Shirikisho la Soka nchini (TFF) limesema kuwa linatarajia kuialika timu ya taifa ya Uganda, The Cranes katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa, Taifa Stars uliopangwa kuchezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
Hatua ya TFF, ya kuialika The Cranes, imekuja kufuatia timu ya taifa ya Malawi ambayo awali ilidhibitisha kuja nchini kumenyana na Taifa Stars kuchomoa kwa madai ya kuwakosa wachezaji wake muhimu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema kuwa baada ya timu ya taifa ya Malawi kukataa kuja nchini kupambana na Taifa Stars sasa hivi wanafikiria kuialika timu yeyote kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na hasa timu ya taifa ya Uganda.
Alisema lengo ni Taifa Stars kupata mchezo wa kirafiki wa kimataifa, ambao utamsaidia Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo kutengeneza kikosi chake kama alivyoagiza.
“Ni muhimu sana kuwa na mchezo wa kirafiki katika tarehe hizi za FIFA, tunaimani kuwa tutapata timu ya kucheza na Taifa Stars lakini sasa itatoka kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki, ambapo kuna uwezekano tukacheza na Uganda,“ alisema Mwakalebela.
Alisema muda uliobaki ni mdogo sana lakini TFF, itafanya kila linalowezekana ili kupata timu itakayocheza na Taifa Stars.
Wakati huo huo Mwakalebela alisema kuwa TFF, imepeta hasara ya Sh. milioni 11 kutokana na timu ya Taifa ya Malawi kuwapa taarifa ya kushtukiza ya kugoma kuja nchini.
Alisema TFF, ilikuwa imeshalipa tiketi za ndege kwenye Shiriki la Ndege la Malawi kwa ajili ya ujio wa timu hiyo pamoja na kulipia gharama za hoteli.
“Wametutia hasara ya Sh. milioni 11 katika milioni 15 tulizotumia, tulikuwa tumeshawalipia tiketi za kuja nhini pamoja na gharama za hoteli ambayo wangefikia, tunachofanya kwa wakati huu ni kuongea na Shirika la Ndege la Malawi ili waangalie ni jinsi gani watatupunguzia gharama,“ alisema Mwakalebela.
Aidha, alisema timu hiyo itaendelea kuwepo kambini kama ilivyopangwa, ambapo mara baada ya mchezo wao wa kirafiki kambi itavunjwa hadi mwishoni mwa mwezi Machi timu hiyo itakapoitwa tena.
Comments
Loading…