UKIANGALIA mwenendo wa mpira wa miguu unaweza ukadhani niliyoandika ni hadithi. Si hadithi, ni ukweli na tunaweza hata kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la mataifa ya Afrika tukitaka. Kwa hiyo suala hapa ni sisi tu kutaka na si vinginevyo.
Siku moja nilimdokezea rafiki yangu mmoja kuwa nataka kugombea uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF). Alinipiga ‘stop’.
Nimekuwa kiongozi wa mpira wa wavu kwa zaidi ya miaka 20 na nilijitahidi kuepuka na kuepusha migogoro. Nilitaka kuwa kiongozi bora na si bora kiongozi.
Rafiki yangu huyu ananiambia kuwa nisifikirie hata siku moja kuwa mpira wa wavu ni sawa na wa miguu. Huko kuna watu wakorofi na chama chenyewe kiko hivyo hivyo.
Baada ya kuambiwa hivyo, nikayakumbuka maneno ya Mwina Kaduguda aliyeongozi wa (TFF) kwa muda kwamba kuwa kiongozi wa chama hicho, hasa ngazi ya juu ni sawa na kuwa mwendawazimu na kugombea uongozi ni uendawazimu.
Sasa kama nafasi za uongozi wa juu wa (TFF) zinaogopwa na jamii kama upupu kiasi hicho basi kweli ni kasheshe.
Nakumbuka Licky Abdallah, mchambuzi wa mpira wa miguu nchini amekuwa akiulizwa ni kwa nini asiwanie uongozi wa (TFF) ili aokoe jahazi. Lakini mara zote ameonesha kuogopa kwa madai mazingira hayatoi fursa kwa watu makini kuongoza. Licky ni mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa hiyo anajua anachokisema.
Lakini mpira wa miguu ni lazima uendeshwe na ili uende inavyotakiwa ni lazima uendeshwe na watu makini. Watu makini wapo, lakini wamepagawa na hofu tu kama alivyo huyu rafiki yangu na wengine.
Kipindi cha mpito ambacho Leodgar Tenga alikuwa Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti Balozi Juma Mwapachu ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA) hatukusikia kelele tunazozisikia leo kwa sababu watu hao walikuwa makini.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Said El-Maamry na wengine. Ndiyo maana baadhi yao walikuja kuwa viongozi wa BMT kwa vipindi tofauti kutokana na michango yao muhimu (TFF)
Ninapokumbuka fainali za Afrika roho inaniuma na kila wakati najiuliza hivi ni kwa nini hatuwezi kurudia historia ya mwaka 1980 ambapo Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho?
Ninaamini tunao watu wanaoweza kutupeleka fainali za Afrika na kuuboresha mchezo huu hapa nchini isipokuwa kufika huko kunataka watu wenye uwezo, makini, nia, maono, mikakati, wasio na uroho wa madaraka, waadilifu na zaidi unatakiwa mkono wa Serikali.
Kucheza fainali za Afrika mwaka 1980 kulitokana na nia ya Serikali kuthamini michezo na kuwatia moyo wanamichezo na viongozi. Michezo ilikuwa ni sera ya siasa ya ujamaa.
Hivi sasa FAT inafanya marekebisho ya Katiba yake. Hili ni jambo jema lakini marekebisho peke yake hayatoshi na hayawezi kutupeleka fainali za Afrika wala kuongeza kiwango wa mchezo.
Kitakachoweza kuirekebisha (TFF) ni viongozi wenye sifa za utendaji makini, maono, mikakati na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na Serikali kuweka mazingira bora ya maendeleo ya michezo nchini.
Tukiacha mzaha tunaweza hata kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la mataifa ya Afrika achilia mbali kushiriki kama Serikali yetu na (TFF) wana nia moja.
Afrika Kusini imewezaje kupata uenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2010?. Unafikiri walitumia mbinu gani za kupata kura za wajumbe huku wakijua kuwa washindani wengine kama Misri, Morocco, Tunisia na Libya wamejiandaa kama wao?
Bila ya juhudi za makusudi ambapo Serikali na watu mashuhuri kama Nelson Mandela na Askofu Desmond Tutu kuhusika moja kwa moja, Afrika Kusini isingeambulia chochote. Unaona hiyo?
Hiyo ndiyo mikakati, yaani kuona mbali na kutenda. Mkono wa Serikali katika jambo hili la uenyeji wa Kombe la Dunia ulikuwa mkubwa kuliko chama cha mpira kwa kuwa hilo ni jambo la kitaifa.
Hivi sasa vyombo vya habari na Serikali vinaupigia debe uwanja mpya lakini inatisha kuona Serikali hiyo hiyo inasitisha michezo ya shule za msingi na sekondari ambapo huko ndiko kwenye vipaji.
Kama juhudi za makusudi hazitafanyika kurejesha michezo hiyo basi nchi hii itakuwa haina vipaji vya mchezo wowote kwa miaka mingi ijayo. Hapa wa kulaumiwa ni Serikali tu.
Ikumbukwe kwamba utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo ya michezo nchini inaanzia shuleni. Kwa hiyo Waziri Joseph Mungai anapong’ang’ania msimamo wake wa kusitisha michezo anaipinga sera yao ya CCM.
Hivi sasa tuko nyuma kwa takribani miaka 20 katika michezo. Pale tunapofikiria kupiga hatua mbele Serikali inaivuta jezi michezo. Hiyo michezo si itaanguka? Je, hiyo siyo faulo? Sasa ni nani wa kuipigia filimbi Serikali kwa kuvunja kanuni hiyo?
