in , , ,

Tuliyojifunza kwenye mechi za kirafiki kuelekea Euro


ENGLAND HAWAKO IMARA KWENYE ULINZI

Kiwango kinachooneshwa na Jamie Vardy na wenzie kwenye mashambulizi ya England ni cha kuridhisha. Timu imeonesha uwezo mkubwa wa kutengeneza na kumalizia nafasi kwenye michezo dhidi ya Ujerumani na dhidi ya Uholanzi.

Kufunga mabao matatu ndani ya ardhi ya Ujerumani kwenye dimba la Olympiastadion dhidi ya Ujerumani ni jambo linalotosha kumwaminisha mwalimu Roy Hodgson kuwa kimashambulizi kikosi kipo tayari kwa ajili ya Euro.

Aina ya mabao yaliyofungwa na Harry Kane na Jamie Vardy kwenye mchezo huo ambao England waliibuka na ushindi wa 3-2 juzi Jumamosi ni mabao yaliyofungwa kwa uwezo mkubwa.

Lakini kwenye upande wa ulinzi Hodgson bado ana mtihani. Anatakiwa kukitazama vizuri kikosi chake na pia wachezaji wanaopewa nafasi wanatakiwa kujituma zaidi kuhakikisha timu inasimama imara kwenye ulinzi.

Kuruhusu mabao mawili dhidi ya Ujerumani ni jambo lililotarajiwa. Lakini aina ya mabao waliyoruhusu yananipa mashaka juu ya umakini ama na uwezo wa walinzi wao pamoja na mlinda mlango Jack Butland.

Licha ya umahiri wa Toni Kroos kwenye mashuti ya mbali lakini shuti lake kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya England lisingeweza kuzaa bao kama Butland angekuwa makini na kwenye ubora wake tuliouzoea.

Ingawa inasemekana golikipa huyo wa Stoke City alikuwa ameshaumia dakika chache kabla ya shuti la Kroos lakini hilo halitoshi kunishawishi kuwa maumivu aliyokuwa nayo yalikuwa chanzo cha bao lile. Ni kukosa umakini.

Pia ingawa Mario Gomez anafahamika wazi kwenye uwezo wake wa mipira ya hewani lakini walinzi wa England hawakuwa naye makini na ndio maana aliweza kufunga bao lake kirahisi bila bughudha.

Nathaniel Clyne, Garry Cahill, Chris Smalling na Eric Dier walikuwa kwenye eneo la hatari na walishajua kuwa Khedira angemimina krosi wakati kwa upande wa Ujerumani ni Mario Gomez na Thomas Muller pekee waliokuwa kwenye eneo la hatari.

Ilinishangaza kuona jukumu la kumchunga Mario Gomez mwenye urefu wa futi 6 na inchi 2 na umahiri wa ajabu wa mipira ya hewani anaachiwa Nathaniel Clyne wa urefu wa futi 5 na inchi 9 na uwezo finyu kabisa wa mipira ya hewani.

Garry Cahill mwenye urefu wa futi 6 na inchi 4 na uwezo wa kutosha wa kupigania mipira ya juu alikuwa na nafasi ya kutazama nyuma na kumsogelea Gomez kisha aruke naye baada ya krosi kumiminwa.

Lakini hakufanya hivyo na ndio maana Mario Gomez ambaye sasa anakipiga katika klabu ya Besiktas ya Uturuki akapiga kichwa rahisi kabisa ingawa Clyne alitumia uwezo wake wote kumzuia.

Pia kwenye mchezo dhidi ya Uholanzi hapo jana Jumanne England walionyesha kiwango cha kutosha kwenye mashambulizi. Namna Adam Lallana, Kyle Walker na Jamie Vardy waliyoshirikiana kuipatia England bao la kuongoza ni ushahidi wa hilo.

Hata hivyo licha ya mabao ya Uholanzi kuonekana kutokana na maamuzi ya ovyo ya mwamuzi kutoka Hispania Antonio Mateu lakini bado England walinipa mashaka kwenye suala la ulinzi katika mchezo huo.

Timu inapotawala mchezo kwa zaidi ya asilimia 60 na kisha wapinzani wakapiga mashuti mengi zaidi yaliyolenga lango kuliko timu hiyo, hiyo ni ishara ya kuwa timu hiyo haikufanya vizuri kwenye upande wa ulinzi kwenye mchezo husika.

Hicho ndicho kilichowatokea England kwenye mchezo wa jana Jumanne waliofungwa 2-1 dhidi ya Uholanzi. Hodgson akitazame kikosi chake. Bado hakiko imara kwenye ulinzi kwa ajili ya Euro.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Chad yajitoa AFCON 2017

Tanzania Sports

GARY NEVILLE APIGWA CHINI VALENCIA