*Ataka washabiki watulie, wamwamini
Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal amewashangaa wadau wa klabu hiyo waliompokea kama mfalme, kisha baada ya mechi moja tu sasa wanamchukulia kama shetani.
Mdachi huyo amesema upinzani anaopata pamoja na chagizo kutoka kwa washabiki si sahihi, na kuwa ameshangazwa nazo, akidaiwa eti hajafanya jitihada kujenga kikosi imara, akaongeza kwamba kwenye soko la soka si rahisi kununua au kuuza wachezaji kama watu wanavyodhani.
Alipoulizwa juu ya kinachofanyika katika mchakato wa usajili, Van Gaal alikunja uso, akakaa kimya na kisha kusema watu wanamshangaza kwa madai ya kutaka mabadiliko ndani ya siku chache namna hiyo.
“Wiki mbili zilizopita nilikuwa Mfalme wa Manchester sasa mimi ni shetani wa Manchester. Si rahisi kununua na kuuza kwenye soko hili la soka. Mambo yatakuwa magumu katika miezi mitatu ya kwanza.
Nimeshamwambia Ed Woodward (makamu mwenyekiti mtendaji) na Glazers (wamiliki wa timu). Nimeajiriwa kujenga timu na huo ni mchakato unaohitaji muda,” akasema kwa ukali Van Gaal.
Hadi Ijumaa hii, usajili ambao Old Trafford walikuwa wamekamilisha ni wa Ander Herrera, Luke Shaw na Marcos Rojo na wanaendelea na kufuatilia uwezekano wa kuwasajili Angel Di Maria, Sami Khedira na Xabi Alonso wa Real Madrid pamoja na Arturo Vidal wa Juventus.
Van Gaal amesema kwamba lazima wanachama na washabiki wa United waamini katika falsafa yake na kwamba wajipe muda, yao itarudia kuwa klabu kubwa, akasema halikuwa jambo la ajabu kupoteza 1-2 kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Swansea wiki iliyopita hapo Old Trafford.
Kocha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Ajax na Bayern Munich, anawania kusajili wachezaji wawili kutoka nchini mwake, Kevin Strootman na Daley Blind, lakini haijulikani kipi kinakwamisha mchakato ambao washabiki wanataka kuona majina makubwa yakitua Manchester haraka.
Comments
Loading…