Shirkisho la soka, TFF, limewashauri viongozi wa klabu za ligi kuu ya Bara kuacha kuwa wazungumzaji wakuu katika vyombo vya habari na badala yake kutoa nafasi kwa wasemaji waliowaajiri.
Katika siku za karibuni, mwenyekiti wa Simba Isamil Aden Rage amekuwa msemaji mkuu wa masuala ya Simba kiasi cha kusababisha aliyekuwa na jukumu hilo kikatiba kuacha kazi.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Msemaji wa TFF Boniface Wambura alisema kuwa kanuni za TFF zinazitaka klabu zote za ligi kuu ya Bara kuajiri maafisa habari wa klabu ambapo moja ya kazi zao ni kuwa wasemaji wakuu wa klabu hizo.
Wambura alisema kuwa kwa kuwa viongozi ndio wenye taarifa zinazohusu klabu ni vizuri wakashirikiana na wasemaji ili kutoingilia mipaka ya utandaji wa kazi.
“TFF haitaki kuingilia utendaji wa klabu, lakini kwa jambo la wasemaji ni vizuri kama viongozi wakawapa nafasi wasemeji kufanya kazi zao vizuri kama ilivyokusudiwa katika kuendeleza soka letu,” alisema Wambura.
“Viongozi ni vizuri kama watatoa nafasi kwa wasemaji wao kufanya kazi zao bila kuingiliwa,” alisema Wambura. Ukiacha Simba, klabu nyingine za ligi kuu, ikiwemo Yanga iliyomuajiri Louis Sendeu, zimekuwa zikitoa nafasi kubwa kwa wasemaji wao kuvipasha habari vyombo mbalimbali vya taaluma hiyo.
Akizungumzia hatua ambazo shirikisho lake linaweza kuichukulia Simba baada ya aliyekuwa msemaji wake Cliford Ndimbo kuacha kazi hiyo kwa madai ya kuingiliwa na uongozi, Wambura alisema TFF haikuwa na taarifa yoyote na haina uthibitisho wa madai ya Ndimbo.
Wambura alisema kuwa TFF haijawahii kupata malalamiko kutoka kwa Ndimbo au maafisa habari wa klabu nyingine wakidai kuingiliwa katika majukumu yao na viongozi wao.
Hivi karibuni Ndimbo ambaye alikuwa msemaji wa Simba tangu TFF ilipozitaka klabu kuwa na wasemaji, aliacha kazi hiyo kwa madai kuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo walikuwa hawathamini taaluma yake na kuchoshwa kuingiliwa majukumu yake.
Hivi hicho kichwa cha habari na habari yenyewe vinaendana?