*Wapigwa 4-0, Ronaldo ndani
Wareno wataikumbuka daima Jumatatu hii kama ‘Blue Monday’ na wengine wataiita siku ya kutokumbukwa.
Matumaini yao makubwa katika nafasi mbili muhimu kwenye Kundi G yalitupwa katika bonde la sahau baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Ujerumani.
Licha ya kuwa na Mchezaji Bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo, Ureno walishindwa kabisa kupata mbinu za kuzuia na kufunga mabao.
Nidhamu pia iliwagharimu, ambapo beki wa Real Madrid, Pepe, alioneshwa kadi nyekundu kwa kutishia kumpiga kichwa mchezaji wa Ujerumani kama wafanyavyo jogoo wanapotaka kupigana.
Jambo hilo liliwagharimu kwa sababu Pepe ni beki, na itabidi wajiulize sana, kwani hii ni kadi nyekundu ya sita kwa Ureno katika mechi 15, na hakuna hata timu moja nyingine ambayo wachezaji wake wameoneshwa zaidi ya kadi tatu katika mechi hizo.
Ujerumani, waliokwishatwaa kombe hili mara tatu, kwa raha zao walipata mabao matatu ya hat-trick ya Thomas Muller.
Alianza kufunga kwa penati dakika ya 12 tu pale Joao Pereira alipomchezea vibaya Mario Gotze.
Mats Hummels alifunga bao la pili kwa mpira wa nguvu wa kichwa kabla ya Pepe kulambishwa kadi nyekundu.
Muller aliongeza bao lake la pili kwa kwa kuchepua mpira kipembeni kabla ya kukomelea msumari kwenye jeneza la Ureno kwa mkwaju wa karibu kabisa na goli.
Ronaldo alicheza licha ya kudaiwa kwamba palikuwapo wasiwasi kama angeweza kutinga dimbani kwa sababu ya goti linalomsumbua, lakini hakuonesha makeke yoyote.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alishangilia kwa nguvu ushindi wa timu yake iliyo kundi moja na Marekani (washirika wake) na Ghana.
Comments
Loading…