KIBARUA cha kocha mpya Thomas Tuchel kimeanza rasmi England. Hamasa ya kocha huyo kwa wachezaji wake imekuwa kubwa na matumaini ya mashabiki wa England kusonga mbele baada ya kushindwa kutwaa mataji mawili chini ya ukocha wa Gareth Southagte. Kwa kipindi cha miaka 9 Gareth Southgate amekuwa kocha mwenye rekodi nyingi na mafanikio kwa kiasi fulani. Mabosi wa chama cha mpira wa miguu England, FA wanataka kocha mwenye uwezo wa kubeba makombe ikiwemo Kombe la Dunia, Kombe la Mataifa ya Ulaya na Nations League. TANZANIASPORTS inachambua masuala muhimu ambayo kocha huyo anatakiwa kuyazingatia kwa kulinganisha na falsafa yake ya soka. Katika uchambuzi huu swali moja muhimu linaloulizwa, je Thomas Tuchel atabadilishwa kiufundi au ataibadilisha England icheze atakavyo? Katika kupata jibu la swali hili ni muhimu kuangalia aina ya mchezo anaotaka kucheza.
Soka la Kiingereza
Mojawapo ya ajenda aliyowasiliha Thomas Tuchel ni kuhakikisha anacheza soka la kiingereza na lenye utambulisho rasmi. Tuchel anatukumbusha soka la kiingereza ambalo lilikuwa likichezwa na vilabu kama vile Crystal Palace, Newcastle United au Liverpool ya Kenn Dalglish. Ukiangalia aina ya ucheza wa vilabu hivyo ni ule wa nguvu za mwili, kasi na ufundi kidogo. Ni timu ambazo zilikuwa zinacheza soka la kiingereza lililojaa mabavu.
Kwa kudhihirisha hilo kocha Thomas Tuchel amemwita beki wa kati wa Newcastle United, Dan Burn. Huyu ni beki ambaye anacheza soka la kiingereza haswa. Ni lile soka la shoka, nguvu, utemi, vurugu nyingi pale nyuma na zaidi si mzuri sana kwenye kukokota mpira wala kuanzisha mashambulizi. Lakini ni beki ambaye anakupa matokeo mazuri kwenye mpira ya juu, kuwadhibiti washambuliaji kimabavu.
Soka lake linaweza kuturudisha enzi za Sol Campbell ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Sven Goran Ericksson. Kama umewahi kuiona Liverpool ya Kenny Dalglish ilivyokuwa ikicheza ndivyo ambavyo Thomas Tuchel anataka kifanyike kwa England.
Bahati mbaya ni kwamba kizazi cha sasa cha England kina wachezaji wachache wanaoweza kucheza soka la Kiingereza. Kwa sasa wana vipaji vingi ambavyo vinaweza kumtetemesha yeyote. Gareth Southgate alibainisha hili kwa vitendo vyake kwenye kikosi alichokuwa akikiita. Wachezaji waliokuwa chini ya Southgate ni mahiri, viungo visheti, vipaji maridhawa, lakini ghafla kubadilishiwa mtindo wa kucheza huku aina ya wachezaji wanaotakiwa kwa mtindo huo wakiwa wachache ni kibarua kigumu cha Tuchel kufuata nyayo za Southgate.
Katika England ya sasa wenye uwezo wa kucheza soka la Kiingereza ni Dan Burn, Ollie Watkins, Kalvin Philips, Harry Kane, Kieran Trippier, Kyle Walker kwa kutaja wachache. Kizazi cha mabavu kimepungua kwa kiasi kikubwa.
Kombe la Dunia na Euro
Kama mafanikio basi Gareth Southgate ameweka viwnago kwa makocha wanaokuja kufundisha England. Waingereza kwa sasa hawataki kusikia matumaini, bali uwezo wao w akunyakua taji la kubwa kama Kombe la Dunia. Mara ya mwisho walichukua taji hilo mwaka 1966, hivyo wana hasira za kulikosa miaka ya karibuni huku wakiwa na wachezaji wazuri na kocha mwenye uwezo wa kuwaongoza. Labda tuseme Southgate alikosa bahati tu, lakini ni kocha mzuri mno. Waingereza wanajua wamekosa makombe katika dakika za majeruhi kama vile Euro, ndiyo maana sasa wanahitaji kocha ambaye anawahakikishia kutwaa taji.
Thomas Tuchel anakabiliwa na kibarua kigumu cha kufuata nyayo za mtangulizi wake ambaye ameweka viwnago vya mafanikio katika timu ya taifa. Katika mazingira ya sasa England wanaweza kumtimua Thomas Tuchel kama hawatakuwa na uhakika wa kunyakua taji la Dunia ua Euro.
Ingawaje Tuchel anawajua vizuri wachezaji wa kiingereza, lakini kuwachezesha kile anachotaka kukifanya inategemeana na aina ya wachezaji wanaozalishwa. Kwa sasa ni dhahiri mabosi wa FA wamechoka kuishi kwa kauli ya “almanusura”, bali wanalitaka kombe. England wanaona inawezekana na kombe hilo linaweza kuwa la kwao bila wasiwasi. Chini ya Southgate walifika nusu fainali Kombe la dunia na fainali kwenye Euro.
Ni mafanikio ya juu sana kwa kocha wa England akiwa mzawa kwahiyo ni wakati wa Tuchel kudhihirisha kuwa anaweza kuvuka kiwango hicho na kuwapa taji watoto wa Malkia. Wana kila sababu ya kutaka ubingwa wa dunia mwaka 2026. Wana kila sababu ya kutaka ubingwa wa Euro mwaka 2028. Na mtu ambaye anaweza kuwapatia taji hilo Thomas Tuchel ameanza safari ya kuipika nchi hiyo. Swali linaloulizwa na wadau wa mpira hapa England, je ataweza angalau kufuata nyayo za Southagate? Je ataweza kunyanyua makwapa ya wachezaji wakiwa na tabasamu na kuvalishwa medali ya ubingwa? Haya ndiyo yanasubiriwa kujibiwa kwenye kikosi chake kilichosheheni vipaji. Ni yeye tu na matumizi yake.
Comments
Loading…