Kenya waongoza kwa medali
*Wawili wanaswa kwa dawa
Wanariadha wa Kenya wameonesha mafanikio makubwa kwenye michuano ya ubingwa wa dunia wa riadha, nchi yao ikiwa juu kwenye jedwali la medali.
Hadi alasiri ya Ijumaa hii, Kenya walikuwa wamejikusanyia medali sita za dhahabu, ambazo hakuna nchi nyingine iliyopata idadi hiyo; tatu za fedha na mbili za shaba.
Kenya wanafuatiliwa na Marekani wenye medali tatu za dhahabu, nne za fedha na tano za shaba huku Jamaica wakiwa na tatu za dhahabu na mbili za shaba. Uingereza ndio wanafuata wakiwa na medali tatu za dhahabu na moja ya fedha.
Nafasi ya tano inashikwa na Poland ambayo wanariadha wake wamepata medali mbili za dhahabu, moja ya fedha na tatu za shaba.
Cuba wana dhahabu mbili na fedha moja. Wenyeji China wametokezea nafasi ya saba, wakiwa na medali moja ya dhahabu, nne za fedha na moja ya shaba.
Ujerumani wanafuatia nafasi ya nane baada ya kutwaa dhahabu moja, fedha mbili na shaba mbili. Nafasi ya tisa imeenda kwa Ethiopia wenye medali moja ya dhahabu na mbili za fedha. Canada wanafunga 10 bora kwa medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba.
Nchi nyingine zenye medali moja moja ya dhahabu ni Afrika Kusini, Colombia, Jamhuri ya Czech, Eritrea na Hispania. Katika 18 bora wamo Bahamas, Uholanzi, Ausralia, Brazil, Croatia, Misri, Israel, Urusi, Tajkistan na Tunisia.
Kenya wamepata pigo kwa wanariadha wake wawili, Joyce Zakary, 29, na Koki Manunga, 21, kusimamishwa kushiriki mashindano hayo, baada ya vipimo kuonesha kwamba walitumia dawa za kuongeza nguvu.
Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) limetangaza hatua hiyo na kwamba wanariadha hao walioshiriki katika mbio za mita 400 na zile za kuruka vihunzi kwa umbali huo huo walifanyiwa vipimo hivyo kwenye hoteli ambayo timu yao ilifikia na wamekubali hatua dhidi yao.
Zakary aliweka rekodi ya kumaliza mbiop hizo kwa sekunde 50.71 Jumatatu hii wakati Manunga alimaliza katika nafasi ya sita kuruka vihunzi baada ya kutumia sekunde 58.96. tayari Chama cha Riadha Kenya (AK) kimekutana na IAAF na wanariadha husika na uchunguzi umeanza juu ya hali iliyosababisha matokeo hayo.
AK wamesema kwamba hatua zaidi zitachukuliwa na Kenya.
Jumla ya wanariadha 13 wa Kenya kwa sasa wanatumikia kifungo cha kutoshiriki michezo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Mapema mwezi huu, shirikisho la kimataifa linalopambana na dawa za kuongeza nguvu zilizozuiwa lilitangaza kwamba lingefanya uchunguzi wa kina juu ya madai kwamba matumizi ya dawa hizo yalikuwa makubwa.
Comments
Loading…