawili tu ndiyo walifikia nusu fainali, kombe la dunia la 1990- Bobby Robson na Terry Venables aliyeiongoza England kombe la Ulaya (Euro) mwaka 1996….
Waliobakia ama walitolewa michuano ya mwanzo au robo fainali.
Toka Sir Ramsey na timu yake ilipoongozwa na nahodha maarufu Bobby Moore kushinda kombe la 1966 makocha wamejaribu na kushindwa. Hatimaye baada ya kufikia kikomo na kuanza kukata tamaa, FA ya England ilianza kuangalia makocha wa nchi za kigeni. Hii si kawaida kwa timu za mataifa yaliyoendelea. Huwezi kusikia Ujerumani, Hispania au Brazil ikamwajiri kocha wa nje. Hata Arsene Wenger wa Arsenal alipofuatwa karibuni alikataa akasema ni haki England ikaongozwa na Mwingereza.
Baada ya makocha wa England kuambulia sifuri, mwaka 2001 meneja wa kwanza wa kigeni M- Sweden, Sven-Goran Eriksson aliajiriwa. Uteuzi wake ulitokana na ushindi wa vikombee kadhaa Ureno, Italia na Hispania. Mwaka 2002, England ilifikia robo fainali ya kombe la dunia lakini wakatolewa na Brazil. Eriksson alikosolewa sana lakini akaendelea kuishia robo fainali kombe la Ulaya 2004 na dunia , 2006.
Alipoondolewa msaidizi wake Steve McClaren aliongoza dimba hadi mwisho wa 2007 naye akatimuliwa baada ya England kuchapwa na Croatia.
Fabio Capello (Italia) alipewa mkataba hadi mwaka 2012. Wakati wa kombe la dunia lililokuwa Afrika Kusini (2010) Capello alikosolewa kwa mbinu mbaya na England haikuambulia hata robo fainali.
Kocha wa vijana Stuart Pearce alichukua ukanda lakini kwa muda mfupi halafu ndipo Roy Hodgson akateuliwa hadi mwaka huu.
Southgate ni tofauti na mameneja waliomtangulia maana hakuteuliwa moja kwa moja. Mbali na kuwa mchezaji wa England na kocha wa timu mbalimbali ikiwemo Middlesborough iliyofanya vyema, baada ya Big Sam kufukuzwa Southgate alisaidia kazi na akaonesha ushindi wa mechi nne , ari nzuri na wachezaji kumheshimu.Pamoja na hayo bado kazi ya ukocha wa England inaogopewa. Bado matumaini ya wananchi kulilia ushindi wa 1966 chini ya Sir Alf Ramsey makubwa.
Mimi nadhani nchi hii ina vyombo vya habari vikali sana vinavyotathmini wachezaji na makocha kiasi ambacho kazi huwa ngumu ingawa mshahara ni mamilioni. Sababu nyingine ni England kuwa na wachezaji wengi wageni kiasi ambacho wanasoka chipukizi hawajengwi vizuri. Tunaposikia klabu za England ni nzuri tusisahau kuwa zamani wachezaji walikuwa wenyeji. Leo asilimia kubwa ya wachezaji si wananchi. Hivyo kocha wa taifa anapoingia huwa na majukumu ya kujenga kitu isiyokuwa na uwezo mzuri.