Kocha wa zamani wa Manchester United, Barcelona na Timu ya Taifa ya
Uholanzi, Louis van Gaal amestaafu.
Van Gaal aliyechukua mikoba ya David Moyes baada ya kustaafu kwa Sir
Alex Ferguson hapo Old Trafford kisha akafukuzwa kazi, amemaliza
kipindi cha miaka 26 ya kufundisha soka.
Van Gaal (65) amekuwa bila kibarua tangu alipofutwa kazi na United Mei
2016, anasema aliwaza kwenda likizo lakini ameona bora aondoke kimoja.
βNilifikiria huenda ningeachana na kazi hii, ila baadaye nikaona
niende likizo, bali sasa naona nipumzike moja kwa moja na sitarudi
tena kwenye soka,β Van Gaal amekaririwa na gazeti la Kidachi la De
Telegraaf akisema.
Mdachi huyo amepata pia kufundisha klabu za Ajax, Bayern Munich na AZ.
Serikali ya Uholanzi imempa tuzo ya heshima kwa mafanikio aliyolipatia
taifa hilo na yeye mwenyewe kwenye soka.
Akiwa na Man U alitwaa ubingwa wa Kombe la FA msimu wa 2015/16, lakini
akafukuzwa kazi muda mfupi baada ya hapo. Anasema moja ya sababu za
kuachana na soka ni kifo cha ghafla cha mume wa binti yake.
Anasema amekataa ofa nzuri za kufundisha soka Mashariki ya Mbali,
akitaka zaidi kukaa na familia yake. Enzi zake alicheza nafasi ya
kiungo kwa klabu za Ajax, Royal Antwerp, Telstar, Sparta Rotterdam na
AZ kati ya 1972 na 1987 kabla ya kuingia kwenye ukocha.