Yanga inayotetea taji lake ilipigwa 2-0 na Atletico ya Burundi na Simba ililala 2-0 kwa URA ya Uganda.
Timu nyingine za Azam na Mafunzo zilifungana 1-1 katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Chamazi.
Sasa matokeo hayo yameziweka timu hizo katika njia panda kwani sasa zinatakiwa kushinda mechi zilizosalia ili kusonga mbele.
Hata hivyo, haitashangaza kwa utamaduni wa wadau wa soka wa Tanzania kwa kupenda mafanikio ya haraka haraka basi wataanza kunoa visu ili kuwatoa makocha hawa.
Sisi tunapenda kuwaambia acheni hayo, bali wapeni muda wachezaji na makocha warekebishe mambo kwenye mechi zilizosalia.
Watanzania ni watu wa kupenda mafanikio ya haraka tofauti na jirani zetu wenye uvumilivu angalau linapokuja suala la kujenga timu.
Yanga kwa mfano ina kocha mpya, ambaye hana muda mrefu lakini sasa kuna watu wamesikikika wakimlaumu.
Hivi Mbelgiji Tom Saintfiet ana dawa ya gani ya miujiza ya kuifanya Yanga icheze soka la hali ya juu baada ya wiki moja.
Watu wanasahau kuwa Yanga imepangua kikosi chake kwa mfano katika safu yake ya ushambuliaji na ina nyuso mpya baada ya kuondoka kwa Davies Mwape na Kenneth Asamoah.
Saintfiet ni mgeni na anakutana na wachezaji wapya sasa lazima anahitaji muda mrefu wa kuandaa timu.
Matatizo kama hayo yamemkuta kocha wa Simba, Milovan Cirkovic kwani naye anatengeneza kikosi chake baada ya kuondokewa na mfungaji mahiri Emmanuel Okwi na beki wa kati, Kelvin Yondani.
Simba imesajili nyota kadhaa wa kigeni na wa humu nchini, ambao wanahitaji kuzoeana ili kucheza kitimu.
Azam huwezi kuilaumu kwani imeanzishwa mwaka 2004 tu, sasa inashiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kimataifa pamoja na ukweli kuwa wameshikwa na Mafunzo, ambayo ni timu ya kawaida.
Kitu kikubwa ambacho Watanzania wanapaswa kubadilika kwa sasa ni kuachana na kuandaa timu kwa zimamoto au kuota mafanikio ya haraka.
Utashangaa timu za Yanga na Simba zinasajili idadi kubwa ya wachezaji na kubadili makocha kama nguo na bado zinaota mafanikio.
Hazitaki kujenga mifumo ya kujenga wachezaji yosso wala suala kwao la kumwachia kocha kufanya kazi kwa muda mrefu kwao ni mwiko.
Licha ya ukweli kuwa klabu za Simba na Yanga ni kubwa lakini zinaendeshwa kama timu za mchangani.
Mathalani Simba ilimtimua kocha wake, Patrick Phiri mwaka jana licha ya ukweli kuwa aliisaidia kumaliza Ligi Kuu Bara msimu wa 2009/10 bila ya kupoteza mechi.
Yanga ndio timu pekee ya Tanzania Bara iliyowahi kumaliza ligi bila ya kufungwa nayo ilitokea mwaka 1983.
Ukosefu wa uvumilivu nao uko kwa Yanga kwani ilimtimua pia kocha wake Sam Timbe mwishoni mwa mwaka jana licha ya kuisaidia kutwaa Kombe la Kagame.
Unaweza kupata picha nzuri ya ubabaishaji uliokithiri katika uendeshaji wetu wa soka katika ngazi ya klabu.
Ushauri wetu wa bure kwa wadau wa soka kuwa sasa wasianze kujenga mawazo kuwa makocha hawa ni bomu badala yake sasa wabadilike na kuwapa fursa kusuka timu nzuri na sio kwa manufaa ya Kagame tu bali kwa muda mrefu ujao.
Comments
Loading…