*Ni kashfa mpya juu ya uenyeji wa fainali za 2006
*Mlungula wa $250,000 uliwakosesha Afrika Kusini
*Blatter alipigana kufurahisha wote na abaki rais
Tuhuma za kashfa za rushwa ndani ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinazidi kutolewa, safari hii ikidaiwa kwamba Ujerumani walihonga ili kupata uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2006.
Habari hizi za kushitua zimekuja wakati maofisa wa Marekani na Uswisi wakichunguza tuhuma dhidi ya maofisa waandamizi wa Fifa, baada ya wengine 14 kufunguliwa majalada na kushitakiwa nchini Marekani kwa rushwa, wizi na utakatishaji fedha.
Mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi, Andrew Jennings, katika andiko lake anaeleza kwamba ulisukwa mkakati wa kuhakikisha Ujerumani wanakuwa wenyeji wa fainali za 2006 kwa rushwa kutolewa kwa mmoja wa wapiga kura wa Fifa kwa ajili ya mwenyeji kujtoa.
Mpango mzima, anaendelea kusema, ulishirikisha watu watatu muhimu mnamo 2000; bilionea wa Ujerumani anayemiliki kituo cha televisheni, Leo Kirch, mmoja wa wanasoka wa zamani wanaoheshimika zaidi nchini Ujerumani, Franz Beckenbauer na ‘mshenga’ Fedor Radmann.
Mbinu hizo chafu zinadaiwa zilitumika kuhakikisha Ujerumani wanapewa uenyeji, na iwapo uchunguzi utathibitisha ukweli, kuna uwezekano wa maofisa zaidi, akiwamo Rais wa Fifa, Sepp Blatter kushitakiwa, hivyo akatakiwa kuachia ngazi mapema.
Kazi mpya imeanza ya kufanya uchunguzi juu ya jinsi uenyeji wa fainali mbalimbali za Kombe la Dunia ulivyokuwa ukitolewa na kitabu cha Jennings kiitwacho ‘The Dirty Game’, kinaweza kuwafungua macho zaidi wapelelezi na umma kwa ujumla.
Ulimwengu wa soka ulishitushwa Mei mwaka huu, pale askari polisi wa Uswisi walipovamia hoteli ya nyota tano jijini Zurich walikokuwa maofisa waandamizi wa Fifa, na kukamata saba kati yao. Wengine saba wamejumuishwa kwenye kashfa za rushwa, wizi na utakatishaji fedha, kutoka maeneo mbalimbali, hasa Asia na Amerika.
Jennings anawapa maofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) mwelekeo wa ushahidi wa kile ambacho kimekuwa kikitendeka Fifa kwa miongo kadhaa sasa na kuchafua shirikisho linalosimamia mchezo unaopendwa zaidi duniani.
Mwaka 2000, wakati njama zilipopangwa na kutekelezwa, Blatter alikuwa vitani kuhakikisha kwamba anahifadhi kiti chake kwenye uchaguzi ambao ungefuata 2002, Ulaya ilikuwa imekasirishwa jinsi Blatter na aliyemfunda, Joao Havelange walivyofanikiwa kuwarubuni wapiga kura kwenye uchaguzi uliotangulia 1998 jijini Paris, Ufaransa.
Inaelezwa kwamba mpango mkakati ulikuwa kwamba zifanyike njia zozote zile, halali na batili, kuhakikisha mwenyeji wa 2006 anatoka Uefa, kwani hilo lingewapoza wakuu wa shirikisho hilo la soka Ulaya kwa sababu maofisa wake wangepata kazi na tiketi kwenye michuanohiyo, hivyo ingekuja kuwa rahisi kumrejesha madarakani Blatter miaka miwili baadaye.
Zabuni ya Ujerumani ilikuwa katika matatizo mwaka 2000 kwani Afrika Kusini walionekana kuongoza katika kupata kura za wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Fifa. Hali hii haikumpendeza Kirch na chaneli zake za televisheni zilizo Munich.
Basi, ikawa kwamba Radmann alikuwa mjanja juu ya kipi cha kufanya kumaliza tatizo hilo. Kirch ndiye aliyekuwa na fedha na Beckenbauer angeweza kusaidia kwenye eneo jingine, kwa sababu ndiye alikuwa rais wa Bayern Munich.
Mpango wenyewe ulikuja na ratiba za ajabu katika mechi za soka, hasa kwa timu ya hadhi ya Bayern, iliyopangiwa kucheza na Timu ya Taifa ya Malta, ambapo zingelipwa ada zisizo za kawaida za televisheni kufikia dola 300,000 katika haki za televisheni zikalipwa kwa vyombo vya habari vya Kirch katika akaunti ya benki isiyotajwa iliyokuwa Malta. Wakati huo, Rais wa Chama cha Soka cha Malta, Joe Mifsud alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Fifa.
