Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) hukutanisha wachezaji waliochujwa kutoka shule mbalimbali, mfumo wa mashindano yao ni kwa kanda.
Pamoja na kuchanua kidogo kwa umoja huu, kwa maana ya wachezaji walioanzia huko kung’ara kitaifa na kimataifa, nguvu zaidi zinatakiwa kuwekezwa.
UMISSETA ni eneo la mpito kwa wanamichezo wanaochipukia, wakiwa wametokea ngazi ya chini ya UMITASHUMTA. Kutoka ngazi yao, wanaweza kuingia kwenye ushindani zaidi wa michezo ndani na hata nje ya nchi.
UMISSETA hushirikisha wanafunzi kwenye michezo ya Bao, Kikapu, Kurusha Tufe, Meza, Netiboli, Mikono, Riadha, Soka na Wavu.
Hiyo ni michezo ambayo ikifanyiwa kazi ipasavyo, hakuna shaka wanafunzi watachanua vyema, kila mmoja kwa eneo lake na kuipa nchi eneo pana la kujidai badala ya kutegemea mchezo mmoja au miwili tu.
Vijana watachanua zaidi ikiwa patakuwapo msingi imara kwenye UMITASHUMTA na kisha uendelevu katika hatua hii muhimu ya UMISSETA. Bila hivyo, ama vipaji vitapotea au nguvu ya ushindani kitaifa na kimataifa kwa mashindano ya wakubwa itafifia sana.
Moja ya maeneo ya kuboresha ni kuwa na uendelevu wa michezo ya wenye ulemavu katika UMISSETA. Rasilimali zaidi zinatakiwa ili mashindano yawe ya nguvu, maana hili ni eneo la kati la kujiimarisha kabla ya vijana kwenda kwenye ngazi ngumu zaidi.
Pamoja na mahitaji ya maboresho, ni haki kuwapongeza wahusika wa UMISSETA, walau kwa kutaja matunda yanayoonekana, ili wadau wayafahamu.
Mashindano haya yamesaidia kukuza vipaji vilivyowika au vinavyoendelea kuwika katika michezo mbalimbali.
Mmojawapo ni Mwanamichezo Bora wa mwaka 2011 nchini Tanzania, Shomari Kapombe, aliyefikia ngazi ya kuchezea mabingwa wa soka nchini. Kwa ushindi huo, Kapombe amejichumia Sh milioni 13, ambazo si haba kwa mazingira yetu.
Wachezaji wengine wa Ligi Kuu ya Tanzania na timu ya taifa kwa nyakati tofauti waliotokana na UMISSETA ni Danny Mrwanda; Mrisho Ngassa; Juma Kaseja na Henry Joseph.
Mrwanda na Joseph wamepata kuchezea au wanachezea timu za nje ya nchi, tena nje ya Bara la Afrika.
Kwa hiyo licha ya UMISSETA kuzalisha wachezaji mahiri kwa michezo ya wakubwa ngazi ya taifa, ni eneo linaloweza kutoa wachezaji wa kulipwa, wanaojipatia kitita kikubwa ndani au nje ya nchi.
Licha ya soka, hivi sasa mchezo wa Kikapu unatamba nchini Marekani, na uzuri ni kwamba wadau wa huko wamekuwa wakifika nchini kusaka wachezaji wenye vipaji, wanaocheza au kuweza kufundishika kukicheza.
Michezo mingine pia ina nafasi ya kuwafikisha mbali vijana wetu, ikiwa watajituma ipasavyo, uongozi utaweka mikakati mizuri, kuitangaza na wadau kujitolea kuendeleza wanamichezo vijana.
Bado tunakumbuka sifa iliyopata nchi kwa wanamichezo aina ya Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa, Mwinga Mwanjala, Gidemus Shahanga na wengine wengi waliotamba kimataifa.
Nani atawasahau akina William Isangura, Salehe Simba, familia ya Matumla na wengineo walivyowachachafya wapinzani wao kwenye ngumi hadi wakaogopeka duniani?
Hiyo ndiyo sura ambayo UMISSETA inatakiwa kuirejesha Tanzania katika sifa waliyoleta wanamichezo hao, ikiwezekana sifa kubwa zaidi.
Comments
Loading…