Zimebaki siku chache kufika Aprili 20 ambapo miamba ya soka nchini Simba wataingia dimbani kupambana na washindani wao Stellenbosch Fc ya Afrika kusini katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho. Baada ya mchezo wa kwanza Aprili 20, marudiano yatakuwa Aprili 27. Kwa hiyo Simba na Stellenbosch fc zinakabiliwa na kibarua kigumu katika michezo yote miwili. TANZANIASPORTS inakuletea tofauti za msingi za timu hizi ambazo zinawinda taji la Afrika. Katika tathmini yake imegundua tofauti kubwa nyingi ambazo zinaweza kutumika kama nyenzo ya kuibuka ushindi kwa pande zote.
Simba wazoefu kuliko Stellenbosch
Kama unazungumzia suala la uzoefu, klabu ya Simba imewazidi wapinzani wao kwa kiasi kikubwa. Simba wameshiriki mashindano ya CAF kwa miaka mingi tangu miaka 1970 ambako walikuwa wakivitetemesha vilabu vya Afrika kaskazini hasa Misri. Katika karne ya 20 Simba inaweza kuwa klabu ya kwanza kutoka Tanzania yenye mafanikio makubw akwenye ngazi ya soka la Kimataifa.
Katika mafanikio hayo Simba wamefanikiwa kutinga robo fainali 6 katika mashindano ya CAF. Katika rekodi hiyo Stellenbosch hawawezi hata kuruhusiwa kufunga kamba za viatu vya wachezaji wa Simba kwa sababu wao ni wageni kwenye mashindano hayo na ushindi wao dhidin ya Zamalek ni historia kwao.
Simba wana faida ya uzoefu mara mbili; kwanza kwa kuanzia mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wamekutana na klabu za Afrika kusini na baadhi yao zilitetemeshwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa na kusababisha makocha wa wapinzani wao kufukuzwa. Mafano Kaizer Chiefs ilinusurika kutupwa nje ya mashindano baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0, bahati pekee iliyowabeba ni ushindi wao kwenye mchezo wa kwanza ambao walishinda mabao 4-0. Matokeo hayo yalisababisha uongozi wa Kaizer Chief kumfukuza kocha wao. Kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho, Simba wana uzoefu mkubwa barani Afrika kuwazidi Stellenbosch fc.
Stellenbosch fc kama Marumo Gallants
Yanga walitinga fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitupa nje ya mashindano klabu ya Marumo Gallants ya Afrika kusini. Katika suala la uwezo na uzoefu Yanga walikuwa mbali mno kwa maana ya walikuwa hadhi ya juu kuliko Marumo Gallants.
Katika Ligi ya Afrika kusini, Marumo Gallants walikuwa wanahaha kuepuka kushuka daraja, lakini kwenye mashindano ya CAF walikuwa moto wa kuotea mbali. Nini maana yake hili? Simba wanaweza kuongeza rekodi hii kwa kufuata nyayo za Yanga. Simba wanaingia kwenye nusu fainali wakiwa miamba ya kutisha, ni kama dude ambalo linatisha mno kama wingu jeusi huku ngurumo za radhi na mvua kali zikinyesha.
Simba wanayo kila sababu ya kuwa na mabavu si kimbinu pekee hata historia inawabeba kuwa wao ni miamba ya Afrika. Timu ya mwisho kutoka Afrika kusini kupambana na Simba ni Orlando Pirates ambayo iliwatupa wanamsimbazi hao kwa hatua ya matuta. Hata hivyo kama unazungumzia hatari ya Stellenbosch baada ya kuitoa Zamalek ambaye ni bingwa mtetezi basi unatakiwa kurudi nyuma hadi mwaka 2003 ambapo Simba waliitupa nje ya michuano ya klabu bingwa Zamalek kwa hatua ya matuta 3-2. Hii ina maana Stellenbosch wanapaswa kuiangalia historia hii kuwa wanakwenda kupambana na dude la kutisha.