Mbaya zaidi ni pamoja na kutotengwa fedha za kutosha kusimamia michezo, Serikali kupitia wizara yake kwa sasa imegeuka kuwa shabiki badala ya kuwa mtendaji. Sera ya Michezo iliyopo haitoi fursa ya mabadiliko ya lazima. Serikali imejiweka pembeni kama inavyofanya kwa mashirika ya umma. Haya ni makosa makubwa.
Ni lazima Serikali ya CCM irudi kwenye ilani yake ya uchaguzi iangalie iliwaambia nini wananchi kuhusu michezo. Si tu kujenga uwanja wa kisasa.
Kazi ya Serikali hapa ni kubwa lakini haitaki kufanya kazi zake. Haitaki kuwajibika. Wajibu wa kwanza wa Serikali katika michezo ni kuisimamia na hasa kuzisimamia timu za taifa za michezo yote.
Mikakati, sera, maono, mbinu, nia ya kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza michezo na timu za Taifa, vyote hivyo vinafanywa na Serikali. Hakuna Serikali yoyote duniani ambayo haijihusishi na masuala ya timu za michezo za taifa hasa katika kuzisadia fedha.
Chama chochote kile ni wawezeshaji tu wa mambo ya ufundi na ukuzaji vipaji kwa vijana kupitia mashuleni katika kuwashindanisha, lakini usimamizi na gharama za michezo hasa timu za taifa ni wajibu wa taifa kupitia vyama husika na taifa linaendeshwa na Serikali na ndiyo maana Serikali imeweka Wizara inayohusika na michezo.
Serikali yetu si kisiwa. Ni lazima ijifunze wenzetu wanafanya nini. Kurugenzi yetu ya michezo na BMT viko pale kwa makusudi hayo. Kwa hiyo ni lazima vyombo hivi vitumike kikamilifu.
Ni kweli Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa fedha kwa baadhi ya timu za taifa, lakini hizo fedha ni kidogo mno na wala haipendezi kuzitaja. Udhamini wa jinsi hiyo hauleti ushindi.
Serikali inafanya hivyo kujiondolea lawama tu. Lazima ipige hatua zaidi ya hapo. Ichukue hatua ya kukuza michezo kwa maana ya sera na usimamizi wa utekelezaji wake na kuigharamia.
Kwa hiyo Serikali iache kijihusisha katika ushabiki wa kulaumu viongozi wa michezo kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya michezo. Si sahihi Serikali kulumbana na viongozi wa michezo.
Wajibu wa Serikali ni kukemea viongozi wabovu siyo kubishana nao. Ni wajibu wa Serikali kumkemea kwa mantiki kiongozi wa ngazi yeyote ile na kwa nguvu zote bila ya kujali mashirikisho yao ya kimataifa kama FIFA, IAAF au FIVB kwa kuwa michezo ni sehemu pia ya utumishi wa Serikali kwa wananchi na Serikali ni sauti ya watu na si kuishia kulaumu tu.
Tendo la Serikali la kulaumu viongozi wa michezo ni ushabiki. Serikali ni mtendaji na mwajibikaji kwa wananchi. Mtu kama Muhidin Ndolanga akiharibu kazi ni Waziri anayehusika na michezo ndiye anayeulizwa maswali na wananchi kupitia Bunge.
Kwa mfano Ndolanga hawezi kuitwa bungeni kujibu maswali ya Bunge ni kwa nini Tanzania haikushiriki fainali za Afrika huko Tunisia mwaka 2004 au kwa nini alirudi madarakani. Hawajibiki huko.
TFFi nawajibika kwa Waziri anayehusika na michezo kupitia vyombo husika kama Kurugenzi ya Maendeleo ya Michezo, BMT na Msajili. TFF na vyama vingine vyote vimesajiliwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bunge.
Kiburi cha viongozi wa vyama vya michezo vya taifa kinachangiwa na hasira ya kuachwa hivi hivi tu bila msaada wowote.
Kwa hiyo Wizara ina wajibu mkubwa kuhusu maendeleo ya michezo na kama michezo inadidimia wa kuulizwa ni Serikali na si viongozi wa michezo hata kama ni wabovu kiasi gani. Sitetei viongozi wabovu.
Chombo cha kudhibiti ubovu huo ni Serikali hata kama ubovu huo unachangiwa na wapiga kura wa vyama husika. Serikali inao uwezo wa kukifuta chama chochote kama maslahi ya taifa hayalindwi.
Watu wa kuifikisha nchi hii mbali wapo. Kinachotakiwa ni kuwawekea mazingira mazuri ya kuendesha michezo ikiwa ni pamoja na Serikali kuwajibika kikamilifu katika kuikuza na kuiendeleza kwa sera na mikakati ya makusudi. Vinginevyo migogoro ya viongozi haitaisha kamwe.
Mwito wangu kwa Serikali ni lazima iwajibike katika kuinua hali ya michezo nchini ikiwa ni pamoja na kuviwezesha vyama na kusimamia matumizi kwa karibu na kuwawajibisha wabadhilifu kama TOC inavyofanya hivi sasa kwa vyama ambavyo havina nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kuvinyima ruzuku nyingine mpaka vitoe maelezo ya matumizi ya awali.
Vyombo vya fedha kama vile Benki ya Dunia na vinginevyo vinatumia mtindo huo huo wa uwajibishaji kwa mikopo yake kwa Serikali.
Naamini watu wengi wenye uwezo watajitokeza lakini hali ikiendelea kuwa kama ilivyo sasa maneno ya kichwa cha habari cha makala hii ni ndoto tupu.
Comments
Loading…