in , , ,

Ushawishi wa Uislamu kwenye utamaduni wa soka EPL

Ligi Kuu ya England (EPL) ilipoanza 1992, alikuwamo mwanasoka mmoja tu aliyejulikana kuwa Mwislamu, naye alikuwa kiungo wa Tottenham Hotspur, Nayim.
Kwa sasa, EPL ambayo ni ligi ya ngazi ya juu zaidi nchini hapa ina wachezaji 40 Waislamu, na kwa kweli wamebadili kwa kiasi kikubwa utamaduni katika mchezo huu.
Februari 5 mwaka 2012, Newcastle United walipocheza na Aston Villa katika dimba la St James’ Park palikuwa na tukio lilioashiria athari za Uislamu katika soka ya Uingereza, kwa mara ya kwanza.
Katika dakika ya 30, Demba Ba aliwafungia bao Newcastle, akakimbilia kwenye kibendera cha kona, akainama, akapiga magoti na kusujudu ardhi kwa nyuso zao, akaungana na raia mwenzake wa Senegal, Papiss Cisse. Wawili hao ni Waislamu wazuri na huuonesha uchaji wao dimbani.
Kumiminika kwa wachezaji Waislamu kwenye EPL kunatokana na soka kuwa ya kimataifa zaidi, ambapo wang’amuzi wa vipaji wametanua nyavu zao kwa ajili ya kunasa vipaji vipya na kuviingiza EPL bila kujali dini wala asili zao.
Ndiyo maana vijana wadogo kutoka maeneo ya vijijini kabisa, hasa huko Afrika Magharibi au pia kwenye maeneo yasiyoendelea sana ya Ufaransa wamenaswa na kutokea kuwa nyota wa kimataifa.
Yawezekana kwamba wamepata utajiri na kuwa maarufu katika klabu za Uingereza, lakini bado wanashikilia kile wanachoona ni cha thamani kubwa katika utamaduni wao, tunu wanayoona inawatia matumaini na kuwalinda – imani ya Kiislamu.
Wakati mchezaji wa kaliba ya Ba alipohama Newcastle na kujiunga na Chelsea mwaka jana, alishikilia kwamba yupo makini na ataendelea kushikilia imani yake hiyo, na kwamba ukubwa wa klabu au kupanda kwake chati hakuwezi kuufunika Uislamu.
Baadhi ya makocha katika klabu hizi mbalimbali kubwa, wanawasikiliza wachezaji Waislamu, wanawaelewa na wameamua kuwapa nafasi ya kutekeleza wanayoyataka kuendana na imani zao za dini.
Wachezaji hawa wa Kiislamu huhitaji kuhakikishiwa, kwa mfano, vyakula wanavyopewa na vinywaji ni halali kuendana na matakwa ya dini yao, kwa hiyo hupatiwa vyakula vyenye nembo ‘halal’ na kama ni wanyama ni wale waliochinjwa na Waislamu.
Kadhalika katika kushikilia usafi kidini, hupewa nafasi tofauti kwa ajili ya kuoga na pia hupatiwa wakati na mahali pa kuswali. Kadhalika, kwa Waislamu ni marufuku kunywa kileo, lakini ushangiliaji wa ubingwa katika mechi nyingi hufanywa kwa kufungua na kumwagiana mvinyo wa champagne. Kadhalika mchezaji bora wa mechi hupewa mvinyo.
Kwa hiyo ni kawaida kabisa siku hizi, wachezai Waislamu, kama akina Yaya Toure kukataa, lakini kwa busara na utulivu zawadi za aina hizo, japokuwa hupokea na kuwapa wenzao baada ya kuhojiwa na wanahabari wa televisheni.
Kadiri muda ulivyokwenda, hata hivyo, champagne imeondolewa katika zawadi kwa wachezaji hao, na badala yake hutolewa vikombe vidogo. Liverpool walipotwaa Kombe la Ligi katika fainali iliyofanyika 2012, wachezaji walikuwa makini, wakaondoa mavazi ya kocha wao Mwislamu kwenye vyumba vya kubadilishia, ili zisimwagikiwe na kilevi walichokuwa wakikifurahia na hata kumwaga huku na kule.
Jambo jingine kubwa linaloibuka siku hizi ni changamoto ya kuwasimamia wachezaji katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo huwapo aina fulani ya shinikizo.
