*Golikipa wa Zambia shujaa wa mechi*Burkina Faso wawazamisha Ethiopia
Uhondo umeanza kuonekana kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ikiwamo uhodari wa golikipa wa Zambia, Kennedy Mweene. Nahodha huyo wa Chipolopolo alimzidi ujanja nyota wa Nigeria, John Obi Mikel anayekipiga Chelsea, kiasi cha kupigisha penati yake kwenye mlingoti wa goli. Hata hivyo, Nigeria walioonekana kudhamiria kupata ushindi na kujihakikishia kuingia robo fainali, waliongeza shinikizo na kupata bao dakika ya 57 kupitia kwa Emmanuel Emenike. Pamoja na kucheza vizuri, Zambia walionekana kukosa ari ya kushinda mechi, kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga. Hali ilikuwa hivyo hadi mechi ilipoelekea dakika 10 za mwisho, ndipo ikatokea bahati ya penati, na Mweene akasonga mbele kuipiga. Alionekana kama vile angekosa kwa jinsi alivyoutenga mpira, lakini likawa funzo kwa Mikel jinsi ya kupiga penati, akiikwamisha upande wa juu wa lango, huku golikipa Vincent Enyeama akilala upande wake wa kulia. Penati hiyo ilitolewa baada ya Ogenyi Onanzi kumchezea rafu Emmanuel Mayuka. Baada ya kuifunga, Mweene alitumia muda mwingi kusali, kama alivyorudia tena baada ya kipenga cha mwisho. Zambia ndio mabingwa watetezi, lakini mwaka huu wanaonekana kuwa na kazi ngumu ya kulipeleka tena kombe nyumbani Lusaka, kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa timu ndani na nje ya kundi lao la C. Kocha wa Zambia, Herve Renard aliyewawezesha kutwaa kombe mwaka jana, anasema amefurahishwa na ushindi, hasa kwa kuzingatia mazingira yenyewe. Katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo, Ethiopia walikosa penati dhidi ya Zambia pia. Hata hivyo, Chipolopolo wangeweza kupata bao jingine, kama Stopila Sunzu angetumia vyema makosa ya kipa Enyeama kutema shuti la Chisamba Lungu kwa kulenga goli. Rainford Kalaba naye alikosa goli la wazi akiwa ndani ya eneo la penati, kwanza akisita kupiga mpira, kisha kuusukuma taratibu na kuwa mboga kwa golikipa Enyeama. Kepteni wa Chipolopolo, Chris Katongo aliyechangia kwa kiasi kikubwa utwaaji kombe mwaka jana, Ijumaa hii alionekana kutokuwa fiti, na ilibidi atolewe na nafasi yake kujazwa Collins Mbesuma aliyerejesha uhai upande wa ushambuliaji. Kwa ujumla Zambia imekuwa tofauti tangu wakati wa maandalizi, ambapo kwenye maandalizi ilifungwa na Tanzania bao 1-0 jijini Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Chelsea, Victor Moses aliingia kipindi cha pili kwa Nigeria, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kwenye mashindano ya mwaka huu. Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Burkina Faso walijitofautisha na wengine, kwa kutoa kipigo kikubwa zaidi katika fainali hizi, huku wakiwa pungufu kwa mchezaji mmoja. Wakiwa mbele kwa bao moja dhidi ya Ethiopia, Burkina Faso walimpoteza golikipa wao, Abdoulaye Soulama baada ya kupewa kadi nyekundu dakika ya 58 kwa kudaka mpira nje ya eneo lake. Ilimchukua mwamuzi muda mrefu kufikia uamuzi, na pia muda mwingine kwa Burkina Faso kumtoa mchezaji mwingine ili golikipa wa akiba aingie. Kwa kuwa na faida ya mchezaji mmoja wa ziada, Ethiopia walidhaniwa wangefanikiwa kusawazisha na hata kupata ushindi, kwani walishaanza kuliandamana lango la wapinzani wao. Hata hivyo, mipango madhubuti ya kocha wa Burkina Faso, Paul Put, kuingiza wachezaji wengine na kubadili mfumo wa uchezaji. Hayo yaliimarisha safu zote, wala pengo la mchezaji mmoja halikuonekana, wakahitimisha dakika 90 kwa kuwakung’uta Ethiopia mabao 4-0. Walipata bao la kwanza dakika ya 34 lilofungwa na Alain Traore, aliyerudia tena kumsalimu golikipa dakika ya 74. Dakika tano baadaye, Djakaridja Kone alipachika bao la tatu na kuwakatisha tamaa Wahabeshi, kabla ya kiungo aliyekuwa akitengeneza mabao hayo, Jonathan Pitroipa alipigilia msumari wa mwisho. Kwa matokeo hayo, Burkina Faso wamejiwekea mazingira mazuri ya kuingia robo fainali, kwani wanaongoza kwa pointi nne na mabao matano. Wanafuatiwa na Nigeria na Zambia wanafungana kwa pointi mbili na mabao mawili mawili huku Ethiopia wakishika mkia kwa pointi yao moja. Jumamosi hii Ivory Coast wanashuka dimbani kutoana jasho na Tunisia, wakati Algeria watacheza na Togo. |
Comments
Loading…