- Arsenal wanapiga hatua kuelekea ubingwa…
- Wolves katika sintofahamu ya kiuongozi…
- Brighton na City wanaonyesha ubunifu wa kimfumo….
- Tottenham na Forest wamo kwenye mtego wa kiakili na kimfumo.
Wikiendi hii ya Ligi kuu ya England, imeacha maswali, simanzi, furaha na mijadala moto moto, kutoka viwanjani. Haya ndiyo mambo 10 makubwa yaliyojitokeza:
1. Arsenal wazidi kupeta kileleni
Arsenal waliendeleza kasi ya ubingwa kwa kuifunga Burnley 2–0 ugenini, wakifungua pengo la pointi saba kileleni. Timu ya Mikel Arteta inaonekana thabiti – ulinzi imara, mipango imara ya mipira ya kona na adhabu ikiendelea kuzaa mabao.
2. Kilio Molineux – Wolves wamfukuza Vítor Pereira
Baada ya mechi 10 bila ushindi, Wolves wametangaza kumtimua kocha Pereira. Uamuzi huu wa ghafla unaibua mjadala juu ya ukosefu wa subira katika usimamizi wa vilabu vya EPL.
3. Brighton wavuna matunda ya mpango wa muda mrefu
Brighton wanaendelea kuonyesha ubora wa usajili wa kimkakati. Diego Gómez, kijana aliyesajiliwa kutoka Inter Miami, ameanza kung’ara. Klabu inaonekana kuvuna ilichopanda – mipango safi, kwa matumizi machache ya pesa..
4. Forest bado wanavuja – Dyche hana uchawi
Nottingham Forest bado hawajarekebisha ulinzi wao. Wakiwa chini ya Sean Dyche, sasa ni mechi 18 bila ‘clean sheet’. Dyche alisema wazi: “Hatuna miujiza.” Hali ni ya wasiwasi.
5. Tottenham wanacheza pamoja, lakini hali ndani chumba cha kubadilishia nguo ni tata…
Baada ya kufungwa 1–0 na Chelsea, Tottenham – kiwango chao cha chini zaidi kwenye kumbukumbu ya klabu. Pia, tetesi za kutokusalimiana kati ya wachezaji na kocha Thomas Frank zimezidisha mashaka.
6. Haaland – hatari inayoendelea
Erling Haaland aliifungia Manchester City mabao mawili dhidi ya Bournemouth, akibaki kuwa silaha kuu ya mabao. Lakini maswali yanasalia: je, City wana kiwango cha ulinzi wa kutosha kuisukuma Arsenal kwenye mbio za ubingwa msimu huu?
7. Newcastle wanalipa gharama ya kupumzisha nyota
Eddie Howe alifanya mzunguko wa wachezaji ili kujiandaa na Ulaya – lakini wakaadhibiwa na West Ham. Uamuzi huo sasa unajadiliwa kama hatari iliyowagharimu pointi muhimu.
8. Fulham waanza kusisimua mashambulizi
Fulham waliichapa Wolves 3–0, Samuel Chukwueze akionyesha ubora mkubwa. Sasa swali ni moja: wanaweza kudumisha kiwango hiki au ni moto wa kibiriti?
9. Saa inamkimbia Reiss Nelson
Akiwa kwa mkopo kutoka Arsenal, Reiss Nelson hapati muda wa kutosha akiwa na Brentford. Shinikizo linapanda – kwa mustakabali wake na kwa klabu anayochezea sasa.
10. Ubunifu wa Pep – viungo kuwa mabeki wa pembeni
Manchester City sasa wanawachezesha viungo kama mabeki wa pembeni (k.m. Matheus Nunes, Nico O’Riley). Mfumo huu mpya unawapa udhibiti wa mpira na unazidi kuleta matokeo.


Comments
Loading…