*Spurs safi, Liver wabanwa*
Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal amesema timu yake inaweza kuchuana na nyingine kutwaa ubingwa wa England, baada ya kushinda 3-2 dhidi ya Southampton.
Japokuwa haukuwa ushindi rahisi, Mdachi huyo aliyemwanzisha tena mshambuliaji mpya wa kati, Anthony Martial, 19, na akafunga mabao mawili muhimu, anasema kikosi chake kinalipa.
United walitoka nyuma kwa 0-1 kwa bao la Graziano Pelle lililosawazishwa na Martial dakika ya 34 kabla ya kuongeza la pili dakika 16 baadaye. Walifarijika zaidi kwa Juan Mata kufunga bao dakika ya 68 kabla ya Pelle aliyemtesa Daley Blind kufunga la pili kwa Saints.
Ushindi huo umewapandisha United hadi nafasi ya pili, baada ya kujikusanyia pointi 13 kwenye mechi sita, mbili pungufu ya mahasimu wao wa Manchester, Man City. Kwa kufungwa, Saints wameangukia nafasi ya 16 na kocha wao, Ronald Koeman anasema makosa yamewagharimu.
Van Gaal alisema bado kikosi chake kipo kwenye mpito, lakini akasema bado wanaweza kuutwaa ubingwa. Wamepunguza pengo lao dhidi ya City ambao juzi walifungwa na West Ham, ikiwa ni mechi ya kwanza kupoteza.
SPURS SAFI, LIVERPOOL WABANWA
Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspur walifanikiwa kuwafunga Crystal Palace 1-0, ambapo kocha Mouricio Pochettino wa Spurs alisema kipa wake, Hugo Lloris ni wa kiwango cha juu sana kimataifa.
Alikuwa mchezaji wa kimataifa wa Korea Kusini, Son Heung-min aliyefunga bao hilo na kuwapa Spurs ushindi wa kwanza nyumbani msimu huu, pia likiwa bao lake la tatu katika mechi mbili kwa klabu yake mpya.
Kusajiliwa kwake kulimaliza ndoto za Emmanuel Adebayor klabuni hapo, na sasa ameruhusiwa kuondoka kama mchezaji huru, baada ya kupewa malipo kutokana na klabu kukatisha mkataba wake. Heung-min alisajiliwa kutoka Bayer Leverkusen.
Liverpool wakicheza nyumbani Anfield, waliendeleza ulegevu na kwenda sare ya 1-1 na Norwich waliorejea Ligi Kuu msimu huu.
Kocha Brendan Rodgers alimchezesha kwa mara ya kwanza mshambuliaji Daniel Sturridge katika kipindi cha miezi mitano, baada ya kuwa ameumia na kupelekwa nchini Marekani kwa ajili ya matibabu.
Alicheza sambamba na Christian Benteke lakini hawakuweza kupata bao, ndipo mshambuliaji mwingine mpya, Danny Ings akaingia dakika ya 45, akatokea kuwa mchezaji bora wa mechi na ndiye pia aliyefunga bao dakika tatu tu tangu kuingia.
Laiti golikipa wa Liverpool, Simon Mignolet asingefanya makosa langoni na kumzawadia Russell Martin bao, huenda Liver wangeondoka na pointi tatu muhimu. Hata hivyo, kipa huyo aliokoa bao la wazi lililokuwa lifungwe na Matt Jarvis huku Liver wenyewe wakikosa bao kupitia kwa Philippe Coutinho aliyefanikiwa hata kumpiga chenga kipa John Ruddy.
Kocha Rodgers atakuwa na kazi ya kuweka sawa kikosi chake, ama kwa kupanga wachezaji wanaoendana au kwenye mazoezi kumaizi nani anaweza kucheza na nani, kwani katika mechi sita za mwanzo wamepata pointi nane tu.
Msimamo wa ligi unaonesha kwamba West Ham wanashika nafasi ya tatu wakifuatiwa na Leicester, timu ambazo si kawaida kuwa eneo hilo, huku Arsenal wakishika nafasi ya tano wakifuatiwa na Everton.
Swansea wamepanda hadi nafasi ya saba, Palace wameshuka mpaka ya nane, Spurs wakapanda mpaka ya tisa, Watford wameshuka na kuwa nafasi ya 10. Mkiani wapo Sunderland ambao msimu uliopita walizoea sana eneo hilo la kushuka daraja, wakiwa na pointi mbili tu sawa na Newcastle, wakisaidiwa na Stoke wenye pointi tatu.