in , , , , ,

Utoto, kutojiamini vyamtesa Ozil 

Mchezaji ghali zaidi wa Arsenal, Mesut Ozil hayupo katika hali nzuri, na yaelekea anasumbuliwa na kutojiamini huku akifanya mambo kitoto.

Niliutazama mchezo baina ya Arsenal na  Bayern Munich Jumatano na kushangazwa na jinsi alivyokuwa uwanjani.

Alijitahidi mwanzoni, akajituma na hata kuingia ndani ya eneo la penati ambapo kwa kawaida akishafanya hivyo huwa hafungi bali hutafuta wa kumpa amalizie kana kwamba amezuiwa kufunga.

Lakini safari hii aliangushwa, Arsenal wakapatiwa penati mapema wakiwa na joto la mashambulizi makubwa makubwa na kujiamini.

Lakini alikuwa ni Ozil aliyepiga kizembe na kidhaifu kiasi cha kuwa mboga tu kwa kipa mzoefu Mjerumani, na Ozil akawa anashangaa ameikosaje.

Lakini kwa historia Ozil si mpiga penati, hivyo Arsene Wenger alitakiwa amwengue kabisa kwenye jukumu hilo, maana tumeona sasa zaidi ya mara mbili akizikosa.

Hata kama Mikel Arteta ambaye ndiye mpiga penati mkuu au Olivier Giroud hawakuwapo uwanjani, bado angepewa jukumu hilo mwingine kwa sababu Ozil hajiamini na ikitokea akifunga ni tatizo la kipa wala si umahiri wake. Angepiga Santi Cazorla au hata kipa Wojciech Szczesny.

Inasikitisha kwamba hadi sasa klabu za Ligi Kuu ya England hazijaweza kununua mchezaji mwenye thamani halisi, ambaye akikaa uwanjani anaendana na bei yake.

Unaponunua mchezaji lazima uzingatie mambo kadhaa; uwezo uwanjani, kujiamini kwake na nguvu ya kisaikolojia na kuwa kiongozi wa wengine. Huwezi kuwa aghali halafu ubaki kama mtoto tu.

Bayern na Barcelona sasa tutawaona jinsi watakavyosonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa sababu wanahakikisha wanabaki na wachezaji wao bora zaidi na wachezaji wenyewe hawataki kuondoka.

Tuliona pia Jumanne, timu nyingine ya England, Manchester City ikinyongwa 2-0 na Barcelona licha ya kuwa na wale wanaodhaniwa kuwa wachezaji bora kabisa hapa England, David Silva, Alvaro Negredo na Jesus Navas. Si Barca wala Bayern waliotaka kuwanunua Wahispania hao, maana wameridhika na kikosi walicho nacho.

Bayern nao kadhalika hawakutaka kumnunua Mjerumani mwenzao Ozil, kwa sababu wanaona bado hajakamilika na pengine itachukua muda kumkamilisha anavyotakiwa kuwa hapo Bavaria.

Ozil alipoingia England alianza kwa nguvu sana, lakini kama mshumaa akaanza kuishiwa na sasa amebaki kulalamikiwa na yeye anazidi kukosa kujiamini.

Bayern waliwazidi Arsenal kila idara Jumatano, lakini niwapongeze tu Arsenal kwa jitihada zao za kuzuia mabao zaidi, ikizingatiwa pigo walilopata la kipa wao namba moja kutolewa nje kipindi cha kwanza kwa kadi nyekundu.

Lakini hungeweza kumlinganisha Toni Kroos na Ozi; walikuwa vitu viwili tofauti kabisa katika kila kitu. Kroos ni mwangalifu sana, anavyopokea mpira, anavyotia pasi na hata ikifika kufunga.

Unaweza kumpata Tony Adams katika Kroos na Manchester United pia wanajua thamani yake – ni maji marefu lakini Ozil anaonekana kutochanganyika vyema na wenzake pia.

Ozil anakaribia kuwa kama Zlatan Ibrahimovic wa Paris Saint Germain, lakini tofauti ni kwamba hata Ibrahimovic awe mbaya kiasi gani, anazaa matunda, anapachika mabao na kuipa timu ushindi muhimu. Ozil ameshindwa katika hilo.

Nilishangaa kuona Wenger amemwacha uwanjani muda wote hata baada ya kukiri kwamba ufanisi wake na kiakili hakuwa vyema baada ya kukosa penati. Wapo wachezaji wengine wengi wangeweza kuingia na kufanya vyema kuliko yeye.

Tuliona mechi ya Liverpool na Arsenal kule Anfield, ambapo Arsenal iliweka kikosi kamili wakapigwa 5-1 lakini Emirates akaweka kama kikosi cha pili na vijana wakawasambaratisha Reds.

Haikuwachukua muda Bayer kutambua udhaifu wa Ozil katika kukaba na walitumia fursa hiyo kupata mafanikio kwa upande wa kushoto, ambako pia Kieran Gibbs alikuwa ametoka kwa kuumia na kuingia Mhispaniola, Nacho Monreal.

Ozil alishakosa penati mbili zilizopita, bado anapiga tu, na yeye mwenyewe kama si utoto alitakiwa kukataa anapopewa jukumu hilo.

Unapotumia pauni milioni 42.5 kununua mchezaji mmoja lazima uhakikishe ana vitu vingi visivyopatikana kwa wengine wengi, na hao ni kama walio Bayern na Barca.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal wateswa na Bayern

MECHI TANO VPL KUCHEZWA JUMAMOSI