Kocha mpya wa Manchester United, Louis van Gaal ameanza kuonesha hana mchezo, baada ya kumtoa nje mshambuliaji namba moja wa Uholanzi, Robin van Persie huku timu ikiwa nyuma kwa bao moja.
Van Gaal alimwondosha uwanjani RVP dakika ya 76 Jumapili katika mechi baina ya Uholanzi na Mexico, ambapo Wadachi walishazidiwa nguvu, huku RVP ambaye ni mpachika mabao tegemeo wa Man U akiwa haoneshi cheche.
Hii inaonesha kwamba Van Gaal atafanya maamuzi magumu atakapoanza kazi yake Old Trafford baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Brazi. Anatarajiwa kujiunga na United kwenye safari ya Marekani iwapo Uholanzi itavuka hadi hatua za mwisho.
Kocha huyo alifanya mabadiliko kw akumtoa nahodha wake na kumwingiza Klaas Jan Huntelaar ambaye hatimaye alikuja kuwapatia Wadachi ushindi dakika za mwisho kutokana na bao la penati.
Van Gaal alitaka kuonesha kwamba hakuna mtu ambaye hawezi kubadilishwa kwenye timu yoyote ile, na ndiyo umekuwa mwenendo wake katika timu nyingine alizofundisha kabla, akizingatia sana nidhamu pasipo kuogopa wala kupendelea mchezaji yeyote.
Kocha huyo alibadilisha mfumo wa 5-3-2 na kufanya 4-3-3 na mwishoni aliwaweka Huntelaar na Dirk Kuyt kuwa wamaliziaji pale mbele.
RVP ni Mdachi kama Van Gaal, na amepata kusema kwamba angependa kuwa nahodha wa timu hiyo, nafasi inayowaniwa pia na Mwingereza Wayne Rooney anayepigiwa pia chapuo kumbadili Steven Gerrard anayeelekea kuchwewa na Jua.
Comments
Loading…