Ada nyingine kubwa ililipwa kwa Bayern kwa ajili ya kucheza na Timu ya Taifa ya Trinidad. Wakati huo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Trinidad, Jack Warner, mmoja wa washitakiwa wa FBI sasa, alikuwa pia mjumbe kwenye chombo hicho cha juu cha Fifa.
Huyu amekuwa akihusishwa na mlungula hivyo kwamba kuna wanaoamini kwamba hata akiwa amelala anaweza kuota na kuunyoosha mkono wake ili apokee rushwa. Mechi hiyo haikufanyika, lakini mwaka mmoja tu baadaye, Warner alipewa haki za TV Caribbean kwa fainali za Kombe la Dunia 2002 na 2006.
Dili jingine la ajabu lilikuwa kwa Bayern kusafiri hadi Tunis, Tunisia kucheza na timu ya Espérance. Rais wake, Slim Chiboub ameoa mtoto wa aliyekuwa Rais wa Tunisia, Ben Ali anayedhaniwa alitia shinikizo kwa wajumbe wa Tunisia waliokuwa na nafasi Fifa. Hapa Bayern wangelipa gharama wenyewe.
Wakati upigaji kura wa mwaandaaji wa fainali za 2006 ukikaribia, kulikuwa na hofu kwamba Ujerumani na Afrika Kusini wangefungana kwa kura 12 kila mmoja. Hapo Blatter angetakiwa kupiga kura ya turufu kuchagua nchi mwenyeji. Naye akasema angeipigia Afrika Kusini, ili kujihakikishia kura kwenye uchaguzi uliokuwa unafuata.
Kura awamu ya kwanza zilishuhudia England wakipata tano, na katika awamu ya pili Ujerumani na Afrika Kusini walifungana wakipata kura 11 kila mmoja, England wakapata mbili na kutupwa nje ya kinyang’anyiro. Mmoja wa wapiga kura wa England alikuwa Charlie Dempsey wa New Zealand aliyeagizwa na Oceania aipigie kura England na wakitolewa awapigie Afrika Kusini. Hapa, hata kama Ujerumani. Hapo, hata kama Ujerumani wangepata kura nyingine iliyokuwa ikieleaelea matokeo yangekuwa sare, hivyo Blatter angepitisha turufu kuwachagua Waafrika, hivyo matokeo yangekuwa wazi – tuonane Cape Town 2006.
Haya, kura zikapigwa na matokeo ya mwisho yakawa ya kushangaza – Ujerumani kura 12 na Afrika Kusini 11, tuonane Munich 2006! Kwa nini nasema matokeo yanashangaza? Hizi ni kura 23, ina maana mjumbe mmoja hakupiga, naye ni nani? Ni Charlie Dempsey. Huyu alitoka nje ya ukumbi wa kura, na walati zikipigwa alishafika Uwanja wa Ndege wa Zurich kupanda ndege kurudi nyumbani.
Habari zilizosambaa mara moja ni kwamba miongoni mwa wale watu watatu muhimu wa kutengeneza mpango wa Ujerumani kufanikiwa, yaani ‘mshenga’ Radman, alimuweka sawa Dempsey. Baada ya kusoma ‘ramani’ na kuona matokeo yangeishia kwa kura 12-12 baina ya Ujerumani na Afrika Kusini kisha Blatter atie turufu yake kwa Waafrika, Dempsey aliambia isifike huko.
Kwamba kabla tu ya kura aondoke mkutanoni, arudi kwenye Hoteli ya Dolder Grand ambako angekuta mkoba umefichwa katika kabati la nguo chumbani mwake. Alifanya hivyo, na hamad, ulikuwa na dola 250,000! Akauchukua na pale pale teksi ilikuwa inamsubiri kumkimbiza uwanja wa ndege arudi zake nyumbani. Mwisho wa mchezo.
Jennings anasema alimwandikia Radmann kumuuliza juu ya mchongo huo kwa ajili ya 2006, akajibu kwamba hakuwa akifahamu chochote juu ya kumshawishi Dempsey kususa kura. Akadai yeye si Fedor Radman aliyetajwa kwenye kimemo cha siri cha mipango ya kugawa mlungula kwa timu za kigeni ili zicheze na Bayern Munich, na kwamba angekuwa ni mtu mwingine wanayefanana tu majina.
Kwa Ujerumani kupata uenyeji huo, Ulaya ilifurahi hivyo ingempa kura Blatter miaka miwili baadaye, na walifanya hivyo wakati ulipowadia. Lakini Blatter alikuwa na kibarua cha kuwaliwaza Waafrika kutokana na kitendo kile dhalili. Hakukosa njia; alisema kwamba siku zijazo fainali hizo zingekuwa zikizunguka kwenye mabara tofauti na Afrika wangepata fursa hiyo 2010. Kweli ilikuwa hivyo, Afrika Kusini walikuwa wenyeji, Blatter akaendelea kupeta kila uchaguzi.