Mechi ya hatua ya 16 bora baina ya Japan na Ubelgiji ilikuwa na mvuto wa kipekee na msisimko mwanzo hadi mwisho.
Ubelgiji walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na wachezaji wake nyota, hasa walio Ligi Kuu ya England (EPL), lakini kama ilivyokuwa kwa vigogo wengine wa dunia, Ubelgiji wakaanza kuelemewa.
Hadi kipindi cha pili walikuwa nyuma, baada ya kuchakazwa mabao 2-0 na Wajapani walioonekana kuwa moto sana, wakiwa wakali kwenye ushambuliaji, ngome imara na kipa aliyewakatalia sana washambuliaji wa Ubelgiji.
Naam, ni kikosi kizito chenye akina Eden Hazard, Romelu Lukaku, Kevin de Bruyne, Marouane Fellaini, Jan Vertonghen, Adnan Januzaj, Vincent Kompany, Michy Batshuayi, Thibaut Courtois, Simon Mignolet, Dedryck Boyata na Thomas Vermaelen.
Wengine ni Thomas Meunier , Toby Alderweireld, Jordan Lukaku, Christian Kabasele, Mousa Dembele, Axel Witsel, Nacer Chadli, Dries Mertens na Christian Benteke.
Wameweka historia ya kutoka nyuma kufungwa 2-0 hadi kuja kushinda ndani ya muda wa kawaida katika kipindi cha pili na kwa hakika wanastahili kuitwa kikosi cha kizazi cha dhahabu kwa tafa hilo la kaskazini magharibi mwa Ulaya.
Zikiwa zimebaki dakika 21 kwa mechi kumalizika, Ubelgiji walikuwa nyuma kwa mabao hayo mawili kwa bila, lakini walicheza kwa kujiamini na kujituma, japokuwa washabiki walishaanza kukata tamaa na wengine kulia lakini Mashetani Wekundu, kama wanavyoitwa waliliendeleza shinikizo dhidi ya Wajapani.
Kocha Roberto Martinez alikuwa na wakati mgumu, akafikiria sana kisha akafanya uamuzi wa kupumzisha wachezaji wawili na kuingiza akina Fellaini na Chadli, na ni baada ya hao kuingia, mambo yakabadilika, kwa Vertonghen kufuta bao moja, Marouane Fellaini akasawazisha na Chadli akatia bao la ushindi katika muda wa ziada – dakika ya 94 na kuwaliza Wajapani.
Ni muhimu kuwarambua Wabelgiji hawa, watawala wa kikoloni wa zamani wa Zaire, ambao Machi 2016 walishika nafasi ya kwanza kwenye viwango vya soka vya dunia kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Hata hivyo, miezi minne baada ya hapo walifurushwa kwenye Euro 2016 katika hatua ya robo fainali na Wales.
Miaka miwili kabla, waliondoshwa pia kwenye fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya robo fainali, wakipigwa na Argentina waliokuja kuwa washindi wa pili 2014 nchini Brazil, wakipigwa na Ujerumani. Wawili hao wote wameshatolewa kwenye mashindano ya mwaka huu.
Leo wamekuja na kikosi hiki, wachezaji 13 waliocheza mechi hiyo ya Jumatatu dhidi ya Japan wameweka rekodi ya kuwa kikosi cha kwanza tangu 1970 kutoka nyuma kwa mabao 2-0 hadi kushinda kwenye hatua ya mtoano kama hiyo.
Mlinzi Kompany, kipa Courtois, kiungoDe Bruyne na mshambuliaji Hazard wametwaa ubingwa wa England mara nane miongoni mwao. Sasa wanahitaji ushindi mara mbili tu ili kufika fainali ya Kombe la Dunia. Ndoto hiyo ilionekana kuwa mbali sana, baada ya mabao ya Takashi Inui na Genki Haraguchi.
Lakini safari hii kwenye robo fainali watakabiliana na ‘Samba Boys’ – Brazil na hivyo Ijumaa itakuwa mechi ngumu, pengine kwa kila timu. Martinez amepata kuzifundisha klabu za Swansea, Wigan na Everton – zote za England.
Brazil wanafundishwa na mwana wa ardhi yao, Adenor Tite (57)mwenye uzoefu mkubwa katika ngazi za klabu, ambapo hadi anawachukua Brazil mwaka juzi, alikuwa ameshafundisha klabu kama 15, nyingi za Brazil, lakini pia amekuwa Mashariki ya Kati na Ureno.
Ubelgiji hawajapata kutofungwa walau bao moja katika mechi zao 12 zilizopita kwenye hatua za mtoano, wakifungwa jumla ya mabao 28. Hata hivyo, Martinez (44) ambaye ni Mhispania, ataangalia zaidi mambo chanya, hasa ushindi mgumu na muhimu dhidi ya Japan.