Menu
in , ,

Ukuta wa Simba ni mali ya Che Malone

KAMA kuna mambo ya kusisimua katika kikosi cha Simba sio wale washambuliuaji na viungo pekee. Ukitaka kuwatazama vizuri Simba angalia kila kona, upande wa kulia, kushoto, mabeki wa kati na viungo. Kati ya nafasi zote ambazo zinasifiwa sijaona nyimbo za shangwe zinazoeelekezwa kwa Che Malone. 

Je ni beki wa aina gani?

Nimebahatika kuonana na Che Malone. Ni mpole awapo nje ya mpira. Ni mtu makini na mtulivu. Unapoonana naye ana kwa ana nje ya majukumu yake ya mpira huwezi kuamini huyu ndiye mmilikiwa safu ya ulinzi ya Simba. Katika hali ya ubinadamu Che Malone ni mtu ambaye pengi si rahisi kuzoeleka kwa watu asiowazoea. Ni beki ambaye hana kimo kirefu kama Kennedy Juma wa Simba au Bakari Nondo kapteni wa Yanga. Che anakuwa mchezaji mwingi wa upole na kuna wakati unaweza kushangaa huyu ni mtu  wa namna gani. Lakini katika uchezaji alioonesha Simba anaendelea kuwa mhimili kikosini.

Je anaweza kumiliki namba yake?

Katika safu ya ulinzi ya Simba Che Malone ameletewa mabeki au kucheza na mabeki kadhaa lakini amebaki kuwa mhimili. Katika kikosi cha Simba amecheza na Inonga Baka wa DRC na ushirikiano wao ulionekana ni wa kawaida. Inonga Baka ni mchezaji mzuri, ana kimo kizuri lakini anakabiliwa na tatizo la hasira. 

Katika safu ya ulinzi ya Simba alikuwa mchezaji bora ndani ya kiwanja lakini alizidisha ulalamishi. Alikuwa beki ambaye analalamika mno na kamera za Televisheni zilionesha vitendo vyake. Katika soka, mchezaji anatakiwa kutoa ushirikiano na kuzungumza pale anapoona inafaa sio kurusha maneno na mikono. 

Che Malone ni beki anayeelekeza. Uchezaji wake ni ule wa kutaka kila kitu kiende vizuri kwa kupeana mawaidha ya mbinu kadhaa. Mara nyingi kumwona Che Malone akilalamikia mchezaji mwenzake ilikuwa dhidi ya Yanga msimu uliopita ambapo Simba walibugizwa mabao 5-1. Katika mchezo ule Che Malone alionekana kumlalamikia golikipa wake Aishi Manula. 

Hata hivyo kadiri mchezo ulivyokuwa unaendelea ulionesha yuko tayari kwa kuipigania Simba. Ukiacha Inonga Baka, pia amepangw ana beki Kennedy Juma, lakini hawakuweza kutengeneza kombinenga ya nguvu. Kwahiyo utaona Che Malone amekuwa mhimili mkubwa katika safu ya ulinzi ya Simba na ameletewa wachezaji kadhaa lakini wote wameshindwa kuchukua nafasi yake.

Je ana kitu gani msimu huu?

Tangu kuanza kwa msimu huu Che Malone amekuja na kitu kingine ambacho alikificha. Tangu alipojiunga na Simba Che Malone hakuonesha kuwa beki mwenye kasi namna hii. Ni beki ambaye anacheza kwa kasi pale apotakiwa kuzuia mashambulizi. Vilevile Che Malone ameonesha kasi hata kwenda kushambuliaji langoni mwa adui ndiyo maana alifanikiwa kufunga bao mechi ya hivi karibuni.

Hadi timu zinaingia katika mechi za 7 za msimu wa Ligi Kuu, Che Malone amekuwa mchezaji mwenye misuli ya kutosha tofauti na misimu iliyopita. Uwezo wa matumizi ya nguvu au utimamu wa mwili umeongezeka kuliko awali. Uchezaji wake unaonekana ameimarika katika matumizi ya mwili na anapambana navyo vyote kwa pamoja;- nguvu, maarifa,kasi na zaidi ufanisi katika kushambulia umeongezeka. Che Malone ameboresha kiwnago chake katika eneo hili na kufanya washindani wake klabuni kuwa na wakati mgumu kumpora namba.

Je muono wake ukoje?

Tanzania Sports
Che Malone

Ingawaje misimu iliyopita alikuwa na mabeki wengine lakini msimu huu anaonekana kuridhishwa na kombinenga yake na Ibrahim Hamza. Uchezaji wao na mgawanyo wao wa majukumu pale wanapokabiliwa na shinikizo la mashambulizi ni ule ambao unawafanya wazungumziwe kuwa na maarifa makubwa katika kufanya uamuzi. 

Tangu mwanzo, Che Malone alikuwa ni beki anayependa kuzuia kutoka eneo lake kuelekea upande wa kati-kulia, lakini sasa amekuwa akihakikisha ‘anatembea’ eneo lote la nyuma. Ni sawa na kusema Che Malone amekuwa mlinzi wa walinzi wa Simba. Badala ya kumlinda golikipa wao, yeye anawalinda walinzi na amesafisha makosa ya mwenzake na viungo mara kadhaa. 

Mabadiliko haya yanaonesha kuwa benchi la ufundi linafanya kazi nzito kuhakikisha beki huyo anaimarika zaidi. Ingekuwa uswahilini kwetu tungesema “Che Malone anapiga kazi sio mchezo” au tungesema “ni jembe la maana”. Kwamba wamefanikiwa kuupata ule ubora wake katika nafasi ya ulinzi. Bila shaka Simba wataendelea kumlinda mlinzi huyo kama mboni za jicho kwa kuhakikisha hasajiliwi na vigogo wa soka barani Afrika.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version