Hapana shaka kila uchwao matamanio ya kuona mpira wetu ukifika sehemu kubwa huongezeka.
Kila mtu huwa na shauku, kila moyo huwa na mhemko wa kuiona ligi yetu ikifika sehemu ambayo ni kubwa.
Ndiyo maana tukatafuta wadhamini kwenye ligi yetu na kwenye baadhi ya vilabu vyetu, hii ni kuonesha kuwa tunatamani kufika sehemu yenye ushindani mkubwa.
Ushindani ambao unaletwa kwa timu mbalimbali kutokuwa na hali ngumu ya uendeshaji wa timu kwa sababu ya mikataba ya wadhamini wanayoingia nayo.
Hata wachezaji pia huingia mikataba na klabu husika, mikataba ambayo ni moja ya kielelezo kuwa tunapitia kwenye daraja la uweledi.
Daraja ambalo lina mambo mengi sana, kuna vitu vingi unatakiwa uvifanye ili ufanikiwe kuvuka salama daraja hili la weledi.
Nidhamu ndiyo wimbo mkubwa unapokuwa unapita kwenye daraja hili. Nidhamu ya viongozi wa mpira wetu.
Viongozi ambao wataiongoza timu katika misingi ya weledi. Timu ipate wadhamini ambao watasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa timu.
Viongozi ambao watahakikisha wachezaji wao wanapata stahiki zao kwa wakati huku wakicheza na kufanya mazoezi katika mazingira ambao ni mazuri.
Mazingira ambayo yanaendana na mahitaji ya mpira kwa sasa ili kuendana na ushindani wa mpira duniani kwa sasa.
Viongozi ambao watapandikiza nidhamu kwa wachezaji wetu, wachezaji ambao watajua mpira ni kazi, kazi ambayo inahitaji kuheshimiwa na mfanyakazi mhusika ili afanikiwe.
Wachezaji ambao watakuwa chini ya wasimamizi sahihi (managers) wasimamizi ambao watawaongoza na kuwashauri kipi sahihi cha kufanya kwa ajili ya kulinda picha yake mbele ya jamii.
Yeye ni kioo, kioo ambacho kila mtu hutumia kujitazama. Kuna vingi vya kufanya ili kulinda kioo hiki kisipasuke na kikashindwa kuonesha taswira halisi ya picha husika.
Mpira ni biashara, neno hili linatajwa kiwepesi sana kwa sababu ni neno jepesi kutamkika. Watu wanalitamka kwa sababu lipo kwenye ulimi wao lakini kwa bahati mbaya likakosekana kwenye akili yao.
Wachache sana wanaoishi kwenye neno “mpira biashara” kwa sababu kwao biashara ipo mdomoni tu na siyo akilini.
Ndiyo maana hakuna mchezaji anayemwajiri msimamizi wake (manager) kwa ajili ya kumuongoza kwenye mambo mbalimbali kama ya biashara hasa hasa kupata mikataba ya matangazo ya bidhaa mbalimbali kutoka kwenye makampuni (endorsements).
Ni furaha kubwa kwa mfanyabiashara kutangaza bidhaa yake sehemu ambayo anaona itaipeleka bidhaa yake sehemu ambayo ni kubwa.
Ndipo hapo suala la nidhamu linapochukua nafasi yake, nidhamu kwa mchezaji husika. Jinsi ambavyo anailinda taswira yake kwa wanaomtazama.
Jamii inamtazamaje? Ni mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya uwanja?
Kucheza vizuri ndani ya uwanja hakutoshi peke yake kuwa mtu mwenye ushawishi nje ya uwanja. Unashiriki vipi kwenye matukio ya kijamii nje ya uwanja? Je ndani ya uwanja una nidhamu gani inayokuuza nje ya uwanja kwenye makampuni?
Ndipo hapo masikitiko yangu yanapokuwa makubwa kila nikikumbuka tukio la Kelvin Yondani.
Beki mahiri wa Yanga kwa muda mrefu, kadri muda unavyozidi kwenda ndivyo kiwango chake kinazidi kuwa kikubwa.
Hapana shaka ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Yanga na mwisho wa siku ni nahodha wa timu.
Nahodha, kiongozi, mwenye sauti ya mwisho ndani ya uwanja, kioo cha wachezaji wengine na mwisho wa siku mashabiki humtazama yeye kama kiongozi wa mwisho ndani ya uwanja.
Hapa ndipo umuhimu wa taswira yake na kitambaa anachovaa mkononi unapokuja.
Hakutakiwa kuwa na maamuzi ambayo yangehatarisha taswira yake kuwa mbovu ndani na nje ya uwanja.
Hapa ndipo umuhimu wa wasimamizi wa wachezaji unapokuja. Watu hawa hutumia muda mwingi kuwashauri wachezaji kufanya kitu chenye faida ndani na nje ya uwanja.
Kwa alichokifanya Kelvin Yondani kina faida gani nje ya uwanja? Taswira yake kibiashara itaonekanaje? Atakuwa na uwezo wa kumshawishi mfanyabiashara awe balozi wa bidhaa yake?
Ndipo hapo ninaposema tunapenda kuhubiri weledi katika sehemu isiyo sahihi, tujivue koti la Kelvin Yondani ndipo tuendelee kuhubiri neno “weledi”.