MKURUGENZI wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Leornad Thadeo amesema mwenendo na hali ya michezo nchini bado hauridhishi kwa sasa kutokana na nchi kushindwa kufanya vizuri katika michezo kimataifa.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alikimwagia sifa chama cha netiboli nchini kwamba ni mfano kuigwa kwa kuwa kimefanikiwa kutumia jitihada zake kuinua mchezo huo nchini.
Akihojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na kituo cha luninga ya serikali cha TBC, Thadeo alikiri kwamba mwamko wa michezo nchini bado uko chini kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Mwenendo wa michezo nchini siyo mzuri sana, kwani bado hatujafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, mwenendo sio mzuri kwa sasa, “alisema Thadeo.
Thadeo alisema baadhi ya vyama vya michezo nchini vimekuwa vikiongozwa bila kufuata katiba ya vyama huku akidai vingine vimejikita kwenye migogoro badala ya kukazania maendeleo ya michezo hali inayosababisha michezo nchini kushindwa kufanya vizuri kimataifa.
Alisema serikali imeandaa mpango mkakati wa michezo nchini ambao utakamilika mwezi ujao ambao utalenga kuleta maendeleo ya michezo nchini sanjari na kuonyesha dira kwa vyama mbalimbali vya michezo nchini.