Na Ally Saleh.
Makala hii inajikita katika suala la riadha kufuatia kurudishwa michezo katika maskuli ya Tanzania hivi karibuni hatua ambayo imefurahiwa na wengi nchini.
Ni hatua iliyopigiwa kelele muda mrefu baada ya Waziri aliyepita wa Elimu, Joseph Mungai kupiga marufuku michezo mashuleni akisema ni upotezaji wa wakati, lakini Waziri wa sasa wa Elimu, Margareth Sitta kuubadilisha uamuzi huo.
Sitta, amerudisha utamaduni uliokuwapo kabla na ambao ulikuwa umejengeka kikweli kweli kwa kuwa na michezo mashuleni, na watu wengi wenye umri mkubwa ni mashahidi wa michezo ya mashule ilivyotoa wachezaji nyota.
Leo, kwa masikitiko makubwa naweza kusema taifa hili halina shujaa, nguli au nyota yoyote yule. Akitokezea nyota basi huwa ni kwa muda mfupi sana , na mara mwanga wake huzimika.
Na nyota, nguli au shujaa huyo, anazimika mara moja kwa sababu hakufikia ubingwa katika mchezo wake kwa kuwa alijengwa kimsingi, isipokuwa hilo limetokea katika juhudi zake za kutafuta ajira, na ajira akiipata, michezo inakuwa imekwisha kwake.
Jitihada za kuendeleza michezo nchini zitafanikiwa tu, endapo michezo kama hii itapewa umuhimu katika maeneo ya Mijini na Vijijini kama tuonavyo hapa Kiluvya kijijini, chini ya ulezi wa Mhe Rashid Mfaume Kawawa.
Ni kweli michezo imerudishwa mashuleni, lakini kwa fikra zangu mipango mingi inahitajika ikiwa ni pamoja na kujenga mfumo wa kupata waalimu, vifaa vya msingi, viwanja na kadhalika.
Lakini pia wakati umefika wa kubadilisha mtizamo kidogo na kuweka juhudi zetu katika mchezo wa riadha ambao nao si haba umetoa wakimbiaji wengi ambao wameipatia sifa nchi hii ya Tanzania.
Ila ndani ya riadha yenyewe pia tuanze kubadilisha muelekeo pia kwa kuanza matayarisho ya kujenga taifa la wanariadha ( nation of athletes) na sio taifa la wakimbiaji (nation of runners), ambao ndio ambao tumekuwa nao siku zote.
Mtu aweza kujiuliza hapa, kwani kuna tofauti kati ya wakimbiaji na wanariadha? Naam, ipo tofauti kubwa sana na tunachofanya sisi Tanzania ni kujenga taifa la wakimbiaji na tukiona uzito au sijui aibu kujenga taifa la wanariadha.
Kujenga taifa la wakimbaji ni kule kulenga kuwa na wanariadha ambao kazi yao ni kwenda mbio za masafa ya kati yaani mita 800, 1500, 5,000, 10,000 hadi Maradhon na kazi huwa ndio imekwisha.
Na kwa mtindo huo ambao umeendelezwa kwa muda mrefu basi timu zote za Tanzania zinazokwenda nje kwa mashindano yoyote yale, huambiwa ni za wanariadha lakini kwa kweli ni za wakimbiaji.
Tanzania kabisa haijatilia mkazo kwa michezo ya mbio fupi kama mita 100, 200,400 na viunzi vyake seuze michezo ya uwanjani kama tufe, kisahani, mkuki, kuruka chini, kuruka juu na kadhalika.
Kama kuna safari na iwapo kunahitajika watu wa kuwapunguza basi shoka la kwanza huwaangukia watu wa mbio fupi na michezo ya uwanjani. Hiyo imeshatokea si mara moja, mbili wala tatu.
Inafika wakati mchezaji wa michezo yam bio fupi na ile ya uwanjani, hawezi kuwa na juhudi katika mazoezi kwa sababu anajua hakika kuwa panga litamuangukia yeye hata awe amefikisha kiwango kinachohitajika.
Tumejenga imani kuwa Tanzania inaweza kufanya vyema tu katika kundi la wakimbiaji yaani wa mbio za masafa ya kati hadi Marathon, lakini kweli Tanzania imefanya uzuri muda wote…au imedondoa tu…hapa Bayi, pale Nyambui, pale Shahanga, pale Bura..na kadhalika na kadhalika.
Hii isijenge hisia kuwa hatukuwahi kuwa na mashujaa wetu katika wakimbiaji wa mbio fupi na michezo ya viwanjani…wapi akina Kyomo, Chihota, Amira, Rahima, Safia Maneno na kadhalika na ambao wameiwakilisha nchi hii vyema Olimpiki na Madola.
Hivi katika sekta hii ya wakimbiaji, ambayo tunajiona tumefanya vyema na kujivimbisha kichwa tunawafika Waethiopia, Wakenya, Wamoroco? Tunafanana nao vipi wakati wao mchirizi wao wa wakimbiaji haujawahi kukauka kabisa… kama maji ya Mto Nile, ilhali sisi tuna mfano wa Ziwa Victoria, lakini hatufanani nao?
Hivi taifa hili halina vipaji au watu wenye uwezo katika michezo hiyo ya mbio fupi na michezo ya uwanjani, ambayo hio ndio riadha kusema kweli? Tutajidanganya mpaka lini kuwa nchi hii ni ya wakimbiaji na wanariadha hawana nafasi?
Wito wangu kwa Serikali, Wizara ya Elimu na Wizara ya Michezo kujipanga vizuri wakati michezo ikirudishwa Serikalini kuwa riadha ipewe nafasi kama maana nzima ya riadha ilivyo.
Uamuzi wa kuweka vituo, yaani shule maalum kuwa ndio vitovu vya michezo ni mzuri lakini pia uambatane na nia ya kweli ya kuleta mabadiliko kwa kuwa na kurugenzi kamili ya kusimamia michezo ambayo sio tu ipatiwe fedha na wataalamu wa kutosha lakini pia ijenge mlahaka mzuri na makampuni ya ndani.
Mimi naamini ikiwa nchi hii itaamua kweli kweli kujenga taifa la wanariadha, basi makampuni makubwa ya michezo nayo yatajitokeza kwa sababu yatajua kuwa fursa ya kuvuna katika taifa linalotoka usingizini ni kubwa.
Na kwa kweli Tanzania imelala kiriadha…wakati wa kuamka umefika…na tuachane na sera za wakimbiaji…maendeleo yako katika sera za kujenga wanariadha….Adidas, Nike, Mitre, Misuka, Admiral zitashuka wenyewe zikijua kuwa Tanzania sasa imeamua kujenga wigo mpana na maana hali ya riadha.
Comments
Loading…