*Ronaldo aweka hai matumaini ya Ureno
*England walala kwa Chile mechi kirafiki
Kipigo cha mabao 2-0 walichopata Ufaransa nchini Ukraine kinawaweka pabaya katika harakati za kufuzu Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Itabidi Wafaransa wacheze kufa na kupona kwenye marudio nyumbani kwao ili wavuke mtihani huu mgumu, na kitakuwa kipindi kigumu kama hawatafanikiwa.
Timu zote zilimaliza mechi na wachezaji 10, baada ya Laurent Koscielny wa Ufaransa na Olexandr Kucher kuzawadiwa kadi nyekundu dakika za mwisho.
Wakati wakitolewa tayari majanga yalishawakuta Wafaransa, kwani Ukraine walishapata mabao yao, la kwanza likifungwa na Roman Zozulya aliyetengewa pande na Andriy Edmar.
Hali ilizidi kuwa mbaya kwa Wafaransa baada ya Koscielny kumwangusha Zozulya na kusababisha penati iliyofungwa na Andriy Yarmolenko.
Kocha Didier Deschamps atalazimika kuwapanga upya vijana wake, ambao walitarajiwa kufanya vyema maana wengi wao wanacheza katika Ligi Kuu ya England (EPL)
URENO YAAMBULIA MOJA KWA SWEDEN
Katika mechi nyingine kali, Ureno walipata bao moja katika robo saa ya mwisho baada ya Sweden kugangamala tangu mwanzo wa mchezo.
Cristiano Ronaldo ndiye aliyevunja kizingiti cha Waswidi katika dakika ya 82 kwa kupiga mpira wa kima cha nyoka kutokana na majalo nzuri ya Miguel Veloso.
Sweden walikuwa wakali, ambapo waliotamba zaidi ni akina Johan Elmander, Sebastian Larsson na Kim Kallstrom.
Itasikitisha, hata hivyo, katika michuano ijayo kukosa moja kati ya timu mbili hizo bora – Ureno na Sweden. Marudiano yatafanyika katika dimba la Solna’s Friends Arena Jumanne hii.
ENGLAND WAPIGWA NA CHILE 2-0
Timu ya Taifa ya England, Three Lions wamekubali kichapo kutoka kwa Chile katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Wembley.
Chile wamerudia kile walichokifanya 1998 katika dimba hili hili, ambapo usiku wa kuamkia Jumamosi hii Alexis Sanchez wa Barcelona ndiye aliyemnyong’onyesha Roy Hodgson katika mechi muhimu ya majaribio.
Wakati ule, 1998, alikuwa Marcelo Salas aliyewaaibisha England lakini katika mechi hii England watajilaumu wenyewe kwa sababu hawakucheza kama timu, bali kila mtu kwa jitihada binafsi.
Hodgson aliwachezesha kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake wachezaji wa Southampton,
Adam Lallana na Jay Rodriguez pamoja na kipa wa Celtic, Fraser Forster.
Hata hivyo, hao hawawezi kulaumiwa, kwa sababu wachezaji wazoefu wa England ndio walioonekana kucheza hovyo na kukatiza mfululizo wa mechi zao 10 bila kufungwa.
Washabiki walisikika wakiwazomea wachezaji wa England baada ya kipenga cha mwisho lakini bado kuna kazi nzito katika mechi nyingine Jumanne hii dhidi ya Ujerumani katika dimba hili hili.
MATOKEO YA MECHI NYINGINE
Katika mechi nyingine za kirafiki, Korea Kusini waliwafunga Uswisi 2-1; Belarus wakaenda suluhu na Albania; Jamhuri ya Czech wakawafunga Canada 2-0; Urusi na Serbia wakatoka 1-1 na Estonia wakawaadhibu Azerbaijan 2-1.
Matokeo mengine yalishuhudia Denmark wakiwapiga jirani zao Norway 2-1; Uturuki wakawashinda Ireland Kaskazini 1-0; Italia wakaenda sare ya 1-1 na Ujerumani; Poland wakalala 0-2 kwa Slovakia; Jamhuri ya Ireland wakawachakaza Latvia 3-0 na Scotland wakaenda suluhu na Marekani.
Comments
Loading…