Je, ni kwa vipi wachezaji watakaa bila kula wala kunywa kwa saa 18 hivi halafu waweze kuwa na ufanisi dimbani kwenye mechi kubwa ya dakika 90 au zaidi? Wapo wachezaji wanaosisitiza kufunga siku nzima.
Hata hivyo, wengine hufunga siku za mazoezi tu na si siku ya mechi, ambapo klabu huonekana kujadiliana na kufikia mwafaka ambao wakati mwingine haimaanishi kwamba wamekubaliana kabisa na wachezaji husika wa Kiislamu, na athari zake huonekana katika matokeo ya mechi.
Kiungo wa Arsenal, Abou Diaby (27) anasema klabu yake hiyo inaona ni vyema asifunge wakati wa Ramadhani, lakini kwamba wakuu wake wanaelewa mfungo ni kipindi maalumu kwake, hivyo hujaribu kumsaidia kwa namna moja au nyingine ili asikose raha.
Ba (28) anakiri kwamba wamekuwa na msuguano na baadhi ya makocha nyakati za mfungo wa mwezi wa Ramadhani, lakini anasema yeye hushikilia msimamo wake katika dini yake na kanuni zilizowekwa na utamaduni wao.
“Kila nilipokutana na kocha asiyependa mambo haya, nimekuwa namwambia; ‘sikiliza, nitafanya hivyo, nikiwa na ufanisi unaotakiwa nitacheza, kama sifanyi vyema basi nitupe benchi’, hakuna mjadala,” anasema Ba.
Mpachika mabao wa zamani, Mamady Sidibe (33) anasisitiza kwamba amepata kuona baadhi ya wachezaji wanaofunga hata siku ya mechi lakini wanakuwa na ufanisi mkubwa, na haoni hilo kama ni tatizo kwa namna yoyote ile.
“Hata hivyo mimi huhakikisha siku ya mechi sifungi ili nisisababishe visingizio kwa watu wengine,” anasema.
Ramadhani ya mwaka huu inamalizika Agosti 7, siku 10 kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu ya England.
Mipango ya udhamini na ufadhili wa EPL nayo imekuwa chanzo cha mvutano kwenye masuala haya ya kidini. Timu zinazotangaza kamari na mikopo kwenye jezi zao huwakwaza wachezaji Waislamu na kuwaweka katika wakati mgumu, kwa sababu vinaenda kinyume na mafundisho ya dini yao.
Mwezi uliopita, Cisse alisema alipanga kukaa na kuzungumza na klabu yake ya Newcastle juu ya wadhamini wao wapya, Wonga, kwa sababu ana wasiwasi kwamba imani yake ya Kiislamu itakwazwa iwapo ataitangaza kampuni hiyo ya mikopo.
Mchezaji wa Crewe, Nathan Ellington (32) aliyewahi kuchezea klabu za Wigan na West Brom anasema uvaaji wa jezi hizo si kitu kwa Uislamu, maana ni vitu vilivyo nje ya uwezo wa mchezaji na hawawezi kuzichagulia klabu wadhamini.
Golikipa wa Wigan Ali Al-Habsi (31) anakubaliana na mwenzake huyo, akisema kwamba wao ni wachezaji tu na yote hayo ni mambo yatokanayo na klabu za soka, na hawawezi kuzuia, kazi Kocha wa Newcastle, Alan Pardew aliwahi kusema kwamba Demba Ba hakuanza vyema msimu wa 2011/12 kutokana na kuwa kwenye mwezi wa mfungo, baadhi ya washabiki walianza kushangilia kila bao alilofunga Ba baada ya Ramadhani.
Hata watoto wanaokusanyika na kucheza kwenye viwanja vinavyozunguka Newcastle, wanaonekana kumuiga Ba kwa kusujudu kila wanapofunga mabao, ikiwa ni mtindo wake wa kushangilia.
Hata hivyo, kuna uwezekano kwamba hawaelewi kwa undani maana yake ni nini, lakini ni dalili kwamba vitendo na utamaduni wa Kiislamu unaanza kuzoeleka kwenye utamaduni wa siku nyingi wa Kiingereza.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

UGANDA CRANES YAWASILI KUIKABILI STARS

TAIFA STARS SASA MMEIVA KUPAMBANA- TENGA