Timu ya soka ya Tanzania, Twiga Stars, inatarajia kuondoka nchini kesho alfajiri kuelekea jijini Harare, Zimbabwe, kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara (COSAFA) ambayo yanatarajiwa kuanza kufanyika Jumamosi jijini humo.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 26 ambapo wachezaji ni 19 pamoja na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha mkuu, Charles Boniface anayesaidiwa na Nasra Mohammed, kutoka Zanzibar.
Wambura alisema kuwa mkuu wa msafara wa timu hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA), Lina Mhando, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.