Thamani ya vikosi
Kama unazungumzia suala la thamani ya vikosi vya Simba na Stellenbosch basi huenda ikawa habari nzuri kwa wapinzani wa wanamsimbazi. Mfano, Stellenbosch kikosi chao kina thamani ya shilingi bilioni 33, wakati Simba thamani yao ni bilioni 64.4. Simba wameitupa nje Al Masry yenye kikosi cheny thamani ya shilingi bilioni 28, ikiwa na maana sasa wakali wa msimbazi wanaendelea kupambana na timu zenye nguvu ya kiuchumi.
Hata hivyo katika kipindi chote cha mapambano Simba imekuwa ikionesha cheche zake uwanjani hivyo thamani ya vikosi inaweza kutokuwa na mchango wowote. Licha ya wachezaji wenye thamani kuwa na vipaji vikubwa lakini bado haiondoi ukweli kwamba kihistoria Simba ni matawi ya juu kuliko Stellenbosch fc.
Mgeni mchokozi
Stellenbosch ilianzishwa mwaka 2016 katika mji wa Stellenbosch, na sasa imetimzia miaka 9 tangu kuanzishwa. Taji pekee ambalo wamechukua ni Carling Cup mwaka 2023. Simba wana historia ndefu kwani wana miaka mingi wakiwa wametimzia nusu karne na ushee. Kwahiyo Stellenbosch ni timu ngeni ambayo imekuja kuwachokoza vigogo wa soka Simba.
Wachezaji wa kigeni
Kila timu ina mipango yake. Stellenbosch kwa sasa inaelekea kuingia kwenye mchezo wao dhidi ya Simba wakiwa na wachezaji watano wa kigeni. Wachezaji hao wanatoka Kenya (Brian Onyango), Nigeria (Kazie Godwill, Ibrahim Jabaar), na Ivoru Coast (Olivier Toure). Kwa upande wao Simba wanamiliki wachezaji 12 wa kigeni ambao wameing’arisha timu hiyo na mchango wao umewafikisha katika hatua ya nusu fainali. Safu ya ushambuliaji ya Simba inaongozwa na wageni Stephen Mukwala na Lionel Ateba, huku safu ya ulinzi ikiongozwa na Mousa Camara na wengineo.
Al Masry na Zamalek
Simba wameitoa Al Masry ya Misri, wakati Stellenbosch wameitoa Zamalake ya Misri. Timu zote mbili zimefanya kazi nzuri kuwatupa nje wawakilishi wa Misri. Lakini Simba wamefanya kazi ya ziada na kwa nguvu zaidi kutoka kufungwa mabao 2-0 hadi kusawazisha mabao hayo kisha kuibuka kwa ushindi wa penati 4-1. Simba walidhihirisha kuwa si kwenye kupachika mabao kwenye dakika 90 pekee bali hata kwenye hatua ya kupigiana penati ni wazuri pia.
Stellenbosch wenyewe waliibuka washindi wa 1-0. Tukizungumzia viwango vya vilabu vya Misri, ni dhahiri timu mbili tu ndizo zimeonesha viwango vizuri kwenye mashindano ya CAF ambazo ni Al Ahly na Pyramids. Al Ahly wametinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, sawa na Pymirads. Kwa kuangalia viwango Zamalek wamekuwa bingwa mtetezi mwenye kiwango duni zaidi msimu huu. Al Masry nao wamekuwa wakicheza mpira wa kujihami zaidi kama mpango wao kwanza wa kuibuka na ushindi.
Ufundi wa Stellenbosch
Kama unazungumzia ubora Stellenbosch wameachwa mbali sana na Simba. Stellenbosch wanacheza soka la kasi pale wanaposhambulia kwa kushtukiza na wanatumia nafasi chache wanazopata kuibuka na ushindi. Sehemu kubw aya ufundi wao ni kujihami na wanategemea zaidi kasi ya vijana wao wenye wastani wa umri wa miaka 25. Lakini kama ni mbinu Simba ya Fadlu Davis ipo mbali na ina uwezo wa kupambana na mpinzani yeyote anayekuja mbele yao.
Simba wanacheza nguvu moja dhidi ya timu kubwa au ndogo. Hakuna mechi ambayo Simba kwenye mashindano ya CAF kwa kulegeza nguvu lakini mechi zote wamekuwa na ari ileile dhidi ya yeyote. Hapa
Comments
Loading…