Serikali ya Uswisi imezuia mamilioni ya faranga za Shirikisho la Soka
la Kimataifa (FIFA) yaliyo kwenye akaunti nchini humo, Wizara ya
Sheria ya Uswisi imeeleza.
Hatua hiyo imekuja wakati vyombo vya dola vya Uswisi na Marekani
vikiendesha uchunguzi mkali juu ya mwenendo wa maofisa wa sasa na wa
zamani wa shirikisho hilo lenye makao makuu jijini Zurich, Uswisi.
Maofisa hao, wakiwamo viongozi wakuu, wanatuhumiwa kuhusika na ufisadi
unaojumuisha wizi na utakatishaji wa fedha pamoja na utoaji na
upokeaji wa mlungula kwa sababu mbalimbali, zikiwamo nchi kupata
uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia.
Tuhuma nyingine ni kwa maofisa hao kujihusisha na mlungula kuhusu
utoaji wa haki za matangazo kwenye televisheni katika michuano
mbalimbali duniani na tayari karibu watu 20 wamo katika majalada ya
mashitaka nchini Marekani na Uswisi.
Wizara hiyo ya sheria ya Uswisi ilisema kwamba maofisa wa Marekani
wanaamini kwamba kuna fedha za rushwa katika akauntihizo zilizozuiwa.
Taarifa za vyombo vya habari zinakadiria kwamba fedha hizo ni kati ya
faranga milioni 50 na 100 za Uswisi, sawa na kati ya pauni milioni 34
na 67.
Marekani iliiomba Uswisi kufunga akaunti karibu 50 za FIFA zilizo
kwenye benki 10 tofauti. Inaeleza kwamba viongozi wengi wa FIFA wana
akaunti nchini Uswisi, ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Shirikisho la Soka
la Amerika Kusini, Nicolas Leoz mwenye akaunti zifikiazo 12.
Wakati hayo yakiendelea, Rais wa FIFA aliyesimamishwa, Sepp Blatter
anaelezwa kufika mbele ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA kwa ajili ya kutoa
maelezo yake. Blatter aliyekuwa amepanga kuachia ngazi Februari 26
mwakani baada ya uchaguzi wa dharura ulioitishwa alifika katika makao
makuu hayo na mmoja wa wanasheria wake.
Blatter alisimamishwa kazi sambamba na Rais wa Shirikisho la Soka la
Ulaya (UEFA), Michel Platini, wakidaiwa kuhusika kwenye dili moja ya
mlungula, ambapo Blatter anatuhumiwa kumpa Platini hongo ya pauni
milioni 1.34 mwaka 2011 ili ajitoe kupingana naye kwenye uchaguzi.
Muda mfupi baada ya kupokea fedha hizo Platini aliyekuwa akiungwa
mkono na wajumbe wenye ushawishi mkubwa ili kumwondosha Blatter
kitini, alijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wawili hao wanakanusha kutenda kosa, wakidai ulikuwa mshahara kwa
Blatter aliyepata kuwa mshauriwa ufundi wa Blatter, lakini
kinachoshangaza malipo yalifanyika miezi mingi baada ya kuacha kazi
hiyo na muda mfupi tu kabla ya uchaguzi.
Kamati ya Maadili ya FIFA inaundwa na jopo la majaji wanne
wanaotarajiwa kutoa uamuzi wao mapema wiki ijayo. Wakati Rais Blatter
ndiye aliyeipa kamati hiyo meno na kuwa huru zaidi tangu 2012, sasa
anajenga hoja kwamba haina nguvu ya kumwondosha madarakani rais
aliyechaguliwa na wajumbe.
Blatter anasema hajapata kutenda kosa lolote la ufisadi, ni mtu safi
na ameangukia tu kuwa mwathiriwa wa uchunguzi unaoendeshwa ndani ya
shirikisho hilo. Taarifa zinasema kwamba kuna uwezekano wa Blatter
(79) kupigwa marufuku kujihusisha na soka kwa miaka kadhaa.
Mapema wiki hii, Blatter alitumia vifaa vyake binafsi vya ofisi
kuwaandikia wanachama wote 209 wa FIFA barua kuwatangazia jinsi
asivyokuwa na hatia.
Katika tukio jingine, wanasheria wa Platini walisema Jumatano hii
kwamba wangegomea usikilizwaji wa shauri la mteja wao mbele ya Kamati
ya Maadili ya FIFA, shauri lililopangwa kufanyika Ijumaa hii.
Wanasheria wa Mfaransa huyo wanasema wanaamini kwamba tayari utiwaji
hatiani na hukumu vimeshaandaliwa na mchakato unaoendelea ni kiini
macho tu.