Klabu 12 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, jana zilipokea vifaa mbalimbali kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, kampuni ya simu za mikononi Vodacom.
Kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Idara ya Udhamini wa kampuni hiyo, George Rwehumbiza, alisema kuwa katika msimu huu, Vodacom imepanga kutumia zaidi ya Sh. bilioni moja ikiwa na lengo la kuboresha ligi hiyo na kuongeza changamoto kwa timu zinazoshiriki.
Rwehumbiza alisema kuwa kati ya fedha hizo, Vodacom imetumia Sh. milioni 667 kwa ajili ya shughuli za kununua vifaa pamoja na gharama za uendeshaji.
Alisema kuwa kiasi hicho walichokitoa, ni kidogo ukilinganisha na gharama halisi za timu na kuwakaribisha wadhamini wengine ili kusaidia timu mahitaji yao ya kila siku.
Naye Mkurugenzi wa Masoko, Ephraim Mafuru, alisema kuwa wanatarajia ligi ya msimu ujao itakayoanza Agosti 21, itakuwa na mafanikio zaidi kuliko miaka iliyopita.
Mafuru alisema usimamizi mzuri na mafanikio katika uendeshaji wa ligi hiyo, vitasaidia kupata bingwa halali wa uwanjani (sio wa mezani).
Alisema kuwa Vodacom itatoa tena jezi kwa timu zote kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili na inatarajia kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kutoka kwa mashabiki nchini kwa ajili ya kuzisadia klabu hizo.
Makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ramadhan Nassib, alisema kuwa timu zote zinatakiwa kufanya maandalizi mazuri ili kuonyesha ushindani na kuacha kuwa washiriki.
Mmoja wa viongozi wa klabu, John Nchimbi, kutoka klabu ya Majimaji, alisema kuwa wameridhishwa na ubora wa vifaa walivyopewa na kuongeza kuwa sasa kazi imebaki moja ya kushindana uwanjani.
Baadhi ya vifaa walivyokabidhiwa viongozi hao wa klabu, ni pamoja na jezi kwa ajili ya mechi za nyumbani na ugenini, sare za kufanyia mazoezi, mipira, viatu na vizuia ugoko.
Vodacom pia ilikabidhi vifaa vingine kwa ajili ya waamuzi watakaochezesha ligi hiyo.
Katika mechi za fungua dimba, mabingwa Simba watacheza dhidi ya African Lyon wakati Yanga waliomaliza wa pili, watakuwa wageni wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.
Comments
Loading…