Mshambuliaji mahiri wa timu ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 20, Thomas Ulimwengu, anatarajia kuondoka nchini mapema wiki ijayo kuelekea Sweden kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Dalkurd.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Florian Kaijage, alisema kuwa maandalizi ya safari ya mshambuliaji huyo yako katika hatua za mwisho.
Kaijage alisema kuwa mbali na klabu hiyo, pia timu nyingine mbalimbali za nje ya nchi zilivutiwa na kiwango cha mchezaji huyo na kuandika barua za kumhitaji ili akajaribiwe.
Hata hivyo, Kaijage alikataa kuzungumzia taarifa zinazomuhusu mchezaji huo kwamba tayari amesaini mkataba wa kuichezea Yanga katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kitita cha Sh. milioni 25.
Kaijage alisema kuwa shirikisho hilo lilipokea maombi kutoka katika klabu tatu za Simba, Yanga na Azam zote za jijini Dar es Salaam lakini hazikupewa jibu lolote.
Aliongeza kuwa klabu hizo zilielezwa pia kutofanya mazungumzo ya aina yoyote na mchezaji huyo kwa sababu ni mmoja wa nyota ambao wana mikataba na Kituo cha Michezo cha Tanzania Soccer Academ (TSA) kinachomilikiwa kwa pamoja kati ya TFF na kampuni ya Kiliwood Investment.
Katika msimu uliopita, Ulimwengu ambaye kipaji chake kilionekana akiwa na timu ya U-17 ya mkoa wa Dodoma mwaka juzi, alicheza kwa mkopo katika klabu ya Moro United.
Mshambuliaji huyo aliifungia timu yake ya vijana mabao mengi katika mashindano ya vijana ya Copa Coca Cola nchini Afrika Kusini, mara moja akifunga mabao matano katika ushindi wa 15-0 dhidi ya Malawi na kuwavutia mawakala mbalimbali.
TFF ilitangaza kwamba klabu haziruhusiwi kuingia mkataba na mchezaji yoyote wa TSA, jambo ambalo linaloonyesha kuwa huenda Yanga ikamkosa nyota huyo.
Comments
Loading…