Michezo ni moja ya maeneo yanayotumika kutambulisha, kutangaza, kuipatia sifa nchi na hata utajiri kwa wanamichezo wake.
Uendelevu wa michezo huwezekana tu kwa kuenzi mfumo wa kutambua vipaji kutoka ngazi za chini, kuviibua na kuvikuza.
Kutokana na ukubwa wa nchi kijiografia na sababu nyinginezo, nchi imegawanywa katika kanda, mikoa na wilaya.
Njia za makuzi ya watoto zaidi ya nyumbani na katika jamii zao ni pamoja na elimu rasmi shuleni, ambapo Tanzania kwa miaka mingi imeweka pia sera ya kutenga muda wa michezo na taaluma nyingine muhimu kama hii katika shule za msingi.
Huko ndiko lilitokea jina maarufu la UMITASHUMTA, ambalo kirefu chake ni Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania.
Umoja huu mwaka 2012 umefanya michezo yake ya 34.
Serikali katika michezo hiyo iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani, imewataka wadhamini mbalimbali ambao huonekana kwenye klabu kubwa kujitokeza kudhamini michezo hiyo muhimu.
UMITASHUMTA huendeshwa kwa mfumo wa kanda, ambapo wanafunzi huchujana kuanzia ngazi za shule, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi kanda na kupata timu ambayo husafiri kuchuana na wenzao katika mji na mkoa uliopangwa.
Kwa kuwa ni vigumu kuibua na kukuza vipaji mitaani katika kila kona ya Tanzania, UMITASHUMTA ni chemchemi bora ya vipaji vya michezo na taaluma, maana ni mkusanyiko wa waliofanya vizuri tangu ngazi ya chini hadi kanda.
Wadhamini wa aina mbalimbali wakiingia katika eneo hilo, hata pengine kabla ya wanamichezo hao ambao huwa karibu 600 kupatikana na kukusanyika, wanaweza kusaidia kukuza vipaji katika michezo mingi.
Moja ya sifa kuwa za michezo hii, ni kule kushirikisha hata wanafunzi wenye ulemavu, ambao katika baadhi ya maeneo na timu mitaani wamekuwa wakikosa nafasi, licha ya kuwa na kipaji na kuwa na uwezo wa kufanya vyema kuliko wasio na ulemavu.
Kwa mfano, katika UMITASHUMTA kuna soka ya wasiosikia (visiwi), ambapo ni burudani na faraja kubwa kuwaona vijana hao wanavyotumia vipaji vyao kucheza na kushindana.
UMITASHUMTA kwa miaka mingi imekuwa ikidhaminiwa na serikali peke yake, na uzoefu umeonyesha wazi kwamba wadau zaidi wanapojitokeza kuchangia nguvu katika michezo, mafanikio makubwa hupatikana.
Ukweli ni kwamba, wachezaji wanaotamba kwenye michezo mbalimbali katika ngazi za juu walianzia chini, na laiti vipaji vyao visingetambuliwa na kukuzwa kwa njia moja au nyingine, ni wazi hawangefikia mafanikio yao.
UMITASHUMTA kimsingi inatakiwa kushirikisha michezo mingi na taaluma kadhalika, na zamani ilikuwa na mvuto mkubwa.
Kujitokeza kwa wadau wengi kwenye udhamini, na pia waandaaji kutayarisha mapendekezo ya uboreshaji wa mfumo wa mashindano yenyewe, kunaweza kubadilisha picha yake kwa njia chanya.
Pamoja na kushirikisha michezo mingi zaidi rasilimali za kutosha zikipatikana si vibaya wanamichezo nao wakaongezeka kutoka kila kanda na pia siku za michezo, ili kuweka alama isiyofutika ya mashindano ya kihistoria, na kutokana nayo, waibuliwe wachezaji wenye ushindani mkubwa.
Huko ndiko kuinua michezo, huko ndiko kulijenga Taifa Tanzania katika jukwaa la kimataifa, na ni tangazo tosha kwa utajiri wake wa maliasili.
Lakini pia huo utakuwa mwanzo wa utajiri kwa wanafunzi watakaotokea kuwa wanamichezo hodari na kuibuka kimaendeleo, kwani michezo kimataifa sasa ni moja ya maeneo yanayolipa sana kiuchumi.
Hii inaweza kufungua ukurasa mpya kwa familia zao, nyingi zikiwa za kipato cha chini na cha kati, na itakuwa fahari kwa jamii na taifa kwa ujumla. Tuikuze UMITASHUMTA ili iwe chemchemi ya kweli itakayobubujisha maji – wanamichezo kutoka kwenye visima, yaani mikoa na kanda mbalimbali nchini Tanzania.