Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward, amewataka washabiki wasitarajie mamia kwa mamilioni ya pauni kwa ajili ya usajili msimu wa kiangazi mwaka huu.
Woodward ambaye amekuwa akilaumiwa na washabiki wa United kwa kitambo sasa kutokana na kushindwa kusajili wachezaji nyota kwa sababu ya kuzidiwa kete na viongozi na makocha wa klabu nyingine Ulaya, amesema fedha mwaka huu ni kidogo.
Woodward amesema virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu iliyosababisha kusitishwa kwa ligi vimekuwa na athari kubwa kwa klabu, kwa hiyo washabiki wanatakiwa kuelewa hali halisi ya uchumi ilivyo na si kutaka tu klabu ‘kuvunja’ benki.
United walikuwa wakihusishwa na usajili wa pauni milioni 200 wa mshambuliaji wa Tottenham Hotspur na Timu ya Taifa ya England – Three Lions, Harry Kane. Kadhalika washabiki walikuwa wakisubiri kwa hamu kuona wakimsajili winga wa Three Lions na Borussia Dortmund, Jadon Sancho.
United wana tatizo kwenye ushambuliaji, ambapo tangu wamtoe kwa mkopo Alexis Sanchez na kumuuza Romelu Lukaku huko Italia, wamekuwa wakiwategemea makinda kama Marcus Rashford. Inadhaniwa kwamba badala ya kununua washambuliaji wakali, United watamrejesha Sanchez na kumpa kazi kocha Ole Gunnar Solskjaer kazi ya kumrejeshea makali aliyokuwa nayo enzi za Arsenal na Barcelona.
“Hatakiwi mtu yeyote kufikiria yasiyowezekana juu ya kununua wachezaji kwa mamia ya mamilioni ya pauni wakati inajulikana kiwango cha changamoto ambayo kila mmoja kwenye soka anakumbana nayo. Huu si wakati wa ‘kazi kama kawaida’ kwenye klabu zetu, tukiwamo sie katika dirisha la usajili kiangazi hiki,” Woodward akasema wakati akihutumia ‘Jukwaa la Washabiki’ wa United Ijumaa hii.
Akasema kwamba kipaumbele cha kila mmoja klabuni hapo ni kufanya vyema kwenye mechi na kuchukua makombe mengi kadiri inavyowezekana ndani na nje ya nchi na pia wangependa wasajili wachezaji wakubwa na vipaji vizuri ili kutimiza malengo yao, lakini si rahisi kwa sasa kutokana na mapato kushuka kwa kiasi kikubwa.
Woodward amekuwa akishiriki kwa kiasi kikubwa mijadala miongoni mwa watu wa Ligi Kuu ya England (EPL) na Ulaya juu ya jinsi gemu itakavyokuwa baada ya changamoto ya janga la virusi vya corona.
Mabilioni ya pauni kutokana na mapato ya matangazo ya televisheni bado yameshikiliwa na haijulikani lini ligi kuu itarudia kwa ajili ya kumaliza mechi zake zaidi ya 90, kwani ugonjwa bado umesababisha watu kujifungia ndani, kukiwa na marufuku ya mikusanyiko iliyowekwa na Serikali ya Uingereza.