“Kwa mara ya kwanza nimemuona namba 9 halisi” haya ni maneno ya kocha wa Mbeya City, Ranadhani Nsanzurwimo baada ya mechi ya Mbeya City na Lipuli.
Shinyanga ndiyo sehemu sahihi ambayo unaweza kupata historia ndefu ya Adam Salamba. Mchezaji ambaye hatua zake zinavutia sana kuelekea kwenye njia za mafanikio.
Hakuna lifti yoyote aliyoitegemea mpaka sasa hivi kwenye njia yake ya mafanikio , kupanda kwake ngazi ndiko kumekuwa siri kubwa ya mafanikio yake mpaka sasa hivi.
Hakutaka lifti yoyote kwenye njia yake ya mafanikio, aliamini katika kupanda ngazi kwa sababu baba yake alimwambia hakuna njia ya mkato kufikia kilele cha mafanikio.
Lazima upande ngazi moja baada ya nyingine mpaka kufika pale unapopatamani, ngazi yake ya kwanza ilianzia Shinyanga, sehemu ambayo amezaliwa na kukulia. Stand United pekee ndiyo waliotumika kama ngazi ya pili kwenye hatua za Adam Salamba. Hakudharau hatua zake, hata alipotakiwa kwenda Lipuli hakupuuzia kwa sababu aliona hiyo ni ngazi moja wapo ambayo anatakiwa kuipitia kufika anapopatamani.
Hakuiona Yanga , Simba au Azam Fc wakati yupo Stand United ila aliiona hatua ya tatu ya safari yake ya mafanikio, hakuipuuzia ila aliiheshimu ipasavyo ndiyo maana alifanya vizuri na Lipuli Fc.
Alijitoa kwa uwezo wake na macho yenye tamaa yalimuona akawa lulu katika jiji la Dar es Salaam na leo hii yupo katika mitaa ya kariakoo.
Mitaa yenye taa nyingi zinazowaka muda wote, ni vigumu kutambua rangi ya usiku na rangi ya mchana ni ipi hivo unaweza ukajikuta hujui kipi sahihi cha kufanya kwa wakati sahihi.
Ndiyo maana wachezaji wengi wanapofika Kariakoo kitu kinachotakiwa kufanywa usiku wao hukifanya mchana na kitu ambacho kinatakiwa kufanywa mchana wao hukifanya usiku.
Usahihi wa maamuzi huwa ni mdogo na hii ni kwa sababu wengi huona Kariakoo ndiyo kila kitu kwao kwenye maisha yao ya soka. Maisha yao ya soka hukamilika kipindi ambacho wao huwa wamefika pale Kariakoo.
Kujishughulisha kwao huwa ni kwa kiwango kidogo sana, kila ndoto zao za kipindi cha nyuma husahaulika wanapofika Kariakoo.
Utakumbuka kipi wakati kila chombo cha habari kitaandika usajili wako kwa kukusifia na wakati mwingine utakuzwa na kufananishwa na wenzetu na kukubatiza jina la Adam Salamba “Drogba”.
Hapa ndipo utajiona huna haja ya kwenda sehemu ambayo aliwahi kufika Didier Drogba kwa sababu jina lake utakuwa unalibeba wewe, kichwa kitakujaa, umaarufu utakulevya hata mazoezi hutoyataka tena.
Hutojituma tena kwa nguvu kwa sababu maono yako yatakuwa yamepotezwa na kalamu zetu zenye njaa ya hela, kalamu ambazo zitakuandika kukusifia ili zipate hela na zitakuandika vibaya ili zipate hela pia.
Hutokumbuka tena kama ni muda sahihi kwako wewe kupata msimamizi wako (manager) mwenye maono na anayetamani kukiona kipaji chako kikifika mbali.
Msimamizi(manager) ambaye atakuwa na uwezo wa kukumbusha kipi unatakiwa kufanya na kwa wakati upi?.
Msimamizi ambaye atakuwa anahusika kuangalia na kukumbusha kuhusu mpangilio wa mazoezi yako binafsi, chakula unachotakiwa kula na muda wa kupumzika.
Msimamizi (manager) ambaye atakujenga namna ya kuongea na vyombo vya habari, msimamizi ambaye atakutahadharisha kuhusu mambo ya nje ya uwanja ambavyo yanaweza kuharibu kipaji chako na maono yako.
Msimamizi(manager) ambaye atakukumbusha kila siku kuwa Simba siyo sehemu ya kukaa muda mrefu ni sehemu ya kupita tu kuelekea kwenye kilele cha mafanikio hivo uwekezaji wa jitihada uwanjani ndiyo kitu cha msingi.
Kila mguu wako unapopokea mpira uwaze kufanya maamuzi ambayo yatakupeleka sehemu ambayo yupo Mbwana Samatta au Simon Msuva.
Kosa kubwa ni pale utakapojisahau na kuridhika na maisha rahisi ya Kariakoo. Ni wakati mzuri kwa Adam Salamba kuongeza njaa yake ya mafanikio.
Kuwepo kwake Simba kusimfurahishe sana na kusahau kuwa Simba ni kama ngazi ya kupandia kwenda juu, uwe mwanzo wa yeye kujituma kwa juhudi kubwa huku nidhamu ikiwa nguzo ya mafanikio makubwa.
Nidhamu ya kuheshimu ratiba yake binafsi ya mazoezi, nidhamu ya kuheshimu ratiba ya timu, nidhamu ya kuheshimu na kuelewana na wachezaji wenzake, nidhamu ya kusikiliza maelekezo ya benchi la ufundi na nidhamu ya kufanya maamuzi bora akiwa uwanjani.
Huu ni wakati wake wa kuwinda swala kwa nguvu zote, aruhusu njaa ya Simba imvae ili awinde kwa hasira , asiruhusu upole wa Swala kwa sababu mwisho wa siku ataliwa na Simba.