Usajili wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2013/2014) sasa
utafungwa Jumatatu (Agosti 5 mwaka huu) badala ya Agosti 3 mwaka huu kama
ilivyokuwa imepangwa awali.
Uamuzi wa kusogeza mbele umetokana kuchelewa kupata disc ya usajili msimu
huu ambayo ndiyo inayotumika kwa usajili wa elektroniki unaofanywa kwa
wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom. Disc hiyo ambayo hutolewa na
kampuni ya NAS Technology ya Tunisia tayari imeshawasili.
Kutokana na mabadiliko hayo, sasa kipindi cha pingamizi kitakuwa kati ya
Agosti 6 na 12 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
itakutana Agosti 13 na 14 mwaka huu kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa
wachezaji wenye matatizo.
Hatua ya pili ya usajili itaanza tena Agosti 15 mwaka huu ikihusisha
wachezaji ambao watakuwa hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu
huu. Timu zitakazoruhusiwa kusajili ni zile ambazo zitakuwa hazijajaza
nafasi zote za usajili. Dirisha dogo za usajili litafunguliwa kuanzia
Novemba 15 mwaka huu hadi Desemba 15 mwaka huu.
Pia klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zinapowasilisha usajili wao zinatakiwa
kuambatanisha nyaraka zinazoonesha viwanja vyao vya mazoezi, nakala za bima
kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi. Masuala hayo yameelezwa kwenye
Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom
*KAMISHNA RWIZA KUSIMAMIA MECHI YA CHAN*
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Rwiza wa
Tanzania kuwa kamishna wa mechi ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Rwiza atakuwa kamishna katika mechi ya kwanza ya raundi hiyo itakayohusisha
mshindi wa mechi kati ya Msumbiji na Namibia dhidi ya Angola itakayochezwa
kati ya Agosti 9 na 11 mwaka huu. Mechi hiyo itachezeshwa na refa Noram
Matemera kutoka Zimbabwe.
Matemera atasaidiwa na Wazimbabwe wenzake Tapfumaney Mutengwa atakayekuwa
mwamuzi msaidizi namba moja, Ncube Salani ambaye ni mwamuzi msaidizi namba
mbili wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Ruzive Ruzive.
Comments
Loading…