*Nyodo na dharau kwa timu pinzani, au ni kujiamini?
Uamuzi wa nyota wa Barcelona kucheza penati kwa mtindo tofauti umezua
utata kwenye ulimwengu wa soka.
Wapo wanaodhani kwamba nyota wa Barcelona – Lionel Messi, Luis Suarez
na Neymar walionesha dharau kwa timu pinzani ya Celta Vigo.
Messi ndiye aliyepiga penati, lakini badala ya kupiga moja kwa moja
langoni, akampasia Suarez aliyekuwa nje ya boksi la penati, naye
akautia mpira wavuni.
Penati hiyo ilipigwa Barca wakiongoza kwa 3-1 na baadhi, ikiwa ni
pamoja na kocha wa Barcelona, Luis Enrique, wanaona ilikuwa hatari
kwani uwezekano mkubwa ulikuwa kukosa bao.
Ni kwa sababu hiyo baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba Barca
waliwadharau wapinzani wao, ndiyo maana badala ya kutumia fursa hiyo
ya penati ambayo ni ‘bao kwa zaidi ya asilimia 90’ kuigeuza kama mpira
wa adhabu ndogo.
Neymar anadai kwamba walifanya mazoezi kwa ajili hiyo na kwamba mpira
huo ilikuwa apewe yeye, ila Suarez akauchukua kutoka kwa Messi,
akikimbia haraka kutoka nje ya boksi la penati.
Kiungo wa Barcelona, Andres Iniesta alisema hawakuwadharau wapinzai
wao, akikiri si kitu cha kawaida kupiga vile lakini akafurahi kwamba
mbinu hiyo ilifanya kazi na hakuna haja ya kuwa na mjadala kwenye
hilo.
Katika mechi hiyo Barca walishinda 6-1. Kocha wa Celta Vigo, Eduardo
Berizzo alisema ni njia tofauti ya kupiga penati. Hata hivyo, alidai
wachezaji wa Barcelona hupenda zaidi kujionesha kwa mtindo wanaotumia
kuliko kushinda tu mechi.
Enrique, mchezaji wa zamani wa Barcelona, alisema angekuwa yeye
hangecheza vile, kwa sababu angeweza kuukanyaga mpira, kuanguka na
kukosa bao.
Wengine wanaona kwamba Messi alikuwa akitoa heshima kwa mkongwe wa
zamani wa Barca, Johan Cruyff aliyefanya hivyo akiwa na Ajax 1982.
Arsenal walijaribu hilo dhidi ya Manchester City 2005, lakini Robert
Pires hakuweza kuupata na kuufunga mpira aliopelekewa na Thierry
Henry.